NLD yaahidi kutekeleza Dira 2050

Dar es Salaam. Chama cha National League for Democracy (NLD) kimesema kinakwenda kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Chama hicho kilizindua kampeni zake Septemba 4, 2025 mkoani Tanga, katika viwanja vya Stendi ya Pangani na kuendelea na kampeni hizo kwa mtindo wa nyumba kwa nyumba.

Akizungumzia kampeni hizo juzi, mgombea urais wa Tanzania kupitia NLD, Doyo Hassan Doyo amesema katika kipindi chote amefanya kampeni kwenye mikoa 27 na wilaya 80 nchini.

Amesema katika kampeni hizo, alitumia mbinu ya mgombea na viongozi wengine kuwasiliana kwa karibu na wananchi.

“Mfumo huo wa kampeni za moja kwa moja umewawezesha wananchi kuelezea changamoto zao kwa urahisi, kusikiliza sera za chama kwa utulivu na kushirikiana na mgombea bila usumbufu wowote, jambo ambalo limeongeza ari ya kuimarisha uhusiano wa karibu kati ya viongozi wa chama na wananchi.

Doyo amesema katika siku 60 za kampeni, mbali na kuinadi ilani ya chama hicho iliyobeba tunu ya uzalendo, haki na maendeleo, pia, alijikita katika malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025/50.

“Lengo ni kuhakikisha ahadi na sera za NLD zinazingatia maisha halisi ya Watanzania, zikiwa na msingi wa kupunguza gharama za matumizi katika sekta za umma, kuhakikisha uwajibikaji, uadilifu na uwiano katika maendeleo ya kila eneo, kwa kuzingatia Dira ya Taifa,” amesema.

Katika kampeni hizo, Doyo ameahidi mambo mbalimbali ikiwamo kuwekeza katika kilimo na uvuvi kwa kujenga viwanda vya usindikaji wa samaki na vyakula, kununua meli za kisasa za uvuvi na kuimarisha kilimo cha mazao yanayohitaji uwekezaji mkubwa kama parachichi, machungwa, mahindi, korosho, pamba, mbaazi na mkonge.

“Ahadi hizi zinalenga kuongeza ajira, kipato na tija, huku wakulima na wavuvi wakipewa fursa ya kuuza mazao yao kwa haki katika soko huru, sambamba na kuongeza thamani ya mazao yao,” amesema.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii, siasa na uhusiano ya umma, Ombe Kilonzo amesema katika mikoa tofauti, ahadi za mgombea huyo zilihusisha utatuzi wa migogoro kati ya wakulima na wafugaji, fidia kwa waathirika wa uharibifu wa mali na kuhakikisha soko la mazao linapatikana.

“Alipokuwa mkoani Tanga, aliahidi kuwekeza katika viwanda vya kuchakata na kusindika samaki sambamba na ununuzi wa meli kubwa zenye uwezo wa kuchakata na kusindika samaki sanjari na kuimarisha kilimo cha mkonge na machungwa.

“Lengo kuu ni kuongeza tija katika sekta za uvuvi na kilimo, kupunguza ulanguzi wa madalali kwa kuhakikisha miundombinu inapitika kwa urahisi kuelekea shambani na kuhakikisha wakulima na wavuvi wanapata ajira na kipato cha kutosha,” amesema.

Akichambua kampeni mgombea huyo katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, amesema ahadi za mgombea huyo zilihusu utatuzi wa migogoro kati ya wakulima na wafugaji na kutoa fidia kwa waathirika wa uharibifu wa mali hasa mazao yanayoharibiwa na tembo.

“Hii inaonesha ni kwa namna gani anataka kuimarisha amani ya kijamii, kulinda mali za wananchi na kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo na mifugo,” amesema.