Watanzania nchini kote, leo Oktoba 29, 2025, wanashiriki uchaguzi mkuu kwa kupiga kura kuchagua viongozi kwenye nafasi za Rais, wabunge na madiwani watakaokwenda kufanya uamuzi kwa niaba yao.
Uchaguzi huu wa saba tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, unashirikisha wagombea 17 wa urais kutoka vyama tofauti, huku vyama 18 vikisimamisha wagombea ubunge na udiwani katika majimbo na kata sehemu mbalimbali nchini.
Wagombea urais wanaoshiriki uchaguzi huu ni Samia Suluhu Hassan (CCM), Salum Mwalimu (Chaumma), Gombo Samandito Gombo (CUF), Saum Rashid (UDP), Haji Ambar Khamis (NCCR Mageuzi), Yustas Rwamugira (TLP) na Abdul Mluya (DP).
Wengine ni Mwajuma Mirambo (UMD), Twalib Kadege (UPDP), Hassan Almas (NRA), Coaster Kibonde (Makini), Doyo Hassan Doyo (NLD), Majalio Kyara (SAU), David Mwaijojele (CCK), Kunje Ngombare Mwiru (AAFP), Georges Bussungu (Ada-Tadea) na Wilson Elias (ADC).
Miezi miwili ya kampeni, zilizoanza Agosti 28, 2025, imekamilika jana na Watanzania sasa wanakwenda kufanya uamuzi kwa kuwapigia kura wagombea wanaowataka baada ya kusikiliza ilani za vyama vyao pamoja na ahadi walizozitoa.
Katika kipindi hicho, wagombea wameahidi mambo mengi kwa kuzunguka nchi nzima na kuzungumza na wananchi ili kuwashawishi wawape ridhaa ya kuongoza Serikali kwa miaka mitano ijayo.
Ifahamike kwamba sifa za msingi kwa mtu kupiga kura ni lazima; awe raia wa Tanzania, mwenye umri wa miaka 18 au zaidi, awe hajapoteza sifa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani na awe amejiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Kwa mujibu wa INEC, jumla ya wapigakura waliopo katika daftari la kudumu la wapigakura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa leo ni 37,647,235.
Idadi hiyo ya wapigakura ni sawa na ongezeko la asilimia 26.53 kutoka wapigakura 29,754,699 waliokuwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura mwaka 2020.
Vilevile, kati ya wapigakura hao 37,647,235, wapigakura 36,650,932 wapo Tanzania Bara na wapigakura 996,303 wapo Tanzania Zanzibar.
Katika idadi hiyo, wanawake ni 18,950,801 sawa na asilimia 50.34 na wanaume ni 18,696,439 sawa na asilimia 49.66.
Kwa upande wa Zanzibar, idadi ya wapigakura walioandikishwa ni 717,557 ambao jana (katika uchaguzi wa mapema) na leo (uchaguzi mkuu)wanapiga kura kuchagua Rais wa Zanzibar, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wawakilishi, wabunge na madiwani.
Kwa mujibu wa INEC, idadi ya vituo vya kupigia kura katika uchaguzi wa mwaka huu ni 99,895, sawa na ongezeko la asilimia 22.47 ya vituo vya kupigia kura 81,567 vilivyotumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Katika idadi hiyo, vituo vya Tanzania Bara ni 97,348 wakati kwa Tanzania Zanzibar nitakuwa 2,547.
“Tume itavipatia vyama vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, orodha ya vituo vya kupigia kura vya Tume ya Huru ya Taifa ya Uchaguzi vitakavyotumika kwenye uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2025,” anasema Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele.
Wakati wananchi wakienda kupiga kura, ni muhimu kuzingatia kwamba NEC ilifanya marekebisho katika maeneo ya uchaguzi ikiwamo kuzifuta kata 10 pamoja na kutengua na kuwaondoa wagombea udiwani saba.
