Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Usimamizi wa Bidhaa za Afya ya Afrika Kusini (SAHPRA) ikitangaza usajili wa dawa kinga dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na kuifanya Afrika Kusini kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuidhinisha sindano hiyo inayotolewa mara mbili kwa mwaka, Tanzania imetaja hatua iliyopo kuifikia.
Juni 19, 2025, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliidhinisha dawa hiyo mpya iitwayo Lenacapavir, inayozuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa asilimia 99.9. Dawa hiyo, inayotolewa kwa sindano mara mbili kwa mwaka, ilizinduliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Marekani (FDA) mapema mwaka huu.
Wiki mbili zilizopita, Waziri wa Afya wa Afrika Kusini, Dk Aaron Motsoaledi, alitangaza kuwa nchi yake inapanga kuzindua Lenacapavir ifikapo Machi mwaka 2026.
Waziri Motsoaledi alibainisha kuwa dawa hiyo inaweza kuziba pengo lililopo katika njia za sasa za kuzuia maambukizi ya VVU nchini Afrika Kusini.
SAHPRA ilieleza kuwa mchakato wa mapitio ya dawa hiyo ulifanywa kwa kushirikiana na Shirika la Dawa la Ulaya (EMA) kupitia mpango wa European Medicines for All Procedure (EU-M4all), unaolenga kuharakisha upatikanaji wa dawa muhimu katika masoko nje ya Umoja wa Ulaya.
Kwa mujibu wa SAHPRA, Lenacapavir inatolewa kwa sindano ya chini ya ngozi, ikianza na dozi ya mwanzo pamoja na vidonge vinavyotumika siku ya kwanza na ya pili.
Dawa hiyo inatumiwa na watu wazima na vijana wenye uzito wa angalau kilo 35 ambao hawajaambukizwa VVU, lakini wako katika hatari ya kuambukizwa.
SAHPRA ilisisitiza kuwa matumizi ya Lenacapavir kama kinga kabla ya kuambukizwa (PrEP) yanapaswa kuambatana na matumizi ya kondomu na njia nyingine salama za kujamiiana ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa mengine ya zinaa.
Mkurugenzi Mtendaji wa SAHPRA, Boitumelo Semete-Makokotlela, alisema: “Usajili wa Lenacapavir ni hatua kubwa kwa Taifa lenye viwango vya juu vya maambukizi ya VVU kama Afrika Kusini. Bidhaa hii ni njia bora zaidi ya kuzuia maambukizi hadi sasa.”
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, ili dawa iingie nchini kuna utaratibu maalumu unaotumika, kupitia kamati ya tiba na dawa ya kitaifa.
Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi, amesema kampuni mbalimbali ndizo husajili dawa hizo, kisha huzileta baada ya kuwa zimeidhinishwa na WHO na Global Fund, wakaipitisha dawa itaingia nchini na itatumika.
“Usajili wa dawa ni suala huria, na kiwanda au mtu yeyote anayetaka kufanya biashara ya dawa husika anaruhusiwa kusajili dawa na kuiuza au kusambaza nchini. Hivyo, kama kuna kampuni au mtu yeyote mwenye nia ya kusajili au kuifanyia biashara dawa mpya ya Lenacapavir nchini, anaruhusiwa kufanya hivyo wakati wowote,” amesema Msasi.
Hata hivyo, Msasi amesema ufatiliaji uliofanyika kuhusu dawa hiyo umebaini dozi ya mtu mmoja kuuzwa kwa takribani Sh75 milioni, ambayo mhusika atadungwa kwa miezi 12, hivyo nchi bado inasubiri awamu nyingine kwa sasa.
“Kuna uwezekano wa India kuanza kuzalisha dawa hiyo baadaye, tunaweza kuiingiza maana bei itakuwa imeshuka. Ijapokuwa kwa sasa ni zaidi ya Sh75 milioni, hivyo hauwezi kusajili kitu ambacho hauwezi kumudu. Kama imesogea mpaka Afrika Kusini, mtu anaweza kuinunua akapita nayo mpakani kwa vyeti maalumu, hatazuiliwa kama itakuwa na watumiaji nchini,” amesema Msasi.
Serikali ya Afrika Kusini inapanga kuingiza Lenacapavir kwenye mifumo ya ndani ya ufadhili wa afya ndani ya miaka miwili ijayo.
Gilead na kampuni sita za dawa, ikiwemo moja ya Misri, zitaanza kuzalisha sindano hiyo kwa Dola 40 za Marekani (sawa na Sh98,627) kwa mtu kwa mwaka, ikilinganishwa na bei ya awali ya dola 28,000 (Sh69,039,432), kupunguza gharama kwa zaidi ya mara 700.
Kampuni kama Hetero na mashirika kama The Gates Foundation pia yanashirikiana kuzalisha matoleo ya generic, huku Serikali ikihamasisha uzalishaji wa ndani.
Afrika Kusini ilisajili dawa hiyo Oktoba 21, 2025, ikitambulika kama Lenacapavir 464mg solution injection – Gilead. SAHPRA iliidhinisha Lenacapavir ndani ya siku 65 pekee, haraka zaidi kuliko hata chanjo ya Johnson & Johnson ya COVID-19 iliyoidhinishwa mwaka 2021.
Jinsi Lenacapavir inavyofanya kazi
Virusi vya VVU haviwezi kuishi peke yake, vinahitaji seli za kinga (CD4) ili kujiendeleza. Lenacapavir ni kizuizi cha kapsidi (capsid inhibitor) kinachokatiza ganda la nje la virusi na kufanya virusi kushindwa kuingia ndani ya seli za CD4 na kujizalisha.
Kwa kinga (PrEP), mtu hupokea sindano mbili za Lenacapavir (kila moja 464mg) kila miezi sita. Kwa sababu dawa hutolewa mwilini taratibu, mtu anapopewa sindano ya kwanza anapaswa pia kumeza vidonge vinne (300mg kila kimoja) viwili siku ya kwanza na viwili siku ya pili ili kufikia kiwango kamili cha ulinzi ifikapo siku ya tatu.
Sindano ya pili hutolewa baada ya wiki 24 hadi 26 bila haja ya vidonge tena. Iwapo mtu atachelewa zaidi ya wiki 26, lazima aanze upya.
Madhara madogo yaliyoorodheshwa ni pamoja na maumivu, wekundu au uvimbe katika eneo la sindano, uvimbe mgumu (nodule) au kidonda kidogo kwenye ngozi.
