Kibatala atia mguu sakata la Niffer

Dar es Salaam. Wakati Jeshi la Polisi likikiri kumshikilia mfanyabiashara Jenifer Jovin maarufu Niffer kwa tuhuma za uchochezi, Wakili Peter Kibatala ameibuka na kusema kama mfanyabiashara huyo atapelekwa mahakamani atapata msaada wa kisheria.

Kibatala amebainisha hilo leo Jumanne Oktoba 28, 2025 kupitia ukurasa wake wa Instagram huku akiwataja watu wanaondelea kumpigania Niffer.

“@farajimangula na @adv._mike54lg wamepigana sana kwa ajili yako leo, na bado wanaendelea kupigana. Kama Polisi watakupeleka mahakamani Alhamisi, kama wanavyokusudia kufanya, utakuwa na wawakilishi bora kabisa wa kisheria, nchi nzima inakuombea na inakuwazia,” amesema.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Jumanne Muliro alithibitisha kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo kupitia taarifa yake aliyoitoa kwa umma jana Oktoba 27,2025.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Oktoba 27,2025  saa 9 mchana eneo la Sinza Kumekucha, limemkamata na linamuhoji Jenifer Bilikwiza Jovin miaka 26 mkazi Masaki Peninsula Kinondoni,” taarifa ya polisi ilieleza.

Kulingana na taarifa za jeshi hilo, Niffer anashikiliwa kwa tuhuma za kuhamasisha vurugu na kuharibu miundombinu katika maeneo mbalimbali jijini hasa siku za kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Kamanda Muliro katika taarifa hiyo, alieleza kuwa hatua zaidi za kisheria zinaendelea kuzingatiwa dhidi ya mtuhumiwa.

Kabla ya taarifa hiyo ya Polisi,zilisambaa  taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa mfanyabiashara huyo ametekwa na watu wasiojulikana katika duka lake Sinza jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo leo Mwananchi imetembelea duka na mfanyabiashara huyo Sinza Kumekucha, Dar es Salaam na kukuta limefungwa huku baadhi ya makabati ya kuweka bidhaa yakiwa nje.

Mbali na dukani hapo hata katika saluni yake iliyopo Mwananyamala nayo imepigwa kufuli kuashiria hakuna shughuli zozote zinazoendelea mahali hapo.

Endelea kufuatilia Mwananchi.