Jaji Mwambegele alisema katika taarifa yake ya Oktoba 12, 2025, kwamba, uamuzi huo ulifikiwa baada ya tangazo la Serikali Namba 596 na 600 la Oktoba 3, 2025, ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) alitangaza marekebisho ya mipaka ya maeneo ya utawala na kufuta kata kadhaa.
Kwa mujibu wa INEC, kata zilizofutwa ni Litapunga, Kanoge, Katumba, Mishamo, Ilangu, Bulamata, Ipwaga, Milambo, Igombemkulu na Kanindo.
Pia, Tume ilitengua uteuzi na kuwaondoa katika orodha ya wagombea udiwani saba walioteuliwa katika kata husika ambao wote kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM).
Wagombea hao ni Salehe Msompola (Kanoge), Elius Elia (Katumba), Mohamed Asenga (Litapunga), Nicas Nibengo (Bulamata), Sadick Mathew (Ilangu), Rehani Sokota (Ipwaga) na Juma Kansimba (Mishamo).
Taarifa hiyo ilieleza kuwa INEC imelazimika kufuta vituo 292 vya kupigia kura vilivyokuwa kwenye kata zilizofutwa.
“Tume imeanzisha vituo vipya 292 vya kupigia kura katika kata jirani na kata zilizofutwa ili kuwapa nafasi wapigakura kutoka katika maeneo yaliyofutwa,” ilisema INEC.
INEC ilibainisha kuwa wapigakura 106,288 waliokuwa kwenye vituo vilivyofutwa wamehamishiwa kwenye vituo 292 vya kupigia kura vilivyoanzishwa kwenye kata za Mtapenda, Uruwira, Nsimbo na Ugala zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi.
Kata nyingine walizohamishiwa ni Sasu, Ilege, Uyowa, Makingi na Silambo zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mkoa wa Tabora na Kata ya Tongwe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Katavi.
Tume imetoa wito kwa wananchi kuzingatia mabadiliko hayo ya maeneo ya uchaguzi ili waweze kutumia haki yao ya msingi kushiriki kupiga kura siku ya uchaguzi.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wameeleza kwamba wanatarajia kiongozi ajaye atasimamia maslahi yao na kuhakikisha uchumi wa mtu mmoja mmoja unaimarika.
Mkazi wa Tabata, Frank Mwanga amesema anatarajia kuona viongozi watakaochaguliwa watabeba mahitaji ya wananchi hasa kwenye utoaji wa huduma za jamii pamoja na kutengeneza mazingira bora kiuchumi.
“Sisi wananchi tukiwa tumeshiba hatuna shida, hata hizi siasa hatufuatilii. Kwa hiyo, kiongozi ajaye ahakikishe kwamba wananchi wanakuwa na kipato cha uhakika, ajira zitolewe, kila Mtanzania afurahie nchi yake,” amesema.
Kwa upande wake, mkazi wa Mabibo, Hamis Uledi amesema hatarajii mabadiliko yoyote kwani anaamini walioko madarakani sasa, ndiyo haohao wataendelea kuwa madarakani, hivyo wataendeleza mambo yaleyale.
“Tutakwenda kupiga kura lakini sina matarajio makubwa kwa sababu sidhani kama watu watabadilika sana, labda huku chini. Kwa hiyo, tusubiri Tume itutangazie washindi ili maisha yaendelee,” amesema Uledi. Anasisitiza kwamba viongozi watakaochaguliwa wajitahidi kuwasikiliza wananchi kwa kuwa sasa wameamka na wanahoji mambo tofauti na wale wa zamani. Anasisitiza umuhimu wa kutunza amani na umoja wa Watanzania.
Melina Kyendesya, mkazi wa Pugu, amesema anatarajia kwamba nchi itaendelea kubaki na amani hata baada ya uchaguzi kwa sababu amekuwa akisikia mitandaoni baadhi ya watu wakihamasisha vurugu siku ya uchaguzi.
“Kitu kikubwa ninachokiomba sana, uchaguzi upite kwa amani kwa sababu vurugu zikianza madhara yatakuwa makubwa sana. Sisi wengine tuna watoto wadogo, tunahitaji utulivu ili tuwalee kama sisi tulivyolelewa kwenye amani,” anasema mwanamke huyo.
