TANESCO YAANDIKA HISTORIA MPYA MIKOA YA LINDI NA MTWARA; YAWASHA MTAMBO WA KUZALISHA UMEME KWA GESI ASILIA WA MEGAWATI 20

*Uwezo wa uzalishaji umeme wapanda hadi megawati 77.5

*RC Mtwara auzindua mradi na kupongeza Wizara ya Nishati na TANESCO kwa jmageuzi katika sekta ya nishati

Na Mwandishi Wetu

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeandika historia mpya Mikoa ya Lindi na Mtwara baada ya kuzindua rasmi mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wenye uwezo wa megawati 20 katika Kituo cha Mtwara II, Uzinduzi huu ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu na endelevu nchini.

Uwekezaji huu umeongeza uwezo wa kituo hicho kutoka megawati 57.5 hadi kufikia megawati 77.5 na hivyo kulifanya eneo la Kusini liwe na ziada ya umeme kwa mahitaji ya Viwanda, biashara na ajira mpya kwa wananchi kujiajiri katika biashara.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala, ametoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa uwekezaji kwenye miradi ya nishati inayowanufaisha wananchi wa Kusini.

“Tuna kila sababu ya kumpongeza na kumshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuongezea mtambo huu wa kuzalisha umeme. Hii ni hatua muhimu katika kuinua maisha ya wananchi wetu na kuchochea maendeleo ya viwanda katika mikoa ya Lindi na Mtwara,” alisema Mhe. Sawala.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kunatoa fursa kwa wawekezaji kutumia rasilimali ya umeme wa uhakika kujenga viwanda na kuendeleza shughuli za kiuchumi.

“Sasa tuna umeme wa kutosha; ni wakati muafaka kwa wawekezaji kuja kujenga viwanda na miradi ya maendeleo itakayowanufaisha wananchi wetu,” alisisitiza Mhe. Sawala.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Uzalishaji TANESCO, Mhandisi Antony Mbushi, alisema mradi huo ni sehemu ya mpango wa TANESCO wa kuimarisha miundombinu ya uzalishaji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika nchini kote.

“Awali, kituo cha Mtwara kilikuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 50. Sasa tumeongeza megawati 20, hivyo kufikia megawati 77.5 ilhali mahitaji ya juu ya sasa ni megawati 38.5. Hii inatupa uwezo wa kutosheleza mahitaji ya sasa na ya baadaye,” alisema Mhandisi Mbushi.

Ameishukuru pia Serikali kupitia Wizara ya Nishati pamoja na menejimenti ya TANESCO kwa ushirikiano uliofanikisha utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa taifa.

Uzinduzi wa mtambo huo wa gesi asilia unatarajiwa kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mikoa ya Mtwara na Lindi, huku ukitoa matumaini mapya kwa wananchi kupitia upatikanaji wa umeme wa uhakika, wa kisasa na wa kutosha kwa shughuli za uzalishaji, biashara na uwekezaji.