Dar es Salaam. Wakati ikiwa imebaki saa chache kwa Watanzania kuamua nani awe diwani, mbunge na Rais, vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu vimejinasibu kuibuka na ushindi kutokana na kazi kubwa waliyoifanya kwenye kampeni.
Kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025, zilianza Agosti 28 na zinahitimishwa kesho Jumanne, Oktoba 28 kwa upande wa Tanzania Bara. Zilikuwa siku 61 za vyama kunadi ilani zao kwa njia mbalimbali ikiwemo mikutano na vyombo vya habari.
Wakati Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ikieleza maandalizi yamekamilika, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime katika taarifa yake kwa umma amewahakikishia wananchi kwamba jeshi hilo limejipanga vizuri kumdhibiti yeyote yule kwa mujibu wa sheria atakaye jitokeza ama kwa makusudi au nia ovu kuvunja sheria za nchi ili kuhatarisha amani ya nchi kwa kisingizio chochote kile siku hiyo ya kupiga kura na baada ya kupiga kura.
Pamoja na hayo, baadhi ya huduma mathalani ya usafiri wa mabasi ya mikoani wa kwenda au kurudi Zanzibar –Dar es Salaam zitasimama ili kuruhusu wananchi kwenda kupiga kura.
Uamuzi huo umeelezwa ni sehemu ya mchango wa kampuni za mabasi kuhakikisha abiria na wafanyakazi wake wanatumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura bila vikwazo vya usafiri.
Katikati ya hayo, Ofisi ya Msajili wa Hazina imezitaka taasisi zilizo chini yake kutoa ruhusa kwa wafanyakazi waliojiandikisha nje ya vituo vyao vya kazi ili waushiriki upigaji kura.
Tayari Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza Oktoba 29, 2025 kuwa siku ya mapumziko ili Watanzania milioni 37.6 waliojindikishaji kwenye Daftari la Kudumu la Mpigakura washiriki kikamilifu huku akiwahakikishia usalama.
Mwananchi imezungumza na baadhi ya viongozi wa vyama 17 vilivyosimamisha wagombea urais kuhusu ya siku 60 za kampeni maeneo mbalimbali nchini huku kila mmoja akieleza kilivyofanya mikutano yake na ushindi wa zaidi ya asilimia 50.
Wagombea hao 17 na vyama vyao kwenye mabano ni, Samandito Gombo (CUF), Salum Mwalim (Chaumma), Abdul Mluya (DP), Yustas Rwamugira (TLP), Saum Rashid UDP), Mwajuma Mirambo (UMD), Samia Suluhu Hassan (CCM), na Wilson Peter (ADC).
Wengine ni Twalib Kadege (UPDP), Hassan Almas (NRA), Coaster Kibonde (Makini), Majalio Kyara (SAU), Doyo Hassan (NLD), Daud Mwajojele (CCK), Kunje Ngombale –Mwiru (AAFP), Haji Ambar Khamis (NCCR-Mageuzi), na Georges Busungu wa Ada Tadea.
Wingi wa watu kwenye mikutano yao na wale waliowafuatilia kupitia vyombo vya habari na mitandaoni inawapa jeuri ya kuonesha wanakwenda kuibuka na ushindi. Hata hivyo, wanazuoni wanaeleza wingi wa watu mikutanoni si kigezo cha kuibuka na ushindi.
Katibu Mkuu AAFP, Rashidi Rai amesema chama chao kimefanya mikutano 67 katika mikoa 23, na kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, wamefanikiwa kufikia watu milioni 77, akidai kuwa wamekizidi CCM kwa asilimia kubwa katika kufuatiliwa.
Rai amesisitiza chama chao kinatarajia kushinda uchaguzi wa mwaka huu kwa asilimia 62, ingawa alionya kuwa ikiwa kutakuwa na hila, ushindi wao unaweza kupungua.
ADC kupitia mgombea wake, Wilson Peter amesema amefanya mikutano 91 katika mikoa 26 na kufikiwa na Watanzania milioni 30 moja kwa moja, huku wakisema kuwa milioni 45 walifuatilia kupitia mitandao ya kijamii.
Peter amekadiria aitashinda kwa asilimia 55:“Mikutano yetu kupitia mitandao ya kijamii wamefuatilia watanzania milioni 45 katika mikutano 91 tuliyofanya kwenye mikoa hiyo 26 na matarajio yetu tutashinda kwa asilimia 55.”
Katibu Mkuu wa DP, Abdul Mluya amesema amefanikiwa kuwafikia Watanzania wengi kupitia mikutano 105 katika mikoa 22.
Hata hivyo, amesema hawezi kutaja asilimia kamili ya watu waliomfuatilia lakini alionesha matumaini ya kushinda kwa asilimia 68, akisema ikiwa haki itatendeka.
