WAFUGAJI ZAIDI YA MILIONI NNE WAAHIDI KURA ZAO KUZIPELEKA KWA DK.SAMIA OKTOBA 29

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Mwanza

WAKATI ikiwa imebaki siku moja Watanzania kupiga kura Oktoba 29 ,wafugaji zaidi ya milioni 4.26 nchini wameahidi kumpa kura za kishindo mgombea urais kupitia CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani katika miaka minne ya uongozi wake amewafanyia makubwa.

Akizungumza leo Oktoba 27,2025  jijini Mwanza, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CHAWATA), Murida Mshota, amesema  wafugaji hawana sababu ya kubaki nyuma katika uchaguzi huu, kwa kuwa Serikali imeonesha kwa vitendo dhamira ya dhati ya kuwainua wafugaji na  kuondoa changamoto zao.

Amesisitiza kwamba kwa kauli moja wafugaji wameamua katika uchaguzi mkuu mwaka huu kura yao ni kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amefanya mambo makubwa kwa wafugaji  kuliko wakati mwingine wowote.

Akieleza zaidi Mshota amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Dkt. Samia, bajeti ya sekta ya mifugo imeongezeka kutoka Sh bilioni 179 hadi kufikia Sh bilioni 475, hatua aliyoitaja kuwa ni ushahidi wa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali ili kuinua sekta hiyo.

Ameongeza kwa kwaka huu peke yake wameshapewa fedha Sh.bilioni 210 kwa ajili ya kuchanja ng’ombe na Sh bilioni 69 kwa ajili ya majosho 754 katika halmashauri 184 nchini,” alisema Mwenyekiti huyo

Katika hatua nyingine amesema chini ya uongozi wa Dkt. Samia, Tanzania imepiga hatua kubwa katika soko la kimataifa la nyama.Mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 1,700 hadi tani milioni 14, jambo ambalo linatoa fursa kubwa kwa wafugaji kupata masoko ya uhakika.

Aidha amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dk.Samia imehakikisha wafugaji wanapata fursa ya mikopo kupitia taasisi za kifedha, jambo ambalo halikuwepo kabla ya Dkt. Samia kuingia madarakani.

Amefafanua kwamba wakati Dkt. Samia anaingia madarakani, hakuna mfugaji hata mmoja aliyekuwa amepata mkopo. “Kwasasa zaidi ya wafugaji 8,013 wamekopeshwa zaidi ya Sh bilioni 106.9.”

Kuhusu utatuzi wa migogoro, ameeleza moja ya mafanikio makubwa ya Serikali ni kutatua migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima, iliyokuwa ikileta uhasama na machafuko katika baadhi ya maeneo ya nchi.

“Hivi sasa tunaona utulivu mkubwa katika maeneo ambayo zamani kulikuwa na migogoro mikubwa. Mfano mzuri ni Morogoro, ambako kupitia programu ya Tupendane, watu wameunganishwa na sasa wanashirikiana vizuri. Wakulima na wafugaji wanaishi kwa amani.”

Wakati kwa upande wa chanjo na afya ya mifugo hadi sasa zaidi ya ng’ombe milioni saba wamechanjwa, hatua ambayo imeongeza uzalishaji wa maziwa na nyama, na kupunguza vifo vya mifugo kutokana na magonjwa.

Ametumia nafasi hiyo kutoa mwito kwa wafugaji hasa vijana kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi, kwani ndio njia sahihi ya kulinda mafanikio yaliyopatikana.