Yaoundé. Paul Biya ametangazwa kuwa rais mteule wa Cameroon katika uchaguzi wa urais kwa mara ya nane mfululizo akishinda kwa asilimia 53.66 ya kura zilizopigwa.
Matokeo hayo yametangazwa leo Jumatatu Oktoba 27, 2025 na Baraza la Katiba la nchi hiyo.
Biya amepata ushindi dhidi ya mpinzani wake mkuu, Issa Tchiroma Bakary, aliyepata asilimia 35.2 ya kura.
Tchiroma, ambaye ni waziri wa zamani alikuwa ametangaza ushindi wake binafsi siku mbili baada ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 12, na kuwataka wafuasi wake kuandamana.
Hata hivyo, maandamano hayo yalisababisha machafuko yaliyogharimu maisha ya watu wanne katika jiji la biashara la Douala, ambapo mashuhuda wamesema vikosi vya usalama vilianza kwa kutumia mabomu ya machozi kabla ya kufyatua risasi za moto.
Licha ya kutangazwa kwa matokeo hayo, wafuasi wa Tchiroma wameendelea kudai kuwa walipata ushindi kwa asilimia 54.8 dhidi ya 31.3 za Biya, wakipinga matokeo rasmi ya Baraza la Katiba.
Biya amekuwa madarakani tangu mwaka 1982, na ndiye rais wa pili pekee kuiongoza Cameroon tangu ilipopata uhuru kutoka Ufaransa mwaka 1960.
Aidha, kiongozi huyo anaendelea kuwa rais mkongwe zaidi duniani akiwa na miaka 92 ambapo ushindi huo utamuweka madarakani hadi atakapofikisha miaka 100.