Mgombea wa UDP, Saum Rashid amesema chama chake kinatarajia kushinda kwa asilimia 88, huku akiongeza kuwa wamefanya mikutano 98 katika mikoa 28 ya Tanzania, na mapokezi ya Watanzania kwa chama chao ni makubwa.
“Tumezunguka mikoa 28 kuna baadhi ya mikoa tulifanya mikutano ya hadhara zaidi ya mitatu, sitaki kusema nilifuatilia na idadi gani ya raia ila wapiga kura nimewafikia,” amesema.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenan Kihongosi, amesema mgombea wa CCM, Samia amefanya mikutano 114 katika mikoa yote ya Tanzania, huku takwimu za mitandao zikionesha amefuatiliwa mara milioni 164.9 na kuthibitisha kukubalika kwake na umaarufu wa chama hicho.
Amesema zaidi ya watu milioni 25.3 walijitokeza kwenye mikutano ya hadhara, na milioni 57.1 walifuatilia kampeni zao kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
“Sisi CCM katika mikutano ya kampeni tumeweka rekodi kubwa ya mahudhurio kuwahi kutokea tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi 1992, watu milioni 25.3 wamehudhuria mikutano yetu ya hadhara, watu milioni 57.1 wamefuatilia kampeni zetu kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ndani na nje ya nchi yetu,” amesema.
Chama cha Makini, kiliongozwa na mgombea urais, Coaster Kibonde, kimesema kimefanya mikutano mingi nchi nzima, na kuahidi ushindi wa asilimia 72.
UPDP, kupitia mgombea wake Twalib Kadege amesema amefanya mikutano mikoani 17 na kuwa anatarajia ushindi mkubwa, lakini ameongeza kuwa ni jukumu la wapigakura kusema ni asilimia gani atapata.
TLP kupitia Katibu Mkuu wake, Bakari Makame amesema matumaini ya chama chao kupata ushindi wa asilimia 90 inawezekana kutokana na mapokezi mazuri ya wananchi katika mikutano yao 96.
Kulingana na maelezo ya Bakari ameongeza mwitikio wa wananchi kwenye vyombo vya habari pia unathibitisha nguvu ya chama hicho kukubalika kupitia sera zao.
Kwa upande wa chama cha NRA, kupitia mgombea wake, Hassan Almas amesema amewafikia Watanzania kwa njia nyingi, akisema kuwa siasa ni mchakato wa imani, na anatarajia ushindi kupitia nguvu ya Mungu na wapigakura.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DSM), Profesa George Kahangwa, amesema asilimia hizo wanazobainisha ni siasa hazina uhalisia wowote huku akisema kuwa na umati mkubwa katika mkutano wako haimaanishi watakupigia kura.
“Wakati mwingine umati mkubwa wa watu kujitokeza hauna uhalisia moja kwa moja kwenye matokeo ya kura, isipokuwa kuna watu wanakuja hawana namna wanakuja kukupa matumaini kama wapo na wewe lakini kura anaenda kupigiwa mwingine,” amesema.
Kulingana na Profesa Kahangwa amefafanua maudhirio ya watu wengi katika mikutano yanaamuliwa na vitu vingi kwanza wapo wanaoenda kwa sababu ya hiyari yao kumsikiliza mgombea, lakini wapo walioshawishiwa kwa kubeba kwenye vyombo vya usafiri.
Amesema makundi makubwa yanaweza kuonesha ni kwa kiwango gani unawafuasi wengi, lakini si lazima wote waliohudhuria watakupigia kura, kwa hiyo huwezi kujihakikishia watakupigia kura.
“Wapo wanaoweza kuamua kumpigia kura mtu mwingine, wapo miongoni mwao hawatapiga kura kwa sababu mbalimbali mathalani hawakujiandikisha au mambo mengine binafsi,” amesema Profesa Kahangwa.
Pia amesema kuna baadhi ya vyama vimekuwa vimeenda kupiga kampeni kwenye masoko na hata kwenye mitandao kuna wanaokuangalia katika kuongeza idadi pekee kuna kuwa hakuna uhalisia.
“Kauli za kushinda asilimia kubwa ni za kisiasa na kwa kuwa wapo kwenye ushindani lazima waseme hivyo, ingawa katika nchi yetu bado mambo ya uchaguzo hajakaa sawa ili kutuwezesha kujua matokeo kwa uwazi,”amesema Profesa Kahangwa.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Abdulkarim Atiki, amesema takwimu hupingwa kwa takwingu ingawa amedai CCM katika mchuano huo haina mshindani wa kweli hivyo uhakika wa kushinda ni mkubwa kwao.
