Na Mwandishi Wetu
“Kama kuna watanzania wanadai hawaoni sababu ya kumpigia Kura Rais Dk.Samia Suluhu Hassan tarehe 29 Oktoba, mwaka huu, sisi wananchi wa Wilaya ya Kakonko tunazo sababu elfu za kumchagua kwa kura za kishindo ili aendelee kututumikia, aendelee kuijenga wilaya yetu kama alivyotufanyia Kwa hii miaka mitano ya urais wake”.
“Rais Samia ameifanyia mambo mengi mazuri wilaya yetu, ametupatia fedha nyingi katika sekta zote za muhimu, kuanzia afya, elimu, maji, umeme, kilimo, barabara, kwanini tusimchague kiongozi wa nanna hii?.
Haya ni maneno ya Aloyce Kamamba, ambaye alikuwa ni mbunge wa Jimbo la Kakonko mkoani Kigoma aliyemaliza muda wake mwaka huu.
Licha ya kushindwa kuteuliwa kuendelea kuwawakilisha wananchi wa wilaya hiyo katika Bunge lijalo, lakini anasema hana kinyongo na ataendelea kuwa mwaminifu Kwa chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwapigania wagombea wote wa Chama husuaani Rais Dk.Samia ili aendelee kuijenga wilaya ya Kakonko na Tanzania kwa ujumla.
Kamamba anasema Dk. Samia ameitendea mambo makubwa wilaya ya Kakonko kuanzia kwenye huduma za afya, elimu, maji, umeme, kilimo, Barabara, masoko, stendi, na huduma nyingine nyingi.
Akifanya mchanganuo wa miradi iliyotekelezwa katika wilaya yake wakati yeye akiwa mbunge, Kamamba anaanza na sekta ya afya ambapo anabainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Samia amejenga hospitali kubwa ya wilaya ambayo awali haikuwepo, amejenga vituo viwili vya afya katika kata za Gharama na Mgunzu, ametoa fedha jumla ya shilingi milioni 250 kuanza ujenzi wa kituo kingine cha afya cha Rugenge ambako ujenzi inaendelea.
Anaendelea kuchambua miradi ya afya iliyotekelezwa kwa kutaja zahanati mbili zilizopandishwa daraja kuwa vituo vya afya katika kata za Kabare na Mtenderi, zahanati mpya nane zimejengwa na kukamilika na tayari zinatoa huduma Kwa wananchi wa vijijini.
“Rais Dk.Samia,amesaidia kuokoa maisha ya maelfu ya wananchi wa wilaya yetu, ameokoa maisha ya watoto na kina mama wajawazito, ameokoa maisha ya wazee wetu wengi Kwa kuwasogezea huduma za afya, tunamshukuru Sana Rais wetu na tunamhakikishia kuwa hatutamwangusha Oktoba 29, lazima tutiki kwake”, anasisitiza Kamamba.
Kuhusu sekta ya elimu, Kamamba anasema kuwa kipindi cha uongozi wa Rais Samia zimejengwa shule mpya 12 za msingi ambazo zimejengwa vijijini zaidi ili kuwawezesha watoto wengi wa huko kupata elimu kama wenzao wa mjini.
Kwa upande wa elimu ya sekondari, Kamamba anasema katika kipindi cha miaka mitano ya Rais Samia amejenga jumla ya shule tisa za sekondari, ambazo moja ni ya kidato cha sita (High school).
Anazitaja shule hizo kuwa ni Shule ya Sekondari Katanga, Shule ya Sekondari DK. Philipo Mipango, Shule ya Sekondari ya wavulana Kakonko, Shule ya Sekondari ya wasichana ya Amani Mtenderi (High School) na Shule ya Sekondari ya wasichana Kakonko.
Zingine ni Shule ya Sekondari Ikambi, Shule ya Sekondari Luhuru, na Shule ya Sekondari Rutenga, ambazo zimejengwa katika kata mbalimbali husuaani maeneo ya vijijini ili kuwawezesha watoto wa huko hasa wa kike kupata elimu kirahisi.
Kamamba anaongeza kufafanua mafanikio katika sekta ya elimu kuwa ni pamoja na kujengewa chuo cha ufundi stadi cha VETA, na kupelekewa walimu wengi ili kupunguza tatizo la upungufu wa walimu katika Shule za sekondari na msingi.
“Mimi NI mbunge wa nane, kabla yangu wabunge Saba walionitangulia walijenga Shule 12 Tu za sekondari, yaani kuanzia mwaka 1965 mpaka 2020, Mimi nimeanza 2020 mpaka 2025 nimeshawishi serikali kutujengea Shule tisa za sekondari kupitia uongozi wa mama Samia, sasa kwanini nisimpigie kampeni achaguliwe tena ili atuongezee Shule zaidi”, anasisitiza Kamamba.
Katika sekta ya maji, Kamamba anasema serikali ya Rais Samia imekamilisha kupeleka maji katika vijiji vyote 44 vya wilaya ya Kakonko, baada ya kufikisha maji katika vijiji 15 vilivyokuwa havijapata maji mwaka 2020.
Kwa upande wa nishati ya umeme, Kama anasema serikali ya Rais Samia imefanya kazi kubwa sana baada ya kufikisha umeme katika vijiji vyote 35 vilivyokuwa havina nishati hiyo mwaka 2020, kwani wakati huo kulikuwa na umeme katika vijiji tisa tu.
“Pamoja na kwamba bado kuna vitongoji ambavyo havijapata umeme, lakini tunashukuru na kuipongeza serikali ya Rais Samia kwa kufikisha umeme katika vijiji vyote 44 vya wilaya yetu, lazima tuwape maua yao kwakweli kwa kazi nzuri waliotufanyia”, anasema Kamamba.
Aidha, Kamamba anasema serikali ya Rais Samia imewajengea Stendi kubwa na ya kisasa, soko la kisasa, makazi ya Mkuu wa Wilaya (Ikulu ndogo), Ofisi ya kisasa ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi za kisasa za Halmashauri ya wilaya hiyo, Mahakama ya Wilaya, na ukumbi wa mikutano wa kisasa.
Kuhusu mirasi ya kilimo, Kamamba anabainisha kuwa serikali imekarabati skims zote za umwagiliaji wilayani humo. Pia serikali imewapatia maafisa ugani wengi wa mifugo, na wakulima imekuwa ikiwapelekea pembejeo za kilimo kwa wakati.
“Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Rais Samia ametufanyia mengi makubwa na anastahili kupigiwa kura nyingi za ndiyo aendelee kututumikia”, anasisitiza Kamamba.