Gamondi aandika rekodi ya kipekee Bongo, mwenyewe ataja siri

BAADA ya kuandika rekodi akiwa na Yanga kwa kuipeleka makundi ya michuano ya CAF ikiwa imepita miaka 25 akiinoa timu hiyo katika msimu wake wa kwanza, kocha Miguel Gamondi amerudia tena akiivusha Singida Black Stars katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Misimu miwili iliyopita Gamondi aliivusha Yanga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuitoa El Merrikh ya Sudan kwa mabao 3-0 kabla ya kurejea tena kuipeleka makundi ya michuano hiyo msimu uliopita kisha kusitishiwa mkataba Jangwani.

Yanga iliachana na Gamondi baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC na Tabora United (sasa TRA United), licha ya kuiongoza katika mechi nane mfululìzo za ligi hiyo bila kupoteza wala kuruhusu bao.

Safari hii amerejea nchini kuinoa Singida BS na kuivusha makundi ya Kombe la Shirikisho ikiwa ni msimu wa tatu mfululizo kwa kocha hiyo, lakini kwa mara ya kwanza Singida katika historia baada ya kuitoa Flambeau de Centre ya Burundi.

SINGI 01

Gamondi pia ameipa tu hiyo taji la Kombe la Kagame 2025 kwa kuinyuka Al Hilal ya Sudan na kuifanya kuwa timu ya nne ya Tanzania kubeba ubingwa huo wa Klabu Bingwa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati baada ya Simba iliyobeba mara sita, Yanga iliyotwaa mara tano na Azam FC iliyonyakua mara mbili.

Kwa sasa Gamondi anasubiri kujua timu hiyo anayoinoa itaangukia kundi gani mara itakapofanyika droo ya makundi Novemba 3 jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Singida imeungana na Azam kutinga makundi ya Shirikisho Afrika sambamba na Yanga na Simba iliyopenya kwa mara ya sita mfululizo katika makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na yanga iliyopenya kwa mara ya nne mfululizo kwa michuano yote ya CAF mbali ya ile ya mwaka 1998 ilipocheza Ligi ya Mabingwa mwaka mmoja tu mara michuano ilipobadilishwa kutoka kuwa Klabu Bingwa Afrika mnamo 1997.

SINGI 02

Kocha Gamondi amesema ni historia nzuri kwake baada ya kutwaa Kombe la Kagame na sasa ameipeleka Singida Black Stars katika hatua ya makundi ya CAF na anafuraha sana kuwa sehemu ya hayo mafanikio akiwapongeza wachezaji, benchi la ufundi na uongozi kwa kumuamini.

“Nina furaha sana ni rekodi nzuri soka la Tanzania linazidi kukua kila mmoja anaona, shirikisho la soka na nchi kwa ujumla, sote tuna kila sababu ya kufurahia mafanikio haya, ni rekodi,” amesema na kuongeza;

“Asante wana Singida kwa kuniamini lakini pia pongezi nyingi kwa wachezaji kwa kuheshimisha nembo ya Singida Black Stars. Bado tuna nafasi zaidi ya kuweka rekodi. Ushirikiano wa kutosha ndio utatupa matokeo zaidi.”

Akizungumzia binafsi kufika mafanikio hayo anaamini uwekezaji, kusajili wachezaji bora wenye uzoefu na wenye hali ya ushindani ndio vitu pekee vimekuwa vikimpa matokeo mazuri.

“Nafurahi kuwa sehemu ya mafanikio ya timu nyingi sio kitu kibaya, uwekezaji mzuri ndio tija ya mafanikio narahisishiwa mambo mengi na ubora wa wachezaji.”