Mwalimu aapa kupunguza umaskini, gharama za maisha

Dar es Salaam. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu amesema chama hicho kina dhamira njema ya kupambana na umaskini pamoja na kuwapunguzia wananchi mzigo wa gharama za maisha.

Mwalimu aliyasema hayo jana Oktoba 26, 2025 katika kampeni zake za lala salama ya zilizofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Tandale, Jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam.

Amesema amedhamiria kutatua kero za wananchi kwa sababu Chaumma ina mipango mizuri ya kuondoa mzigo huo kwa Watanzania.

“Tunakwenda kupiga kura Oktoba 29, ahadi yangu iko palepale, kwenda kukabiliana na umaskini wa kipato na umasikini wa maisha. Leo, gharama za mapambo, chakula, usafiri, kodi ziko juu wakati uwezo wa kuingiza kipato bado ni mdogo kwetu.

“Naomba mniamini ndugu zangu kwenda kupunguza gharama za maisha, inawezekana, uchumi una mambo mawili tu, upatikanaji wa huduma na vitu vinavyohitajika,” amesema mgombea huyo.

Mwalimu amesema  watu wanapigania bidhaa kwa sababu zilizopo ni kidogo na kueleza kama waliopo madarakani wangeamua kundoa gharama za uzalishaji, Tanzania ingekuwa na uwezo wa kuilisha dunia nzima.

“Leo tunanunua kilo ya sukari kwa Sh3,000 wakati tuna ardhi ya kutosha kulima miwa lakini tunaambiwa hadi iingizwe kutoka nje.

“Pia, tani 300,000 za mafuta ya kula zinaingizwa nchini na kulipiwa kodi na gharama zingine na wakati hayo yanafanyika, nchi hii kuna alizeti zinaoza, tuna pamba zinazozalisha mafuta na tuna ufuta unaozalisha mafuta,” amesema Mwalimu.

Amesisitiza kwamba, Chaumma wanakwenda kuirudisha nchi kwenye kilimo cha kutosha na hakitasimama chenyewe, kitaunganisha na viwanda vidogovidogo na hawataagiza sukari kutoka nje wala mafuta.

Kutokana na mipango hiyo waliyonayo, Mwalimu amesema akiingia madarakani, ndani ya miezi sita ya kwanza gharama za maisha ndani zitakuwa zimeshuka.

Kuhusu umaskini wa maisha

Akizungumza kuhusu umaskini wa maisha, amesema gharama za vifaa vya ujenzi zimekuwa juu, hali inayowafanya Watanzania kushindwa kujenga hata nyumba ya chumba kimoja na ukiuliza unaambiwa kodi.

Amesema hilo linatokea wakati nchi ina viwanda vingi vya saruji na huko mkoani Njombe kumejaa mbao, bado kuna mawe ya kutosha katika mikoa mbalimbali nchini.

“Watanzania tunashindwa kuwa na nyumba nzuri kwa sababu ya vifaa vya ujenzi kuwa bei juu na tukiendelea kuwachekea walio madarakani tutaendelea kulia na kodi za nyumba za kupanga.

“Ndiyo maana leo familia zimeng’ang’ania kukaa kwao, nyumba moja hata pale anapopata watoto anaendelea kukaa hapohapo na nyumba ya familia moja inageuka kuwa shule kutokana na kuwa na watu wengi ndani.

 “Inasikitisha leo mbao ya Njombe inapelekwa China inarudishwa hapa ikiuzwa kama samani tena kwa bei juu wakati mbao ni ya kwetu, hii ni ajabu sana,” amesema Mwalimu.

Wakati Oktoba 29 2025 ikiwa ndio siku ya kupiga kura kuwachagua madiwani wabunge na Rais, Mwalimu Chaumma imefunga kampeni zake jana katika Uwanja wa Shule ya Msingi Segerea.

Akizungumzia kufungwa kwa kampeni zake, Mwalimu amesema angependa kuona wafuasi wote wa Chaumma kutoka kona mbalimbali za Dar es Salaam wanaungana pamoja Segerea kuhitisha kampeni hizo zilizodumu siku 60.

“Nasemaje, wao wamelikimbia Jiji, sisi tumezindulia Dar na tumeamua kufungia Dar, hivyo mjitokeze kwa wingi (kesho kutwa),” amesema Mwalimu.

Mgombea ubunge wa Kinondoni, Moza Ally amesema atahakikisha anatoa mchango wake kuhusu upatikanaji wa Katiba mpya akishirikiana na wabunge wengine.

“Mkinipeleka bungeni nitakuwa mmoja wa wabunge watakaoshinikiza kuhusu upatikanaji wa Katiba mpya. Ndugu mnitumie nikawe sauti ya wanaKinondoni, nitakwenda kubanana na Waziri wa Katiba,” amesema Moza.

Moza amesema yeye ndio mgombea atakayewatetea wananchi wanaokabiliwa na kero Kinondoni, ikiwamo changamoto ya maji na upatikanaji wa mikopo ya uhakika kupitia asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.

“Kinondoni mimi ndiyo hazina yetu nitumeni niende bungeni nikawatumikie. Bunge likianza mtaona moto wangu wa kutetea kero zenu.

“Walisema tutakuwa na kampeni za kichovu, lakini mmeona wenye hata muda ukiongezwa nipo vizuri sana,” amesema Moza.