Yamoussoukro/Yaounde. Wakati Rais wa Cameroon, Paul Biya akitangazwa mshindi katika uchaguzi wa Oktoba 12, 2025, mwenzake wa Ivory Coast, Alassane Ouattara naye ametangazwa mshindi huku ghasia zikiibuka nchini humo kupinga ushindi wake.
Viongozi hao wa Afrika Magharibi na Kati, licha ya kupata ushindi huo, wameibua mjadala kwenye nchi zao na kwingineko duniani kutokana na umri wao kuwa mkubwa, wamekaa madarakani kwa muda mrefu huku waking’ang’ana kuendelea.
Licha ya kuongoza kwa muda mrefu, wakosoaji wa viongozi hao wanasema wananchi wa nchi hizo wanakabiliwa na changamoto lukuki zinazosababishwa na rushwa na usimamizi mbovu wa rasilimali kwa manufaa ya wote.
Ushindi wa viongozi hao ulitarajiwa kutokana na ukandamizaji wa wapinzani na mifumo ya uchaguzi inayolalamikiwa na wapinzani kwenye nchi hizo, jambo lililoibua vurugu hasa Ivory Coast baada ya kutangazwa washindi wa uchaguzi.
Kwa mujibu wa Al Jazeera, Tume Huru ya Uchaguzi ya Ivory Coast ilitangaza Jumatatu kwamba Ouattara, mwenye umri wa miaka 83, ameshinda urais muhula wa nne kwa kupata asilimia 89.77 ya kura zilizopigwa.
Wapigakura karibu milioni tisa walikuwa na haki ya kupiga kura Jumamosi iliyopita katika uchaguzi ambao wapinzani wakuu wa Ouattara hawakuruhusiwa kushiriki.
Rais wa zamani, Laurent Gbagbo alipigwa marufuku kutokana na hukumu ya makossa ya jinai, huku Tidjane Thiam, aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya mikopo, Credit Suisse, akitolewa kwa sababu ya kuwa na uraia wa Ufaransa.
Wagombea wengine wanne waliobaki hawakuonekana kuwa na nafasi kubwa, kwani hawakuwa na uungwaji mkono kutoka vyama vikubwa vya siasa, wala uwezo wa kifedha.
Mmoja wao, aliyekuwa Waziri wa Biashara Jean-Louis Billon, ambaye Jumapili alimpongeza Ouattara, amepata asilimia 3.09 ya kura.
Simone Gbagbo, mke wa Rais wa zamani, alipata asilimia 2.42, kwa mujibu wa matokeo yaliyosomwa kwenye televisheni ya taifa na Ibrahime Coulibaly-Kuibiert, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi.
Coulibaly-Kuibiert alisema asilimia 50 ya wapigakura walijitokeza – kiwango sawa na waliojitokeza uchaguzi wa urais wa miaka ya 2010 na 2015, lakini chini ya asilimia 80 waliopiga kura katika duru ya kwanza ya mwaka 2010.
Akiwa anaripoti kutoka mji mkuu Abidjan, mwandishi wa Al Jazeera Ahmed Idris alisema kuwa marufuku ya wagombea wakuu dhidi ya Ouattara pamoja na idadi ndogo ya wapigakura kumempa “ushindi mkubwa kiongozi huyo”.
“Watu wengi wanajiuliza kama huu ni ushindi wa kweli, lakini Tume ya Uchaguzi imesema zaidi ya asilimia 50 ya wapigakura walishiriki, jambo linaloweza kumpa Ouattara uhalali wa kuendesha serikali,” alisema Idris.
Wapinzani wa Ouattara wamemlaumu kwa kuipeleka nchi katika mkondo wa kiimla ambapo yeye mwenyewe huchagua wapinzani wake wa kisiasa.
Wapigakura wengi walijiondoa kushiriki kutokana na hasira juu ya uamuzi wake wa kugombea muhula wa nne mfululizo. Katiba inaruhusu mihula miwili pekee, lakini Ouattara anasema ukomo wake “ulianza upya” baada ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2016.
Wiki chache kabla ya uchaguzi, kulikuwa na maandamano ya hapa na pale kupinga marufuku kwa wagombea muhimu, hali iliyosababisha serikali kupiga marufuku maandamano na kukamata zaidi ya watu 200 kutoka kundi la kampeni la Common Front.
