Rais mpya kujulikana ndani ya saa 72

Dar es Salaam. Wakati kampeni za wagombea zikikamilika, hamu ya Watanzania inahamasishwa na kumpata Rais, wabunge na madiwani watakaoibuka na ushindi katika uchaguzi huu.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) tayari imeshaweka wazi kuwa itamtangaza mshindi wa urais ndani ya saa 72 baada ya kukamilika kwa upigaji kura, ikiahidi uwazi, uadilifu na haki katika zoezi hilo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa INEC, Ramadhani Kailima, kupitia vyombo vya habari hivi karibuni.

Kailima alisema tume imejiandaa vyema kuhakikisha wananchi wanapata matokeo kwa wakati.

“Tume imekamilisha maandalizi yote muhimu ya uchaguzi, na tunawahakikishia Watanzania kuwa matokeo ya urais yatatangazwa ndani ya saa 72 baada ya upigaji kura,” alisema Kailima.

Alibainisha kuwa tume imejipanga kuhakikisha uwazi na ufanisi katika kusimamia uchaguzi huru na wa haki.

 “Tume itaratibu ukusanyaji na uhakiki wa matokeo kwa ngazi zote kwa wakati, kuanzia vituo vya majimbo hadi makao makuu, na ndani ya masaa 48 hadi 72 matokeo yatakuwa yametangazwa. Matokeo ya madiwani na wabunge yatatangazwa muda wowote baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika vituoni, tume itapokea matokeo ya urais na kufanya majumuisho kwa muda uliopangwa,” alisema Kailima.

Kauli hiyo imepokelewa kwa hisia chanya na baadhi ya wagombea wa urais na wananchi, ambao wamezungumza na Mwananchi.

 Baadhi wameonesha matumaini makubwa juu ya uadilifu wa tume na maandalizi yake ya kutoa matokeo kwa wakati.

Wakati chama tawala CCM kikitoa tathmini ya kufikia wananchi zaidi ya milioni 57 na kuwa na uhakika wa ushindi, baadhi ya wagombea wa upinzani wamesema saa 72 za INEC zitashuhudia washindi.

Mgombea wa urais wa chama cha United People’s Democratic Party (UPDP), Twalib Kadeghe, amesema ana imani tume itafanya kazi yake kwa haki na muda uliotolewa ni dalili ya maandalizi mazuri.

“Nina imani kubwa na Tume ya Uchaguzi. Kampeni zimekwenda vizuri, tumefika kila kona ya nchi na tumewasilisha sera zetu kwa wananchi. Nina uhakika tutashinda,” amesema Kadeghe.

Mgombea wa urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Samandito Gombo, amesema amefurahishwa na taarifa hiyo na anaamini wananchi wamemuelewa kupitia kampeni alizozifanya kwa muda wa miezi miwili.

“Tumefanya kampeni zenye amani, tumezungumza na wananchi wa kila tabaka na tumeona mapokezi makubwa. Najua wananchi watanipa ridhaa, na naamini ndani ya saa hizo 72 Tume itanitangaza,” amesema Gombo.

Mgombea mwingine, Doyo Hassan Doyo wa Chama cha National League for Democracy (NLD), ameonesha imani yake kwa wapiga kura akijiandaa kutangazwa Rais wa awamu ya saba kupitia muda uliopangwa na tume.

Watanzania nao wamejipanga kupiga kura na kusubiri matokeo kwa shauku. Emmanuel Kasembo, mkazi wa Bagamoyo mkoani Pwani, amesema kampeni zimepita kwa utulivu, ingawa hazikuwa na mvuto mkubwa kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita.

“Mimi nitapiga kura yangu na kisha kusubiri matokeo kama ilivyotangazwa. Ni matumaini yangu Tume itafanya kazi yake kwa haki,” amesema Kasembo.

Taarifa hiyo ya INEC imeongeza hamasa miongoni mwa wapiga kura, huku wachambuzi wakiipongeza hatua ya saa 72 na kupendekeza maboresho ya mifumo ya upigaji kura ili kurahisisha zaidi.

Dk Onesmo Kyauke, mchambuzi wa masuala ya siasa, amesema ni hatua nzuri kidemokrasia, lakini wangeenda mbali zaidi kwa kurahisisha mpigakura kupiga kura mahali popote ndani ya nchi bila kulazimika kwenda alikojiandikisha.

Hayo yanajiri wakati INEC imekamilisha maandalizi yote ya vituo vya kupigia kura na vifaa vyote muhimu vikiripotiwa kufikishwa maeneo yote ya nchi.

 Tume pia imetoa wito kwa vyama vya siasa na wananchi kudumisha amani na kushiriki uchaguzi huo kutimiza haki yao ya kikatiba.

Watanzania sasa wanasubiri kwa hamu saa 72 zijazo, muda utakaotoa majibu ya nani ataongoza taifa kwa miaka mitano ijayo, huku macho yote yakielekezwa kwa INEC, mamlaka iliyopewa jukumu hilo kisheria.