Viongozi wa dini wasisitiza haki, amani kuelekea uchaguzi mkuu

Dar/Mikoani. Zikiwa zimebaki siku mbili Watanzania kupiga kura kuchagua viongozi wawatakao, viongozi wa dini nchini wametoa wito wa haki na amani wakati wa uchaguzi huo huku wakiwahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura.

Jana, Oktoba 26, 2025, ikiwa ni Jumapili ya mwisho kabla ya shughuli ya kupiga kura inayotarajiwa kufanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025, viongozi wa dini wametumia fursa hiyo kutoa mahubiri ya haki na amani kuelekea uchaguzi huo.

Wito huo, ambao umekuwa ukirudiwa mara kwa mara, umesisitizwa zaidi jana kwenye nyumba za ibada, ambapo viongozi wa dini wakiwahamasisha wananchi kulinda amani katika mchakato mzima wa uchaguzi ili taifa liendelee kubaki salama hata baada ya uchaguzi.

Wakati wito wa amani ukisisitizwa, Jeshi la Polisi limetoa hakikisho kwa Watanzania kuwa hali ya usalama imeimarishwa kikamilifu kuelekea uchaguzi huo, ambapo wananchi watatekeleza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kuwachagua Rais, wabunge na madiwani.

Kupitia taarifa iliyotolewa jana, Oktoba 26, 2025, na Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime, wananchi na wageni waliopo nchini wamehakikishiwa utulivu wa hali ya usalama na kutakiwa kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura bila hofu yoyote.

“Hali ya usalama wa nchi ni shwari sana na hakuna tishio lolote la kiusalama linaloweza kufanya shughuli hiyo isifanyike kwa amani,” amesema Misime katika taarifa hiyo.

Jeshi hilo limeeleza kuwa limejipanga vema kuhakikisha kila eneo nchini linabaki salama kabla, wakati, na baada ya uchaguzi, likisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria dhidi ya mtu yeyote atakayejihusisha na uvunjifu wa amani.

“Atakayethubutu kuvunja sheria asilaumu hatua zitakazochukuliwa dhidi yake, kwani elimu imetolewa vya kutosha na kwa muda mrefu,” limesisitiza jeshi hilo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa wananchi wanapaswa kutumia siku hiyo muhimu kwa utulivu, kushiriki katika zoezi la kupiga kura kwa amani na kuepuka taarifa au vitendo vyovyote vinavyoweza kuchochea vurugu au taharuki.

Wakati amani na haki vikiwa ndiyo kiini cha mahubiri ya viongozi wa dini, wengine wamehamasisha Watanzania kujitokeza kupiga kura, kwani ni haki yao ya kikatiba na inawapa fursa ya kuchagua viongozi wawatakao.

Akizungumza kwenye Misa Takatifu ya kilele cha Hija, Nyakijoga huko Bukoba mkoani Kagera, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Jovitus Mwijage, ametoa wito kwa waumini na viongozi wa Serikali kuzingatia sheria kuu ya Mungu (Natural Law) katika mchakato wa kutunga na kutekeleza sheria.

Amesisitiza kwamba ni muhimu kuzingatia mapenzi ya Mungu katika kila hatua wanayochukua ili sheria ziweze kuwa za haki, za kweli, na zisizo na upendeleo.

“Mtuombee tulio na wajibu wa kuongoza, tunapotunga sheria ziendane na sheria kuu ya Mungu, ziwe sheria za haki,” amesema Askofu Mwijage katika ibada hiyo iliyowakusanya waumini wa kanisa hilo kutoka sehemu mbalimbali.

Kwa mujibu wa maelezo ya askofu huyo, ni muhimu kwa viongozi wa kitaifa na wa dini kuzingatia matakwa ya Mungu, badala ya kufuata matashi binafsi au maslahi yao wakati wa kutunga sheria.

“Ziwe sheria zinazotuongoza kwenye ukweli ni muhimu na hili tuliombee kwa viongozi wetu ili waendelee kutunga sheria ambazo zitahakikisha haki, usawa na amani katika taifa letu,” amesema.

Amekumbusha kuwa uongozi wa haki ni kielelezo cha utawala bora na sheria zilizotungwa kwa kufuata mapenzi ya Mungu zitakuwa na manufaa kwa jamii nzima.

Akihubiri katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kijitonyama, Dar es Salaam, katika ibada ya jana, Mchungaji Eliona Kimaro ametoa wito kwa wote wenye sifa za kupiga kura basi wakatekeleze shughuli hiyo ifikapo Oktoba 29, 2025.

“Oktoba 29, 2025 ni siku ya uchaguzi mkuu, siku hii ni ya mapumziko nawakaribisha kwa ajili ya kwenda kupiga kura kwa wale waliojiandaa na waliojiandikisha. Hii ni nchi yetu na hapa ni nyumbani kwetu, hatuna nchi nyingine wala mahala pengine ambapo panafaa sisi kuwepo wala hatuna nyumbani kwengine, hapa ni nyumbani kwetu. Tuibariki, tuiombee, na tuipende nchi yetu,” amesema.

