UKIACHANA na Misri na Morocco zenye uwezekano wa kuingiza timu nne makundi ya michuano ya CAF ngazi ya klabu msimu huu, hivi sasa unaposoma hapa Tanzania na Algeria pekee ndizo zina rekodi hiyo.
Tanzania imeweka rekodi hiyo kwa mara ya kwanza klabu zake nne zinazoshiriki michuano ya CAF zimefuzu makundi ambapo Yanga na Simba zinacheza Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Azam na Singida Black Stars upande wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Ilizoeleka kuona timu mbili za Tanzania zikifuzu makundi pamoja mara nne ambapo ilikuwa 2020-2021 (Simba na Namungo), kisha 2022-2023, 2023-2024 na 2024-2025 (Simba na Yanga). Safari hii zote nne zilizoshiriki, zimetoboa.
Kwa upande wa Algeria, JS Kabylie na MC Alger zinashiriki Ligi ya Mabingwa, huku CR Belouizdad na USM Alger zipo Kombe la Shirikisho.
Misri na Morocco, timu zao mbili zinasubiri kurudiana katika mtoano kusaka nafasi ya kufuzu makundi, zikifanikiwa, zitaungana na Tanzania na Algeria kuwa nchi pekee kuingiza timu nne hatua hiyo msimu huu wa michuano ya CAF.
Pyramids kutoka Misri ambayo ni bingwa mtetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, inakabiliana na Ethiopian Insurance ya Ethiopia, mechi ya kwanza iliyofanyika Oktoba 26, 2025, ilimalizika kwa sare ya bao 1-1, marudiano ni Novemba 1, 2025 nchini Misri, mshindi wa jumla anafuzu makundi.
Misri tayari imetanguliza timu zake tatu hatua ya makundi ambazo ni Al Ahly (Ligi ya Mabingwa), pia Zamalek na Al Masry (Kombe la Shirikisho).
Morocco nayo inamsikilizia bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, RS Berkane inayokwenda kurudiana na Al Ahli Tripoli kutoka Libya.
Mechi ya kwanza jana Oktoba 26, 2025 iliyochezwa nchini Libya, ilimalizika kwa sarw ya bao 1-1. Marudiano Novemba 1, 2025 nchini Morocco. Mshindi wa jumla anafuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku timu za Morocco zilizofuzu makundi ni AS FAR Rabat (Ligi ya Mabingwa), Wydad AC na Olympique de Safi (Kombe la Shirikisho).
Nchi yenye timu tatu hatua ya makundi CAF ni Afrika Kusini, imeingiza Mamelodi Sundowns (Ligi ya Mabingwa), Stellenbosch na Kaizer Chiefs (Kombe la Shirikisho).
Zambia zipo mbili, Power Dynamos (Ligi ya Mabingwa) na ZESCO United (Kombe la Shirikisho). DR Congo kuna St Eloi Lupopo (Ligi ya Mabingwa) na AS Maniema (Kombe la Shirikisho). Mali zipo Stade Malien (Ligi ya Mabingwa) na Djoliba (Kombe la Shirikisho).
Nchi zilizoingiza timu moja ni Nigeria (Rivers United-Ligi ya Mabingwa), Angola (Petro Luanda-Ligi ya Mabingwa), Tunisia (Esperance-Ligi ya Mabingwa), Sudan (Al Hilal-Ligi ya Mabingwa), Congo (Otoho d’Oyo-Kombe la Shirikisho), Kenya (Nairobi United-Kombe la Shirikisho) na Ivory Coast (San Pedro-Kombe la Shirikisho).