JWT yatoa wito wafanyabiashara kufunga maduka kushiriki uchaguzi

Dar es Salaam. Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) imetoa wito kwa wafanyabiashara wote nchini kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika kesho, Oktoba 29, 2025, ikisisitiza umuhimu wa amani na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi.

Katika taarifa iliyotolewa leo, Oktoba 28, 2025 na Mwenyekiti wa  JWT, Hamis Livembe imeeleza kuwa siku hiyo ni ya kihistoria kwa Taifa kwa kuwa ni kilele cha demokrasia na utekelezaji wa haki ya kikatiba kwa kila Mtanzania aliyejiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura.

“Tunawahimiza wafanyabiashara wote kote nchini kutumia haki yao ya msingi kwa kwenda kupiga kura kwa amani na utulivu. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha tunachagua viongozi watakaoliletea Taifa letu maendeleo,” amesema Livembe.

Aidha, JWT imewataka wafanyabiashara kufunga biashara zao kesho ili kutoa nafasi kwao na wafanyakazi wao kushiriki kikamilifu katika hatua hiyo muhimu ya kitaifa.

“Tunashauri biashara zote zifungwe kwa siku ya kesho ili kila mmoja apate fursa ya kushiriki, hata hivyo, huduma za msingi kama vile maduka ya dawa, vituo vya afya, migahawa na hoteli zinaweza kuendelea na shughuli zao kama kawaida,” imeeleza taarifa ya jumuiya hiyo.

Pamoja na hayo, JWT imewakumbusha wafanyabiashara wote kuzingatia sheria na taratibu baada ya kupiga kura, ikiwa ni pamoja na kurejea nyumbani  baada ya hatua hiyo ili kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama au kuvunja sheria.

“Tunasisitiza kila mfanyabiashara kujiepusha na vitendo vya uchochezi au jinai,  tusingependa kusikia yoyote miongoni mwetu anakumbwa na changamoto zinazotokana na ukiukaji wa sheria kipindi hiki cha uchaguzi,” amesema.

Jumuiya hiyo pia imewapongeza Watanzania wote kwa maandalizi mazuri kuelekea siku ya uchaguzi na kuwataka kutumia haki yao kwa busara ili kuchagua viongozi bora watakaoliletea Taifa maendeleo endelevu.