Dar es Salaam. Mabadiliko ya kiuchumi na kijamii yanayoendelea duniani yameifanya elimu isibaki kama chombo cha kupata maarifa pekee, bali iwe nyenzo ya kumjengea binadamu uwezo wa kuishi, kufikiri na kufanya kazi kwa ufanisi.
Ndiyo maana Tanzania, kupitia mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (toleo la 2023), imeanzisha mtalaa mpya wa elimu ya amali katika shule za sekondari, mkondo unaolenga kumpatia kijana ujuzi wa vitendo mapema ili kuandaa nguvu kazi yenye stadi za kazi, ubunifu na uwezo wa kujitegemea.
Kwa miongo kadhaa, elimu ya Tanzania imekuwa ikilalamikiwa kwa kuandaa wahitimu wasio na stadi za kazi. Wengi wamekuwa wakiishia vyuoni bila kuwa na ujuzi wa vitendo unaohitajika sokoni, hali iliyosababisha tatizo la ajira kukua kwa kasi.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imekuja na suluhisho jipya, kuingiza elimu ya amali katika ngazi ya sekondari.
Elimu hii inatoa fursa kwa wanafunzi kujifunza masomo ya vitendo kama ufundi umeme, useremala, ushonaji, kilimo, ufundi bomba, teknolojia ya magari, mapishi, kompyuta na mengineyo, sambamba na masomo ya kawaida ya kitaaluma.
Lengo kuu la mfumo huu ni kuondoa dhana kwamba mafanikio ni lazima yapitie elimu ya darasani pekee. Badala yake, mfumo huu unahimiza dhana ya “kujifunza kwa kutenda,” ambapo vijana wanapata nafasi ya kutumia mikono yao kujenga ujuzi unaoweza kuwasaidia kuajiriwa au kujiajiri mara tu baada ya kuhitimu.
Hii ni hatua muhimu katika kufikia azma ya taifa la uchumi wa viwanda, kwani mafanikio ya viwanda hayawezi kupatikana bila nguvu kazi yenye ujuzi wa vitendo.
Sambamba na lengo hilo, Serikali imeweka wazi kwamba elimu ya sekondari sasa itakuwa na mikondo miwili; mkondo wa jumla na mkondo wa amali.
Hii inamaanisha kuwa wanafunzi watakuwa na uhuru wa kuchagua aina ya elimu wanayoitaka kulingana na vipaji, uwezo na matarajio yao ya baadaye.
Mfumo huu wa mikondo unakusudia kuondoa tatizo la “mfunge kila mtu njia moja,” kwa kutambua kwamba vijana wana vipaji na uwezo tofauti, hivyo elimu inapaswa kubadilika kulingana na mahitaji ya kila mmoja.
Elimu ya amali kutoua Veta
Katika utekelezaji wake, VETA, NACTVET na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) zimehusishwa kikamilifu katika maandalizi ya mitalaa, utoaji wa mafunzo na usimamizi wa ubora.
Hata hivyo, swali limekuwa likiibuka: je, ujio wa elimu ya amali kwenye shule za sekondari unaweza kuathiri vyuo vya ufundi kama Veta? Au ni hatua ya kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya ufundi stadi nchini?
Kwa mujibu wa Meneja Uhusiano wa Veta, Sitta Peter, ujio wa elimu ya amali haupingani na malengo ya Veta, bali unaongeza fursa za upatikanaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa Watanzania wengi zaidi.
“Kwa miaka yote, Veta imekuwa ikitoa mafunzo ya ufundi kwa vijana waliomaliza darasa la saba na kidato cha nne. Sasa ujio wa elimu ya amali katika shule za sekondari unasaidia kufika kwenye maeneo ambayo Veta hatukuweza kufika awali.
“Tulikuwa na maombi ya zaidi ya milioni moja ya wanaotaka kusoma, lakini uwezo wetu ulikuwa chini ya asilimia 10. Hivyo, mfumo huu mpya unasaidia kusambaza elimu ya ufundi stadi katika eneo kubwa zaidi la nchi yetu,” anasema Peter.
Anabainisha kuwa, mfumo huo unatoa mwanya mkubwa wa kuendeleza ujuzi, kwani wanafunzi wa sekondari wanaomaliza mkondo wa amali bado wanahitaji kujiendeleza katika ngazi nyingine kupitia Veta.
“Wanafunzi wa amali wakimaliza kidato cha nne wanaweza kuja Veta kuongeza levels zao za ujuzi. Hata watu wazima wenye elimu kubwa kama vyuo vikuu, wengi wanarudi kujifunza Veta ili kupata ujuzi wa vitendo kwa ajili ya miradi yao binafsi,” anaongeza.
Veta, kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), imehakikisha mitalaa ya shule za amali inalingana na ile ya vyuo vya ufundi stadi, ili kuwezesha mwendelezo wa kielimu.
