Mrundi Fountain Gate aanza kutamba

BEKI wa kati wa Fountain Gate, Mrundi Derrick Mukombozi, amesema kwa sasa timu hiyo inaanza taratibu kujipata kutokana na mwanzo mbaya walioanza nao, ingawa bado wana kazi kubwa ya kufanya kuendeleza kiwango bora kwa sababu ya ushindani.

Kauli ya nyota huyo inajiri baada ya juzi kuibuka na ushindi wa bao 1-0, dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Manyara, ukiwa ni wa pili msimu huu, kufuatia kuchapwa mechi tatu za kwanza za Ligi mfululizo na kutoka sare mmoja tu.

“Taratibu tunaanza kujipata kwa sababu kama unavyojua tulianza vibaya msimu huu, hali ya ushindi kwetu inatuongezea sana morali ya kuzidi kupambana, bado hatujafikia kule tunapohitaji ingawa kuna mwanga unaanza kuonekana,” amesema Mukombozi.

Akizungumzia kiwango chake tangu ajiunge na timu hiyo msimu huu, Mukombozi amesema kadri anavyoendelea kucheza ndivyo anavyozoeana na wenzake, japo hadi sasa hakuna changamoto yoyote kutokana na kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza.

MUKO 01

Nyota huyo amejiunga na Fountain Gate akitokea Namungo aliyoitumikia kwa mkataba wa miezi sita tangu alipoondoka msimu wa 2023-24, ambapo alijiunga na ‘Wauaji wa Kusini’ kwa mara ya kwanza Agosti 24, 2023, akitokea Nkana FC ya Zambia.

Kwa msimu wa 2023-2024, beki huyo alifunga mabao manne ya Ligi Kuu Bara, ingawa kwa msimu wa 2024-2025, alitupia moja tu katika ushindi wa kikosi hicho wa 2-1, dhidi ya Mashujaa, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Aprili 20, 2025.

Beki huyo licha ya kuichezea Nkana na Namungo ya Tanzania, timu nyingine alizowahi kuzichezea ni Prisons Leopards ya Zambia na LLB Academic ya kwao Burundi, akitazamiwa kuongeza nguvu katika kikosi hicho kutokana na uzoefu wake mkubwa.

MUKO 02

Timu hiyo hadi sasa imecheza mechi sita za Ligi Kuu Bara, ikianza kwa kufungwa bao 1-0 na Mbeya City, Septemba 18, 2025, ikachapwa mabao 3-0 na Simba, Septemba 25, 2025 na kisha kulala 2-0 dhidi ya ‘Wakata Miwa’ Mtibwa Sugar, Septemba 28, 2025.

Baada ya hapo kikosi hicho kikashinda bao 1-0, dhidi ya Dodoma Jiji, Oktoba 17, kikiwa nyumbani, kikatoa sare ya bao 1-1 na Coastal Union Oktoba 22, kisha Oktoba 25, kushinda 1-0, mbele ya KMC na kushika nafasi ya tano kikiwa na pointi saba.