Niffer bado ashikiliwa Polisi Dar

Dar es Salaam. Mfanyabiashara Jenifer Jovin, maarufu mitandaoni kama Niffer, bado anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa mahojiano dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Jumanne Muliro amethibitisha kwamba jeshi hilo linaendelea kumshikilia mfanyabiashara huyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, Niffer, aliyetiwa mbaroni jana Oktoba 27, 2025, anakabiliwa na tuhuma za kuhamasisha vurugu na kuharibu miundombinu katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam hasa siku za kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza na Mwananchi leo, Oktoba 28, 2025 kuhusu kinachoendelea baada ya kuhojiwa mfanyabiashara huyo, Muliro amesisitiza ni kama alivyotoa taarifa yake, kwamba bado wanamshikilia.

“Nilishaitolea taarifa tangu jana na ipo kwenye mitandao, hakuna kilichobadilika,” amesema Muliro.

Taarifa hiyo ya jana ilieleza kuwa jeshi hilo Oktoba 27, 2025 saa 9 mchana, eneo la Sinza Kumekucha, lilimkamata na kumuhoji Niffer (26), mkazi Masaki Peninsula, Kinondoni.

Pia, taarifa hiyo ilieleza kuwa hatua zaidi za kisheria zinaendelea kuzingatiwa dhidi ya mtuhumiwa.

Mbali na hilo, Muliro amesema hali ya kiusalama na ulinzi imeimarika ndani ya jiji la Dar es Salaam na  kuwahamasisha wananchi kesho kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba kwenda kupiga kura kumchagua kiongozi wanayemtaka.

“Kifupi maandalizi ni mazuri, wananchi wajitokeze kwa wingi, usalama ni mzuri tena wa kiwango cha juu, hakuna kiashiria chochote cha vurugu, Polisi tuko wengi kuhakikisha wanaoenda kutimiza haki yao ya kikatiba wanakuwa salama na bila uoga wowote,” amesema.