MCHENGERWA AFUNGA KAMPENI KWA KUTOA WITO KWA WANANCHI KUZINGATIA AMANI

Na Yohana Kidaga- Utete, Rufiji

Mgombea wa Ubunge jimbo la Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa amefunga kampeni yake huku akitoa wito wananchi kushiriki kwenye uchaguzi wa kesho kwa amani na kurejea majumbani huku akimwombea kura Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika mkutano wa kufunga kampeni jana kwa jimbo la Rufiji kukiombea kura Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika kesho Oktoba 29, 2025 kwa ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani katika eneo la Utete Mhe. Mchengerwa ambaye pia ni Waziri wa TAMISEMI ametoa wito kwa wananchi wote nchini kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura wakizingatia amani na utulivu katika kipindi cha uchaguzi.

Aidha, amefafanua kuwa wananchi wawaepuke baadhi ya watu wenye nia mbaya ya kuleta fujo kwa kuwa amani ikitoweka watakaopata shida ni watoto, wazee na akina mama ambao hawana hatia.

“Ndugu zangu naomba ieleweke kuwa watanzania hatuna Tanzania nyingine hivyo ni muhimu kuelewa kuwa nchi yetu imejengwa katika misingi ya amani aliyotuachia baba wa taifa Mwalimu Nyerere hivyo hatuna budi kuendelea kutunza amani yetu katika kipindi hiki cha uchaguzi”. Amesisitiza Mhe Mchengerwa 
Aidha, ameeleza kuwa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeleta mapinduzi makubwa nchini ambapo Jimbo la Rufiji limekuwa ni miongoni mwa wanufaika wakubwa.

Ametaja baadhi ya maeneo ambayo Serikali imeboresha kwa jimbo la Rufiji ni kwenye kuleta huduma ya umeme kwenye vijiji vyote na ujenzi madaraja na barabara za kiwango cha lami, huduma ya maji safi na salama, ujenzi wa zahanati na vituo vya afya pia madarasa ya shule za msingi na Sekondari.

Amesema endapo wananchi watampa ridhaa tena ya kuliongoza jimbo hilo atahakikisha anaiomba Serikali kukamilisha kazi kubwa iliyofanyika hususan ya ujenzi wa barabara ya Utete- Nyamwage na ahadi zote zilizo ndani ya Ilani ya CCM.

Mkutano wa kufunga kampeni ulikuwa na vibe Babkubwa kutoka kwa wasanii mbalimbali wa muziki wakiongozwa na msanii anayetamba nchini Mboso, na msanii chipukizi Dogo Pattern aliyechana mistari na kuwaacha wapenzi wa Singeli kuserebuka vilivyo.
Mhe. Mchengerwa ni Mbunge wa tisa wa kuchaguliwa katika jimbo hilo la Rufiji toka lianzishwe na kuongozwa na wabunge kadhaa kuanzia Mhe. Bibi Titi Mohamed ambapo anaelezewa kuwa ni miongoni mwa wabunge walioliletea maendeleo makubwa Jimbo hilo ukilinganisha na wabunge waliotangulia.

Licha ya kuwa Mbunge wa tisa wa Jimbo hilo, Mhe. Mchengerwa ni miongoni mwa wanasiasa wachache nchini ambao wamehudumu kwenye mihimili yote katika nafasi za juu za uandamizi.

Akiwa kwenye mkutano wa kampeni zake alioufanya Ikwiriri, Mgombea wa Urais, mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alimwelezea Mhe Mchengerwa kuwa amefanya kazi nzuri katika Wizara zote nne alizomteua kuhudumu kwenye kipindi chake cha uongozi.