Kura ya mapema yakamilika ikilalamikiwa Zanzibar

Unguja.Kazi ya upigajiwakura ya mapema imefanyika leo Jumanne Oktoba 28, 2025 katika vituo 50 visiwani Zanzibar kwa utulivu na amani licha ya malalamiko katika baadhi ya maeneo.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), upigaji kura ulianza saa 1:00 asubuhi na kumalizika saa 10:00 jioni kwa mujibu wa sheria namba 4 ya mwaka 2018, inayoruhusu watendaji wa Tume na askari wanaotarajiwa kuwa kazini siku ya uchaguzi mkuu, kupiga kura mapema.

Hata hivyo, baadhi ya wagombea wamelalamikia changamoto kadhaa zilizojitokeza katika vituo vya kupigia kura.

Mgombea uwakilishi wa Jimbo la Pangawe kupitia ACT-Wazalendo, Omar Said Shaaban, amesema katika kituo cha Kijitoupele kulikuwa na kasoro ya watendaji kuanza kupiga kura bila kutumia Daftari la Kudumu la Wapigakura.

“Asubuhi watendaji hawakuwa na Daftari, hivyo wapigakura waliruhusiwa kupiga kura bila uhakiki. Nilitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Tume, aliingilia kati na kusimamisha kwa muda upigaji kura hadi Daftari lilipotolewa,” amesema Shaaban, akiongeza kuwa tatizo hilo lilitatuliwa mara moja.

Shaaban ametaja changamoto nyingine kuwa ni malalamiko ya baadhi ya watu wasiokuwa wakazi wa maeneo husika kuruhusiwa kupiga kura.

Naye Mgombea Uwakilishi wa ACT-Wazalendo Jimbo la Malindi, Ali Saleh amedai katika kituo cha Haile Selassie, kulikuwa na wapigakura wengi ambao si wakazi wa eneo hilo.

Hata hivyo, akijibumalalamiko hayo, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi amekiri kuwapo kwa kasoro katika kituo hicho na kufafanua kuwa ilishughulikiwa mara moja.

“Ni kweli watendaji walikuwa wameanza kupigisha kura bila Daftari, lakini tulipoarifiwa tulisimamisha kwa muda, tukaleta daftari na shughuli ikaendelea kwa utaratibu. Tutakutana na watendaji hao kwa ajili ya kuwaelimisha zaidi,” amesema.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji George Joseph Kazi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchakato wa upigaji kura ya mapema. Picha na Jesse Mikofu

Kuhusu madai ya watu wasiokuwa kwenye orodha ya wapigakura kuruhusiwa kupiga kura, Jaji Kazi amesema hilo haliwezekani kwa kuwa orodha ya wapigakura imebandikwa hadharani na kila mpigakura lazima awe amejiandikisha katika daftari hilo.

“Haiwezekani mtu ambaye hayumo kwenye daftari apige kura. Tume inahakikisha kila aliyeorodheshwa ndiye anayepiga kura, na mawakala wanashuhudia kila hatua,” amesisitiza Jaji Kazi.

Aidha, amefafanua kuhusu hoja ya kutowekwa kwa vituo vya kupigia kura ndani ya kambi za jeshi, akieleza kuwa ni kwa mujibu wa sheria.

“Sheria hairuhusu kuendesha shughuli za kisiasa ndani ya kambi za kijeshi. Askari wanapiga kura katika maeneo waliyosajiliwa kama wakazi wa kawaida,” amesema.

Mwisho wa yote, Jaji Kazi aliwahimiza wananchi wa Zanzibar kuendelea kudumisha amani waliyoionyesha wakati wa kura ya mapema na kusubiri matokeo kwa subira, akiahidi kuwa ZEC itatangaza matokeo kwa uwazi, haki na bila upendeleo wowote.

Mwananchi ilizungumza pia na Mgombea Udiwani wa Wadi ya Urusi, Jimbo la Jang’ombe, Ishaka Said Hussein, amesema hali ya usalama imekuwa ya kuridhisha tofauti na chaguzi zilizopita.

“Safari hii hakuna vitisho wala vurugu. Watu wanaendelea na shughuli zao kama kawaida, hakuna dalili za hofu,” amesema Hussein.

Akizungumzia hali ya usalama, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Kazi amesema upigaji wa kura ya mapema umeenda vizuri.

Askari wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiwa kwenye foleni kupiga kura ya mapema katika kituo cha kupigia kura Kijitoupele Jimbo la Pangawe Mkoa wa Mjini Magharibi. Picha na Jesse Mikofu

“Tunashukuru kuona usalama umeimarika na hali ikiwa shwari. Wote waliokuwa kwenye orodha wamepiga kura wamepiga kwa amani. Kila kituo kilikuwa na Daftari la Wapigakura linalotumika na mawakala wote kwa uthibitisho,” amesema Jaji Kazi.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kesho Jumatano, Oktoba 29, 2025, kupiga kura kwa amani na utulivu.