Kimbunga Chenge chasambaratika, TMA yasema…

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeeleza kimbunga Chenge  kimepoteza nguvu yake na kusambaratika wakati kikikaribia ukanda wa pwani ya nchi.

Licha ya kusambaratika, TMA imeeleza kuwa mvua na mawingu yaliyokuwa yakiambatana na kimbunga hicho yamesambaa katika maeneo ya ukanda wa pwani hususan katika mikoa ya Lindi, Pwani, Dar es salaam na Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Taarifa ya TMA imeeleza hali hiyo imesababisha vipindi vya mvua katika baadhi ya maeneo hayo.

“Kwa mfano hadi kufika saa 12 jioni ya jana (Oktoba 27), kituo cha hali ya hewa kilichopo uwanja wa ndege wa Julius Nyerere Dar es salaam kiliripoti mvua ya milimita 9.1 kwa kipindi cha saa tisa zilizopita.

“Vilevile katika kipindi hicho, kituo cha hali ya hewa kilichopo katika bandari ya Dar es Salaam kiliripoti mvua ya milimita 3.5.”

“Uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa mabaki ya kimbunga hicho yanatarajiwa kuendelea kusababisha vipindi vichache vya mvua hadi leo Oktoba 28,” imeeleza taarifa ya TMA.

TMA imeeleza vipindi hivyo vya mvua ni kwenye maeneo ya mikoa ya Pwani, Dar es salaam na Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo jirani.

Mamlaka hiyo ya hali ya Hewa imeeleza hakuna madhara makubwa yanayotarajiwa

“Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa mabaki ya kimbunga Chenge na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi,” imeeleza taarifa yake.

TMA pia imetoa ushauri kwa watumiaji wa Bahari na wananchi kwa ujumla kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka TMA pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalamu wa kisekta.