KLABU ya Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro, imetozwa faini ya jumla ya Sh20 milioni kwa kosa la kuanza msimu wa Ligi Kuu Bara na kucheza mechi nne bila kuwa na kocha mkuu mwenye ujuzi kwa mujibu wa Kanuni ya 77:3(1, 2, 3).
Taarifa iliyotolewa leo Oktoba 28, 2025 na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imesema Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya TPLB, katika kikao chake cha Oktoba 27, 2025 baada ya kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya ligi.
“Adhabu hii ya faini Sh5,000,000 (milioni tano) kwa kila mchezo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:19 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu,” imeeleza taarifa hiyo.
Mechi hizo nne ambazo Mtibwa Sugar imecheza bila kuwa na kocha mkuu mwenye ujuzi ni dhidi ya Mashujaa (Septemba 21, 2025), Fountain Gate (Septemba 28, 2025), Coastal Union (Oktoba 19, 2025) na Dodoma Jiji (Oktoba 22, 2025).
Katika mechi hizo, Mtibwa Sugar ilikusanya pointi tano, ikishinda moja, sare mbili na kupoteza moja.
Wakati huohuo, TRA United ya mkoani Tabora nayo imetozwa faini ya jumla ya Sh15 milioni kwa kosa kama hilo, huku ikicheza mechi tatu ambao ni dhidi ya Dodoma Jiji (Septemba 20, 2025), Pamba Jiji (Septemba 28, 2025) na Mashujaa (Oktoba 22, 2025) ambazo zote imetoka sare ikikusanya pointi tatu.
Kanuni ya 47:19 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu, inasema: “Timu yoyote ya Ligi Kuu itakayoanza msimu mpya na kucheza mchezo wa Ligi bila kuwa na kocha mwenye ujuzi kwa kanuni ya 77:(1,2,3) itatozwa faini ya shilingi milioni tano (5,000,000) kwa kila mchezo kwa michezo mpaka sita (6) ya Ligi Kuu, endapo bado itashindwa kutimiza sharti hili la kuwa na kocha anayehitajika kikanuni, itaondolewa kwenye Ligi Kuu na kushushwa daraja.”
Kwa maana hiyo, Mtibwa Sugar ambayo leo Oktoba 28, 2025 ikiwa inacheza mechi ya tano ya ligi dhidi ya Yanga huku ikiendelea kuongozwa na Kocha Awadh Juma ambaye hajakidhi vigezo vya kusimama kama kocha mkuu, imebakiwa na mechi moja dhidi ya KMC itakayochezwa Novemba 25, 2025 kufika sita. Hadi kufikia hapo ikiwa haijakidhi vigezo vya kuwa na kocha mkuu, itashushwa daraja kwa mujibu wa kanuni.
Timu nyingine iliyokumbana na adhabu hiyo kikanuni msimu huu ni Dodoma Jiji baada ya kucheza mechi tatu dhidi ya KMC, TRA United na Coastal Union, ikatozwa faini ya Sh15 milioni, ndipo ikamchukua Aman Josiah.
