Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake 2025, JKT Queens, imepangwa Kundi B kwenye mashindano hayo baada ya leo Jumatatu Oktoba 27, 2025 kufanyika droo ya makundi hayo iliyochezeshwa makao makuu ya CAF jijini Cairo, Misri.
Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika nchini Misri kuanzia Novemba 8, 2025 hadi Novemba 21, 2025 katika viwanja vya Suez Canal na Right To Dream.
JKT Queens iliyopata nafasi ya kushiriki mashindano hayo baada ya kuwa mabingwa wa CECAFA, katika Kundi B ipo na bingwa mtetezi TP Mazembe (DR Congo), ASEC Mimosas (Ivory Coast) na Gaborone United (Botswana).
Upangaji huo wa makundi ulifanywa na mchezaji wa kimataifa wa Misri, Sarah Essam, na kuashiria rasmi kuanza kwa maandalizi ya msimu huu wa michuano mikubwa zaidi ya klabu za wanawake barani Afrika.
Michuano hiyo itafunguliwa kwa pambano la Kundi A kati ya FC Masar (Misri), iliyomaliza nafasi ya tatu mwaka 2024, na mabingwa wa mwaka 2022, AS FAR (Morocco) katika Uwanja wa Suez Canal uliopo Ismailia.
Pia, timu mbili zitakazoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza, 15 de Agosto (Guinea ya Ikweta) na US FAS Bamako (Mali), ziko katika Kundi A na zinatarajiwa kutoa mchezo wa kuvutia na wenye msisimko.
Kwa mujibu wa CAF, kuna ongezeko la asilimia 52 katika zawadi ya fedha, mwaka huu mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake watapokea Dola za Marekani 600,000 (Sh1.5 bilioni za Tanzania), huku washindi wa pili wakipata Dola za Marekani 400,000 (Sh995.5 milioni za Tanzania).
MAKUNDI LIGI YA MABINGWA AFRIKA WANAWAKE 2025
Kundi A: FC Masar (Misri), AS FAR (Morocco), 15 de Agosto (Guinea ya Ikweta), US FAS Bamako (Mali)
Kundi B: TP Mazembe (DR Congo), ASEC Mimosas (Ivory Coast), Gaborone United (Botswana), JKT Queens (Tanzania)