Mchungaji huyo amewaomba na kuwashukuru wale wanaoendelea kuomba kwa ajili ya taifa, huku akisema anafahamu kuna walio kwenye mfungo maalumu ya kuombea nchi, akiwashukuru.

“Nawashukuru wanaoendelea kuomba ili Mungu atuvushe salama, nchi yetu iendelee kuwa na amani, nasi tufanye kazi na kufanikiwa tusipatwe na mabaya,” amesema mchungaji huyo.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Michael Msonganzila, amewataka waumini wa kanisa hilo na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kushiriki uchaguzi Oktoba 29, 2025, huku akisema haki inapaswa kuchukua nafasi kubwa kwani ndio msingi wa kila kitu.

Askofu huyo amesema hayo jana kwenye ibada ya Jubilei ya miaka 10 ya Parokia ya Buhemba, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara, ambapo amesema kupiga kura ni haki ya msingi ya kila Mtanzania mwenye sifa, hivyo kila mmoja anatakiwa kutumia haki yake hiyo.

Amesema msingi wa amani, utulivu, na umoja ni haki, hivyo suala la haki linapaswa kupewa kipaumbele kwa kuzingatia heshima na utu wa mtu bila kujali tofauti zozote zilizopo, ikiwepo ya kijinsia, dini, rangi, kabila, na vingine vingi.

Askofu Msonganzila amesema Watanzania wanapaswa kuzingatia umuhimu wa amani, utulivu, na mshikamano, huku akisema kila mmoja anapaswa kurudi nyumbani mara baada ya kupiga kura na wala wasiwe chanzo cha fujo ama vurugu kwenye vituo vya kupigia kura.

“Kwa wale ambao tuko wengi nyumbani, basi msiende kwa pamoja kwenye vituo, pishaneni wakati wengine wanakwenda, wengine wabaki nyumbani ili wa kwanza wakirudi, wengine pia mnakwenda, na kamwe tusifanye fujo kwenye vituo vya kupigia kura,” amesema.

Wakati huohuo, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuber Bin Ally, amesema suala la viongozi wa dini kuhimiza amani linafanyika siyo kwa shinikizo la mtu yeyote, bali ni kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa vitabu takatifu.

Sheikh Zuber ameyasema hayo Oktoba 25, 2025, jijini Dar es Salaam, katika kongamano la kuliombea Taifa lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini ya kiislamu.

Amesema suala la kuhamasisha na kuilinda amani ni amri toka kwa Mungu ambayo kila mwanadamu anapaswa kuitekeleza.

“Niendelee kusisitiza kuwa suala la kuzungumzia amani ni wajibu wa kila muumini, wanazuoni, masheikh, kwa mujibu wa vitabu vya Mwenyezi Mungu,” amesema.

Amewahimiza wananchi inapofika Oktoba 29, kutoka kwenda kupiga kura kwa amani ili kumchagua kiongozi wanayemtaka.

Amewasisitiza pia kwamba baada ya kumaliza kupiga kura warudi majumbani na wengine waendelee na shughuli zao za kila siku.

“Msilifanye jambo la kupiga kura kama ni la ajabu, limeshafanyika hata miaka iliyopita tangu mwaka 1961, basi lifanyike kama ilivyokuwa desturi yetu miaka iliyopita,” amesema.

Amesema kupiga kura ni muhimu kwani ndio huamua mustakabali wa jamii na taifa kwa ujumla katika siku zijazo.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Nurdin Kishki, amesema suala la kuombea taifa siyo uchawa bali ni mafunzo katika uislamu.

Pia, amesisitiza kwamba ni jukumu la kila muumini kuhakikisha anaiombea nchi iendelee kuwa na amani.

“Wanaweza kutokea watu ambao ni wavivu kufikiri kusema tunachokifanya ni uchawa na siyo kitu sahihi, suala la kuiombea nchi limetajwa hata katika vitabu takatifu,” amesema.

Naye Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Alhad, amewakumbusha masheikh kutoa mawaidha yao kwa waumini kwa kuzingatia kizazi kilichopo sasa.

Amewasisitiza wanapotoa mawaidha kwa waumini, kuhakikisha pamoja na kusoma aya na sura mbalimbali katika vitabu vya dini, wawaeleze na mifano halisia iliyotokea katika jamii.

Amesema kwa kutumia mbinu hiyo wataweza kueleweka vizuri na kuona matokeo ya elimu wanayoitoa, hasa katika kizazi cha sasa alichokiita “Kizazi cha Chat GPT.”

“Kizazi tulichonacho ni cha Chat GPT; utamuelimisha sunna na hadithi, akitoka hapo anaingia Chat GPT kuona inakubaliana, ikiwa hivyo sawa ila ikikataa, atakuletea mjadala hadi utatamani kuhama darasa. Sisi, waliofundisha madarasani, hili tunakutana nalo sana,” amesema.