Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), imezitaka taasisi zilizo chini yake kutoa ruhusa kwa wafanyakazi waliojiandikisha nje ya vituo vyao vya kazi ili waweze kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Haya yamesemwa ikiwa zimebaki siku mbili kabla Watanzania kwenda kupiga kura kumchagua Rais, mbunge na diwani atakayewaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 27,2025 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Usimamisi Mashirika ya Kibiashara kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Lightness Mauki wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Mauki amesema ni vyema kuhakikisha watumishi wote wa umma waliopo katika taasisi na mashirika ya umma kote nchini wanatumia haki yao ya msingi ya kikatiba kwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu.
Amesema kupiga kura ni jambo la mabadiliko chanya, yanayowawezesha wananchi kuchagua viongozi wenye maono, uadilifu na uwajibikaji na ushiriki mkubwa wa watumishi wa umma unaonesha mfano wa uzalendo, nidhamu ya kitaifa na uelewa wa majukumu ya kikatiba.
“Ofisi ya msajili wa hazina inaamini kuwa kwa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huu, watumishi wa umma wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha utawala bora, uchumi endelevu na ustawi wa wananchi,” amesema.
Ili kufanikisha hilo, iliwataka wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kuhakikisha watumishi wao wanapatiwa fursa ya kutekeleza haki hiyo muhimu bila kuathiri majukumu yao ya kikazi, kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Amesema Ofisi ya Msajili wa Hazina, ambayo imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina (Madaraka na Majukumu), Sura ya 370, ina jukumu la kusimamia na kuendeleza uwekezaji wa Serikali katika taasisi na mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa au masilahi.
Hili linafanyika wakati ambao tayari Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza Oktoba 29, 2025 kuwa siku ya mapumziko ya kitaifa ili kuwawezesha Watanzania kushiriki katika shughuli ya kupiga kura.