Naye Samson Almasi, mkazi wa Kikuyu jijini Dodoma, anasema anatarajia kwamba uchaguzi utakuwa wa amani kwa sababu ameona namna kampeni zilivyokuwa na utulivu huku vyama vya siasa vikinadi sera zao bila bughudha.
“Naomba vijana wenzangu tuendelee kuwa wavumilivu katika kipindi hiki, tupunguze mihemko ili tuilinde amani. Wagombea wote wanaoshiriki uchaguzi huu, wakubali kuyapokea matokeo na kama hawakutendewa haki, basi wafuate utaratibu kudai haki zao,” anaeleza mfanyabiashara huyo.
Wakizungumzia uchaguzi huu, wachambuzi wa siasa wanaeleza umuhimu wa haki kutendeka kwani kura ni matakwa ya wananchi, hivyo ziheshimiwe na mamlaka zilizopewa dhamana ya kuratibu uchaguzi huu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie amesema demokrasia maana yake ni wananchi wanapewa nguvu ya kuamua kuhusu viongozi wanaowataka, hivyo lazima uamuzi wao uheshimiwe.
“Msisitizo mkubwa ni katika kuheshimu uamuzi wa wananchi, mgombea aliyechaguliwa ndiye atangazwe na wasimamizi. Hiyo itasaidia kudumisha amani kwa kuwa amani inakuja kama kuna haki,” anasema mwanazuoni huyo.
Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa, Benedict Ombeni anawahimiza wananchi kwenda kupiga kura kuchagua viongozi wawatakao kwa sababu ni haki yao ya kikatiba na wanatakiwa kuitumia ipasavyo.
“Pamoja na yote, ni muhimu kutambua kwamba kura yako ni muhimu na ili upate viongozi kuanzia ngazi ya chini, hupaswi kususia kupiga kura. Nenda kachague unayemtaka, hapo utakuwa umetimiza wajibu wako,” anasema mchambuzi huyo wa siasa.
Mgombea urais wa DP, Abdul Mluya, amesema atapiga kura katika Mtaa wa Mtakuja, Kata ya Vingunguti jijini Dar es Salaam, wakati Salum Mwalimu wa Chaumma) akipiga kura Jimbo la Kikwajuni, Mjini Unguja.
Kwa upande wa Swaum Rashid, anayewania urais kwa tiketi ya chama cha UDP, atapiga kura Kata ya Mzinga, Jiji la Dar es Salaam, wakati mgombea urais wa chama cha NRA, Hassan Almas, atapiga kura Chamazi, Mbagala, Dar es Salaam.
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wakulima (AAFP), Kunje Ngombale-Mwiru, atapiga kura Ubungo, Dar es Salaam; Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha NLD, Hassan Doyo atapiga kura Kata ya Kabuku, Kijiji cha Kwedikwazu Mashariki, wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.
Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Richard Lyimo, amesema mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Yustas Rwamugira, atapiga kura katika Kata ya Vingunguti, jijini Dar es Salaam huku Mwenyekiti wa Chama cha Ada-Tadea, Juma Khatib, amesema mgombea urais wa chama hicho, Georges Bussungu, atapiga kura eneo la Ikiguru, Misungwi mkoani Mwanza.
Sambamba na hao, mgombea urais wa Chama Makini, Coaster Kibonde ameliambia Mwananchi kuwa atapiga kura katika kituo cha Shule ya Msingi Miogoni iliyopo Sinza Vatican, wilayani Ubungo, Dar es Salaam. Meneja kampeni wa mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Yusuph Mbungiro, amesema mgombea urais wa chama hicho, Samandito Gombo, atapiga kura eneo la Kitunda, wilayani Ilala, Dar es Salaam.
Kwa upande wa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan atapiga kura Chamwino mkoani Dodoma, kwa kuwa ndilo eneo alikorekebishia taarifa zake za mpigakura Mei 17, mwaka huu.