Ahmed Idris, mwandishi wa Al Jazeera, ameripoti kwamba bado haijulikani kama Ouattara ataweza “kuunganisha taifa lililogawanyika sana” na kwamba atahitaji “kufanya kazi ngumu” kuwashawishi wakosoaji wake.
Ouattara, ambaye amewahi kufanya kazi katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki Kuu ya Nchi za Afrika Magharibi, anajivunia mafanikio ya kiuchumi wakati wa utawala wake, ikiwa ni pamoja na ongezeko la uwekezaji wa kigeni, miundombinu iliyoboreshwa, na utulivu wa kisiasa.
Hata hivyo, pengo la kijamii bado ni kubwa na rushwa inaendelea kukithiri.
Nchi hiyo, ambayo ni koloni la zamani la Ufaransa na mzalishaji mkubwa wa kakao duniani, bado inakabiliwa na deni la serikali la takribani asilimia 60 ya Pato la Taifa (GDP), huku kukiwa na upungufu mkubwa katika elimu na huduma za afya.
“Wakosoaji wengi wanasema mafanikio ya kiuchumi hayajawafikia. Wengi bado wanahangaika kulisha familia zao kutokana na gharama kubwa za maisha. Aidha, kuna uhaba wa ajira kwa vijana,” alisema Idris.
Idris alisema Ouattara ameahidi kufanya mageuzi kupunguza tofauti hizo.
“Lakini kama ahadi hizo zitaleta ajira nyingi na utajiri zaidi kwa wananchi, hilo bado halijabainika,” aliongeza.
Huko Cameroon, Biya ambaye ni Rais mwenye umri mkubwa zaidi duniani, akiwa na miaka 92, ameshinda uchaguzi kwa muhula wa nane, kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa Jumatatu.
Hata hivyo, ushindi huo umechochea makabiliano kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa upinzani wanaodai kuwa uchaguzi ulipangwa na ulighushiwa.
Wafuasi wa mgombea wa upinzani, Issa Tchiroma Bakary, wakiwa na zana kama fimbo na mawe, walifunga barabara kwa taka na matairi yanayowaka moto katika mji mkuu wa kibiashara wa Douala.
Polisi walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wamevaa barakoa au kujifunika nyuso zao kwa nguo. Katika maeneo mengine ya jiji hilo, barabara ambazo kwa kawaida hujaa pikipiki zilionekana zikiwa tupu.
Biya, sasa ana mamlaka mpya inayoweza kumwweka madarakani hadi atakapokuwa karibu kufikisha miaka 100. Kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, Biya alisema wananchi “wamempa tena imani ya kuongoza” na akatoa pole kwa walioathiriwa na vurugu hizo.
“Fikra zangu kwanza ziko kwa wote waliopoteza maisha yao bila sababu, pamoja na familia zao, kutokana na machafuko baada ya uchaguzi,” alisema Biya.
Hata hivyo, Serikali imekanusha madai ya upinzani kuhusu dosari kwenye uchaguzi huo.
Matokeo rasmi yaliyotolewa Jumatatu iliyopita, yalionyesha Biya akishinda uchaguzi wa Oktoba 12 kwa asilimia 53.66 dhidi ya asilimia 35.19 alizopata kiongozi wa upinzani, Tchiroma.
Tchiroma alikuwa ametangaza ushindi wake mapema wiki iliyopita na akasema hatakubali matokeo mengine yoyote. Maandamano yalizuka katika miji kadhaa baada ya matokeo ya awali kuonyesha Biya anaelekea kushinda. Serikali iliwataka wananchi kusubiri matokeo rasmi.
Mwishoni mwa wiki, watu wanne waliripotiwa kufariki dunia katika makabiliano na vyombo vya ulinzi na usalama mjini Douala, kwa mujibu wa taarifa za upinzani, kama zilivyoripotiwa na Reuters.
“Tunatarajia machafuko yataongezeka kwani Wacameroon wengi wanakataa matokeo rasmi, na hatuoni Serikali ya Biya ikidumu kwa muda mrefu zaidi,” alisema Francois Conradie, mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka katika taasisi ya Oxford Economics.
Tchiroma, kupitia ukurasa wake wa Facebook, alisema risasi zilifyatuliwa dhidi ya raia karibu na nyumbani kwake katika mji wa Garoua, kaskazini mwa nchi, na kusababisha vifo vya watu wawili.
