Afrika yaunganisha nguvu kukomesha udumavu

Arusha. Tatizo la utapiamlo barani Afrika limeendelea kutafutiwa ufumbuzi baada ya kuingiwa makubaliano ya ushirikiano wa utafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia za kidijitali.

Makubaliano hayo yametiwa saini kati ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Afrika (NM-AIST) na Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kusini na Kati (ECSA-HC)  kwa lengo la kushirikiana katika tafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia za kidijitali zitakazo kabiliana na tatizo la utapiamlo na kuimarisha mifumo ya afya barani Afrika.

Kupitia ushirikiano huo wa miaka mitatu, taasisi hizo zinalenga kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu kama njia ya kupata suluhisho endelevu katika kupunguza udumavu na changamoto nyingine za kiafya katika kanda hiyo.

Akizungumza leo Jumanne, Oktoba 28, 2025, jijini Arusha, wakati wa hafla ya utiaji saini, Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Maulilio Kipanyula, amesema kuwa taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2009 na ni kituo cha umahiri katika sayansi, uhandisi, teknolojia na ubunifu.

Profesa Kipanyula ameongeza kuwa NM-AIST inalenga kutengeneza suluhisho za kiteknolojia zinazokabiliana na changamoto za kijamii, ikizingatia umuhimu wa teknolojia katika kuboresha maisha ya jamii na kuendeleza maendeleo barani Afrika.

 “Leo tumesaini makubaliano na ECSA kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika utafiti wa pamoja, ubunifu na usambazaji wa maarifa katika masuala ya afya.

“ Sisi NM-AIST tunajikita kuzalisha teknolojia na kutafuta majawabu ya changamoto zinazokabili jamii zetu,” amesema Profesa Kipanyula.

Ameongeza kuwa kupitia ushirikiano huo, taasisi hizo mbili zitaendeleza tafiti katika mifumo ya afya, uvumbuzi wa afya mtandaoni, na matumizi ya teknolojia mpya za kidijitali ili kuboresha utoaji wa huduma na matokeo ya lishe.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo utaanza mara moja, ukilenga maeneo 10 ya kipaumbele, ikiwemo kukuza teknolojia zinazoibukia kama akili bandia (AI).

Maeneo mengine ni sayansi ya data, ujifunzaji wa mashine  na roboti, yote kwa lengo la kuboresha mifumo ya afya na utoaji wa huduma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ECSA-HC, Dk Ntuli Kapologwe, amesema kuwa makubaliano hayo ya miaka mitatu yanahusisha maeneo kumi ya ushirikiano, ikiwemo kuanzishwa kwa Kituo cha Umahiri cha Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na Utafiti, pamoja na kukuza diplomasia ya sayansi na teknolojia.

 “Pia, tutashirikiana katika tafiti zinazohusu lishe na afya moja (One Health),” amesema Dk Kapologwe.

 “Tunataka utekelezaji uanze mara moja ili kushughulikia changamoto kama udumavu, upungufu wa lishe, magonjwa ya mlipuko na masuala ya afya moja.

“ Lengo letu ni kuhakikisha bara la Afrika linanufaika na matokeo ya tafiti na teknolojia bunifu zinazozalishwa hapa NM-AIST,”.

Kwa upande wake, Profesa Mwemezi Rwiza kutoka Shule ya Sayansi za Vifaa, Nishati, Maji na Mazingira (MEWES), amesema ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha uhusiano wa kitaaluma na kiutafiti kati ya NM-AIST na ECSA-HC.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Lishe Duniani, katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini, zaidi ya  watoto milioni 13 wanakabiliwa na utapiamlo mkali, kati yao milioni nne wana utapiamlo sugu wa kiwango cha juu.