Samia: Tujitokeze kupiga kura, tusibaki kunung’unika mitandaoni

Mwanza. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amehitimisha kampeni za chama hicho huku akiwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kesho Jumatano, Oktoba 29, 2025 kupiga kura.

Samia amesena kukataa viongozi wazembe na kueleza lawama, kebehi na matusi havichagui wala kubadilisha viongozi.

Mbali na ahadi mbalimbali zilizopo kwenye ilani ya chama hicho ya 2025/2030, amesema chama hicho kikipata ridhaa maeneo mengine mahsusi watakayoyapa mkazo wa kipekee ni vita dhidi ya rushwa, utawala bora, maridhiano, upatikanaji wa Katiba mpya na kuwa wataanzisha Tume ya Upatanishi ili kujenga msingi wa umoja wa kitaifa.

Samia ameyasema hayo leo Jumanne Oktoba 28, 2025 alipokuwa akifunga kampeni za chama hicho, katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Amesema wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni haitoshi bali wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kesho kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka.

“Siyo vyema kubaki kujadili na kulalamika mitandaoni wanaofanya maamuzi ya mwelekeo wa nchi yetu ni wale wanaopiga kura na siyo wale wanaonung’unika. Lawama, kebehi na matusi havichagui wala kubadilisha viongozi, kura huchagua na kukataa viongozi wazembe, twendeni kwa wingi wetu tukapige kura,” amesema.

Huku akishangiliwa, Samia amesema:”Serikali imetangaza kesho ni siku ya mapumziko ili kutoa fursa kwa wale wenye sifa kupiga kura kushiriki bila vikwazo, hii ni haki unayoipata siku moja tu ndani ya miaka mitano itumie isikuponyoke.

Vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi hii vinatuhakikishia kuwepo kwa utulivu na amani wakati wote wa uchaguzi na baada ya uchaguzi hivyo tujitokeze kwa wingi na tuhamasishane kwenda kupiga kura.”

“Mkitupa ridhaa yapo maeneo mahususi ambayo tutayapa mkazo wa kipekee ambayo ni vita dhidi ya rushwa na kama mnavyojua kwa kiasi fulani Tanzania tumepanda kwenye kutokuendekeza rushwa tumeachana na mambo ya rushwa na hadhi yetu inapanda polepole,” amesema.

Amesema kwenye utawala bora, maridhiano, hupatikanaji kwa katiba mpya na kulinda mila na desturi za Mtanzania, hayo ni maeneo muhimu kwani yana umuhimu wa kipekee katika ustawi wa taifa na watu wake.

“Maendeleo jumuishi tunayokusudia hayana budi kuendana bega kwa bega na maridhiano, tumedhamiria kwa dhati kuanzisha tume ya upatanishi ili tujenge msingi mmoja wa kitaifa, matarajio yetu ni kwamba mtatukopesha imani yenu ili tuweze kulipa uadilifu na ufanisi katika kutumikia nchi na kustawisha utu wa Mtanzania,” amesema Samia.

Kuhusu vyama vya siasa, mgombea huyo amewapongeza vyama kwa kushiriki kampeni kistaarabu.

“Kwa pamoja tumefanya kazi kubwa kunadi ilani ya CCM, nawashukuru kwa kufanya kampeni za kistaarabu na zilizotawaliwa na hoja na siyo kuzodoana, mmeonyesha njia kwa vyama vingine kuendana na ukomavu wetu wa kidemokrasia.

Vilevile navipongeza vyama vyote vya kisiasa kwa kuendesha kampeni za kiungwana na kushindana kwa hoja, tumeshindana kwenye kujieleza namna tutakavyotekeleza ahadi zetu kwa wananchi wakituchagua na sasa ni wakati wa kushindana kwenye maboksi ya kura,” amesema

“Niombe vyama vya siasa kuwa na utulivu na kuachia wananchi wafanye uamuzi wao wa kupiga kura ni haki yako ili uweze kuweka madarakani viongozi unaoona watakutendea mema,” amesema.

Kwa upande wake, mgombea mwenza wa uais wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi amesema Watanzania wana imani na Samia na kuwa iwapo watachaguliwa atamsaidia kwa uwezo wake wote ili ndoto na maono yake na ilani ya CCM itekelezwe.

“Nikuhakikishie imani uliyoijenga kwangu, namna pekee ninayoweza kuilipa ni kukusaidia kwa nguvu zangu zote na akili zangu zote na kwa uwezo wangu wote ni kukusaidia kwa uaminifu wangu wote ili ndoto na maono yako na ilani ya CCM ifanyike kwa mafanikio makubwa,” amesema Dk Nchimbi.

“Tumezunguza katika nchi yetu kunadi utekelezaji wa ilani, nataka nikwambie kwa dhati Watanzania wameridhika na utekelezaji wa ilani iliyofanywa chini yako. Nikuhakikishie kwa mambo tuliyoongea na wananchi zawadi waliyoahidi kukupa ni ushindi wa kishindo,” amesema.

Dk Nchimbi amesema:”Watanzania wana matumaini makubwa na wewe, wana imani kubwa na wewe, wanajivunia wanaamini hutawaangusha miaka mitano ijayo. Natamani sana baada ya miaka mitano ijayo watakaopita kunadi chama chetu waje wakisema kwa ujasiri kama mimi na wewe tulivyofanya kwa sasa.”

Naye Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira amesema moja ya sifa ya kiongozi bora ni yule anayepambana kuleta mabadiliko katika mazingira magumu.

“Samia amekuwa Rais kwa miaka minne na miezi saba wote tunajua majanga ambayo nchi ilikuwa nayo wakati anaingia madarakani, uchumi wa nchi na dunia ulianguka kutokana na Uviko 19, msiba wa aliyekuwa Rais (Hayati John Magufuli). Samia ametuvusha toka janga la Uviko-19, kuinua uchumi,” amesema.

Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro amesema tangu Samia alipokuwa Rais amekuwa kiongozi wa mfano unaovunja vizingiti na kufungua milango ya fursa kwa wengine na kuwa mlezi wa fursa sawa kwa wanawake na wanaume.

“Historia tutakayoiandika ni ya CCM ni ya Tanzania, ni ndoto ya Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere) ambaye katika uongozi wake aliwahi mara kadhaa kuzungumza na umoja wa wanawake wa Tanu.

Akazungumza juu ya uongozi wa mwanamke. Ni hadithi iliyoanzia Kizimkazi hadi majukwaa ya kimataifa tunaona ndoto ya Mwalimu Julius Nyerere kujenga usawa wa kijinsia ikitimia,” amesema.