Othman aibua tuhuma mpya kuhusu uchaguzi, ZEC yamuonya

Unguja. Wakati mgombea urais wa Zanzibar kupitia ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman akitoa tuhuma tofauti dhidi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), yenyewe imemuonya kuacha kutoa taarifa za uongo na zinazoashiria kuleta taharuki kwa wananchi.

ZEC imevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua kutoka na kauli zinazotolewa ambazo hazina uthibitisho zikiashiria uvunjifu wa amani wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu utakaotanguliwa na kura ya mapema.

Akizungumza leo Oktoba 27, 2025 na waandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa uchaguzi mkuu na tathmini ya kampeni zake, Othman amesema wamebaini mbinu zote zinazopangwa na ZEC ikiwemo kutangaza matokeo tofauti na yatakayokuwa kwenye vituo vya kupigia kura.

Othman amesema licha ya ubaya wa sheria ya kura ya mapema, Tume ya Uchaguzi imeamua kuongeza ubaya wake kwa kwenda kinyume nayo.

“Kwa sasa imetangaza orodha ya wapiga kura wa mapema ambao kitakwimu ni wengi zaidi kuliko sio tu wale waliotajwa kuruhusiwa na sheria hiyo, bali inazidi wafanyakazi wote wa serikali yote ya Zanzibar na ya Muungano waliopo Zanzibar wakichanganywa,” amesema Othman.

Amesema orodha hiyo ina majina ya makada wa kawaida wa CCM na idadi kubwa ya wageni ambao hawajulikani kwa yale maeneo waliyopangiwa kupiga kura zao.

Kinyume na ubandikaji wa orodha wapiga gura wa kawaida ambao wanaambatana na picha za mpiga kura, amesema orodha hiyo haina picha zilizoambatanishwa.

Pia, Othman amesema wamebaini mbinu za kuwatoa mawakala wa chama hicho kwenye vituo vya kupigia kura.

Kadhalika, Othman amesema pia kuna njama za kupika matokeo na ndio wanayopanga kutangaza tofauti na uhalisia.

“Tuna taarifa za kufutwa uchaguzi kwa baadhi ya majimbo ya kisiwa cha Unguja ambayo tayari wametambua kuwa hawezi kushinda, hadi sasa tuna taarifa za majimbo matano ya Pangawe, Mwanakwerekwe, Kijini, Nungwi na Malindi,” amesema Othman.

Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi

Akijibu tuhuma hizo, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi amesema hakuna tuhuma hata moja ambayo mgombea huyo anaweza kuithibitisha na amemtaka aache kutengeneza taharuki zinazolenga kuvuruga amani.

Amesema kura ya mapema ilianzishwa kutokana ripoti ya waangalizi wa kimataifa walipendekeza iwepo ili kutoa fursa kwa kila mmoja kupiga kura na serikali ilifanyia kazi ripoti hiyo na ndio katayarishwa sheria na kanuni.

“Kuhusu orodha ambayo imewekwa sio ya mtu yeyote bali ni watu wote ambao wameandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura,” amesema

Akizungumzia kuhusu njama za kuwaondoa wakala wa chama hicho kwenye vituo vya kupigia kura, Jaji Kazi amesema sio kweli na lengo la kutoa taarifa hizo za upotoshaji wanajua wenyewe wanataka kuashiria kitu gani, hivyo akasema ni vyema wakalifafanua wananchi wakajua.

Jaji Kazi amesema chama hicho kimekuwa na utaratibu wa kutengeneza matukio mapema na wanajifanya yametokea kumbe zinakuwa ni njama za kuleta taharuki.

“Inasikitisha na aibu kuona kwamba ni mwanasheria na mweledi lakini anatoa taarifa za uongo, kwa kweli hili linasikitisha, kama tungekuwa na lengo hilo tulikuwa na kisu cha kufanya hivyo Septemba 10 wakati wa kurejesha fomu, zilikuwa na kasoro lakini tulimpa muda akamilishe.

“Na hili tungekuwa na nia mbaya ilikuwa sababu ya kumuondoa tena kisheria kwani alikuwa hajatimiza vigezo lakini tulimpa muda tena nje ya ule unaotajwa na sheria, nasikitika kuona tuhuma ambazo lengo lake ni kuleta taharuki,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Ninatoa onyo kwa mgombea huyo kutoa habari za uongo katika kipindi hiki na taarifa hizi tunataka amani, taasisi zichukue hatua na wawe makini kwa taarifa za uongo na za uchochezi ambazo zinaweza kuvunja amani.”

Ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wapuuze taarifa uongo akisema tume itasimamia kwa sheria miongozo, uchaguzi uwe wa haki, uhuru na uadilifu wananchi wajitokeze kumchagua kiongozi wanayemtaka.

Akizungumza kuhusu tathmini ya kampeni zao kwa takribani siku 43, Othman amesema wamekutana na kero tisa ambazo zimeonyesha wananchi wanavyohangaika lakini wakapata matumaini mapya baada ya kueleza sera za chama hicho jinsi wanavyokwenda kuzishughulikia.

“Tumetambua mgogoro mkubwa wa ardhi ambapo watu hawafuati sheria, adha za huduma za hospitali na mfumo wa elimu wa ukandamizaji unaotumika kisiasa,” amesema Othman.

Amesema wamekutana za wafanyabiashara na jinsi wanavyoelemewa na kodi na tozo, wananchi kuishi katika dhiki kubwa na vijana kukata tamaa kwa kukosa ajira na maisha magumu huku Jamii ikiwa na wasiwasi na mporomoko wa maadili.

“Mengi yalikuwa sauti za Wazanzibari ikionesha namna walivyochoshwa na mambo yanayowanyima haki na kutoa dhuluma na uonevu, hivyo wakaonyesha matumaini yao ni kwa ACT Wazalendo.

Baada ya kusikia vilio hivyo, Othman amesema wametoa ahadi ambazo pia zimegusa moja kwa moja nyoyo zao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Mamlaka kamili na kuwa na alama yake yenyewe katika kuimarisha utamaduni na mila za Mzanzibari.

Amesema wameahidi kutoa fursa za ajira kwa usawa na kukuza vipato huku kima cha chini itakuwa ni shilingi milioni moja.

“Kingine ni vita dhidi ya ufisadi na upotevu wa fedha umma na kuondoa wizi wa kura kwani unaondoa uwajibikaji na uadilifu,” amesema Othman.

Amesema watakwenda kuondoa ushuru na tozo katika bidhaa zote za chakula ili Mwananchi apate mlo kamili na aweze kumiliki chakula chake.

Naye Katibu wa Itikadi Uenezi na Habari wa ACT Wazalendo, Salim Bimani amesema wamesimamisha mgombea mwenye uwezo hivyo wanaamini wananchi watampigia kura nyingi bila kuzingatia tofauti zao lengo ni kuinusuru Zanzibar.