Pipino ajipanga kuuwasha upya | Mwanaspoti

KIUNGO wa KMC, Ahmed Bakari ‘Pipino’ amesema anajisikia vizuri baada ya kurejea uwanjani akitoka kuuguza majeraha ya enka aliyoyapata katika michuano ya Kombe la Kagame iliyofanyika Dar es Salaam kuanzia Septemba 2 hadi 15, mwaka huu.

Wakati wa kuuguza majeraha hayo, Pipino alikosekana katika mechi tatu za Ligi Kuu Bara, lakini sasa amerejea na kucheza mbili, hata hivyo, KMC imekuwa haina matokeo mazuri ikishika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

“Sijauanza msimu vizuri kutokana na kusumbuliwa na enka, lakini tayari nimecheza mechi mbili kwa kupewa dakika chache, naamini nitarejea katika kiwango cha kuipambania timu,” amesema Pipino na kuongeza;

“Natamani kiwango nilichokionyesha msimu uliopita kiwe na muendelezo na siyo kupotea, hivyo nafanya mazoezi kwa bidii, naamini kila kitu kitakaa katika mstari.”

Mbali na hilo, tangu kocha Marcio Maximo, raia wa Brazil ajiunge na KMC, kabla ya Pipino kuumia enka mechi alizocheza alimpanga namba tofauti 8, 10 na 11 ambapo mwenyewe amesema: “Sijajua kocha kaona nini, maana namba ninayocheza ni sita, lakini unapopewa majukumu huna budi kuyafanyia kazi, huenda kocha kaona kitu cha ziada kwangu.”

Tangu arejee uwanjani, Pipino amecheza kwa jumla ya dakika 85 katika mechi mbili dhidi ya Mbeya City (dakika 65) na Fountain Gate (dakika 20).

KMC imekuwa na wakati mbaya msimu huu katika Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mechi tano, ikiburuza mkia ikikusanya pointi tatu kufuatia kushinda mechi 1 na kupoteza 4.