Fundi ujenzi adaiwa kujinyonga kisa msongo wa mawazo

Njombe. Fundi ujenzi, Henry Mhagama (25) amefariki dunia baada ya kujinyonga ndani ya chumba chake katika mtaa wa Kambarage, Halmashauri ya Mji wa Njombe, mkoani Njombe, chanzo kikidaiwa kuwa ni msongo wa mawazo.

Marehemu inadaiwa kuwa makazi yake ni Kibamba jijini Dar es salaam, lakini huko Kambarage Block X alifika Oktoba 27, 2025 na kufikia kwa mwenyeji wake aliyefahamika kwa jina la Sesko Mng’ong’o.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 28,2025 na Kamanda wa Polisi mkoani Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa.

Amesema kuwa, Oktoba 27, 2025, mwenyeji wa marehemu aliporejea nyumbani kutoka kwenye shughuli zake saa tano kasoro usiku, alijaribu kumpigia simu mara kadhaa bila mafanikio, kwani simu haikupokelewa.

Baada ya kuona hali hiyo, Mng’ong’o alivunja dirisha na kukuta marehemu akiwa amejinyonga kwa kutumia kamba ya manila. Kufuatia tukio hilo, alitoa taarifa kituo cha polisi.

“Lakini sababu kubwa ya kifo hiki nafikiri ni msongo wa mawazo kwa sababu ndani ya shauri lake tumeelezea kwamba amejiua kwa sababu ya dada anayefahamika kwa jina la Astelina,” amesema Banga.

Amewataka wananchi mkoani humo wanapokuwa na jambo lolote wajaribu kushirikisha watu wengine ili kupata mawazo tofauti na kuacha kukaa na vitu moyoni na kupelekea kufanya maamuzi yasiyo sahihi.

Mng’ong’o, ambaye pia ni shemeji wa marehemu Mhagama, amesema kuwa Oktoba 15, 2025, alikabidhiwa Mhagama na dada yake baada ya kupigiwa simu akielezwa kuwa shemeji yake angewasili mkoani humo kwa ajili ya kazi.

Amesema kuwa baada ya Mhagama (marehemu) kuwasili, alimpigia simu na kwenda kumpokea, kisha akampeleka nyumbani ambako alianza kuishi.

Mng’ong’o amesema tangu wakati huo, Mhagama alikuwa akifanya shughuli zake za kila siku na kurejea nyumbani jioni.

Amesema kuwa katika kipindi cha takribani wiki mbili alizokaa naye, hakuwahi kugundua changamoto yoyote kwa Mhagama, kwani walikuwa wakizungumza mara kwa mara na hakuonyesha dalili zozote za kuwa na tatizo.

“Hajawahi kunionyesha dalili yoyote kama ana msongo wa mawazo kwa sababu kila akirudi alikuwa ananichangamkia tunapiga stori,” amesema Mng’ong’o.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kambarage, Francis Msanga, amewasihi wananchi kuepuka kuchukua maamuzi magumu wanapokabiliwa na changamoto, badala yake wawashirikishe watu wengine ili kupata ushauri na msaada wa mawazo mbadala.

“Nilipigiwa simu saa sita usiku kwa kweli linasikitisha sana kila mmoja ameumbwa ili kuishi mtu anapojinyonga au kufa katika kifo ambacho hakijapangwa inasikitisha sana,” amesema Msanga.