“Matokea kuwa tofauti ni labda wananchi waamue au wawe wamekichukia chama kweli ndipo kura waelekeze sehemu nyingine, lakini ilivyo CCM ni kama Yanga kwenye ligi hawana mshindani wa kushindana naye,”amesema
Si hivyo tu Atiki amesema CCM kina mengi ya kueleza kwa wananchi kwa kuzingatia wapo madarakani kwa muda mrefu na wanaleta huduma za kijamii kwa wananchi hivyo wanaweza kueleza wamefanya mambo gani.
‘Wafanyakazi waruhusiwe’
Katika hatua nyingine, Ofisi ya Msajili wa Hazina imezitaka taasisi zilizo chini yake kutoa ruhusa kwa wafanyakazi waliojiandikisha nje ya vituo vyao vya kazi ili washiriki katika uchaguzi huo.
“Ofisi ya Msajili wa Hazina inaamini kuwa kwa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huu, watumishi wa umma wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha utawala bora, uchumi endelevu na ustawi wa wananchi,” amesema.
Ili kufanikisha hilo, iliwataka wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kuhakikisha watumishi wao wanapatiwa fursa ya kutekeleza haki hiyo muhimu bila kuathiri majukumu yao ya kikazi, kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Wakati Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) ikieleza sababu za baadhi ya kampuni kusitisha safari zake kati ya kesho Oktoba 28 hadi 30, Chama cha Kutetea Abiria kimesema sababu hizo hazina mashiko kwani kila mtu ana shida zake za kijamii, kifamilia,misiba na au ugonjwa.
Baadhi ya kampuni za usafirishaji wa barabara na nyingine za majini zimetangaza kusitisha safari zake kati ya kesho Oktoba 28, hadi 29 na nyingine kwenda hadi Oktoba 30.
Baadhi ya kampuni za mabasi yanayofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, Tarime (Mara), Kilimanjaro, Arusha, Tabora, Mpanda (Katavi), Bukoba, Karagwe (Kagera), Kigoma na baadhi ya mikoa imetangaza kutosafirisha abiria Oktoba 29, siku ambayo Watanzania watapiga kura.
Msemaji wa Taboa, Mustapha Mwalongo amesema huo si msimamo wa Taboa, isipokuwa ni kampuni mojamoja zimeamua kutofanya safari siku hiyo.
“Ni kweli baadhi ya kampuni zimeamua kusitisha safari zake hususani siku ya kupiga kura (Oktoba 29) baadhi ya kampuni zina hofu kwamba abiria watakuwa wachache, hivyo zikaona zisitishe.
“Kama nilivyosema huo si msimamo wa Taboa, ni kampuni moja moja, zipo baadhi zimepunguza ruti, mfano mtu anapeleka gari tano Mbeya, siku hiyo ana hofu kama abiria hawatokuwepo, hivyo anapunguza na kusalia na ruti moja,” amesema.
Amesema wamiliki wa mabasi wanaamini uchache wa abiria siku hiyo, hivyo wamelazimika kupunguza ruti na wengine kusitisha safari ili kutoa mwanya kwa Watanzania kushiriki kikamilifu kupiga kura.
Hata hivyo, Katibu wa Chama cha kutetea abiria, Hashim Omary amesema sababu za wamiliki wa mabasi ni za nidhamu ya uoga ambazo hazina mashiko.
“Huko ni kukiuka sheria za usafirishaji, kwani unaweza usipeleke gari na watu wasipige kura, zingekuwa na mashiko kama Serikali ndiyo ingekuwa imewambia wasitishe, lakini kama ni uamuzi binafsi, hizo ni sababu ambazo hazina mashiko,” amesema.
Amesema kila mtu anaposafiri huwa na sababu zake za msingi, wengine ni za ugonjwa, mwingine anawahi sehemu ambayo hawezi kuacha kwenda.
“Sasa unaachaje kumpeleka kwa sababu ya kupiga kura? Sidhani hata Serikali inaunga mkono hili, hayo ni mawazo yao ya uoga kwamba wataunguza mafuta.
“Kama chama cha kutetea abiria tunaamini siku hiyo abiria wapo kama kawaida, kwani kila mtu ana shida zake za kijamii,kifamilia, misiba wagonjwa, kusitisha safari hakuna mashiko,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Johansen Kahatano alipoulizwa juu ya baadhi ya mabasi kusitisha huduma za usafiri, amesema amezungumza na baadhi ya wamiliki na kujua sababu.
“Mmoja kasema ni sababu ya usalama, lakini tayari polisi walishatoa taarifa kuhakikisha hali ya usalama nchini siku ya uchaguzi hilo sio tatizo, na tumewambia na chama chao kuhusu hilo.
“Baadhi ya wamiliki wamesema wao wataendelea kutoa huduma kama kawaida, hakuna shida, ni wachache sana ambao wamesitisha, lakini ni kwa sababu zao tu,” amesema.