“Tumehusika moja kwa moja katika uandaaji wa mitalaa ya amali. Tumetengeneza ulinganifu wa maudhui ya miaka mitatu ya Veta ili yatumiwe kwa miaka minne ya sekondari. Hii inaleta uwiano mzuri wa elimu ya vitendo,” anasema.
Aidha, Veta imekuwa ikishirikiana na shule nyingi za sekondari nchini zenye mkondo wa amali, kwa kuwaruhusu wanafunzi kutumia karakana za vyuo jirani kwa mafunzo ya vitendo, hasa pale shule zinapokosa vifaa vya kutosha.
Kwa upande wa Nactvet, taasisi yenye dhamana ya kusimamia ubora wa elimu ya ufundi stadi, inasema kuanzishwa kwa elimu ya amali ni hatua muhimu katika kukuza ujuzi wa taifa.
“Mkondo wa amali hauzuii wanafunzi kujiunga na vyuo vya ufundi kama Veta, bali unapanua wigo wa upatikanaji wa ujuzi nchini,” anasema Dora Tesha, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko Nacvet.
Anasema mfumo huu unamwezesha kila Mtanzania kujiendeleza kielimu na kitaalamu kwa njia mbalimbali, bila kujali kiwango cha elimu alichonacho.
“Serikali imeweka mfumo nyumbufu unaomruhusu kila mtu kuendelea kujifunza. Lengo ni kuwa na Watanzania wenye maarifa, stadi na mtazamo chanya wa maendeleo,” anasema Tesha.
Anasema Nactvet imeweka mifumo thabiti ya kusimamia ubora wa mitaala na kuhakikisha wahitimu wote wanalingana na mahitaji ya soko la ajira.
“Tunataka kuhakikisha kila mhitimu wa elimu ya amali au ufundi stadi anakuwa na uwezo wa kutenda kazi kwa ubora unaotakiwa na sekta binafsi na za umma,” anaongeza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Nactvet, Bernadeta Ndunguru, anasisitiza kuwa changamoto kubwa iliyobaki ni mitazamo ya wazazi.
“Baadhi ya wazazi bado wana shaka kuhusu mkondo huu wa amali, lakini ukweli ni kwamba huu ndio mkombozi wa tatizo la ukosefu wa ajira. Nilipotembelea shule ya Baobab, nimeona walimu wenye moyo na wanafunzi wenye ari ya kujifunza huu ndio mwelekeo sahihi wa elimu ya leo,” anasisitiza Ndunguru.
Elimu ya amali msingi wa uchumi wa viwanda
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Dk Suleiman Ikomba, anasema elimu ya amali ni kati ya mafanikio makubwa zaidi ya sekta ya elimu hapa nchini, kwani inamjengea kijana stadi za vitendo, ubunifu na uwezo wa kujitegemea.
“Sasa kupitia elimu hii, vijana wetu hawasubiri ajira tena. Wengi wanakuwa wazalishaji wa ajira kwa wengine. Hii ndiyo misingi ya uchumi wa viwanda,” anasema Dk Ikomba.
Anabainisha kuwa hakuna ushindani kati ya sekondari zenye mkondo wa amali na Veta.
“Wanafunzi wanaohitimu sekondari watakuwa tayari wana ujuzi wa msingi, na watakapoingia Veta itakuwa ni mwendelezo wa kujifunza zaidi,” anabainisha.
Hata hivyo, Dk Ikomba anatoa ushauri kwa Serikali kuendelea kuandaa walimu wenye ujuzi wa kufundisha masomo ya amali, kwani walimu wengi bado hawana stadi za kutosha kufundisha fani hizo mpya.
“Kila jambo linaanza hatua kwa hatua. Tunaunga mkono jitihada za Serikali kujenga maabara na karakana mpya. Elimu ya amali ni dira ya mustakabali wa Taifa letu,” anasisitiza.
Maoni kutoka kwa wakufunzi wa Veta Kihonda mkoani Morogoro yanaonyesha mtazamo wa mchanganyiko. Fatma Mrope, mkufunzi wa ufundi, anaona huenda idadi ya wanafunzi wa Veta ikapungua kutokana na wanafunzi wengi kusoma sekondari.
“Wengi watakuwa wanapata mafunzo ya ufundi mapema sekondari, hivyo Veta inaweza kupata wanafunzi wachache. Pia, huenda walimu wa Veta wakaajiriwa kufundisha sekondari kutokana na uhaba wa walimu wa fani hizi,” anasema.
Lakini Ramadhan Ngare, mkufunzi mwingine wa Kihonda, anaamini vinginevyo…. “Elimu ya amali haitaiathiri Veta. Tofauti ni kwamba sisi tunachukua wanafunzi wote waliomaliza msingi, hata wale wasiokuwa na ufaulu. Wengine walioshindwa sekondari bado wanakuja kwetu. Serikali ikituongezea vifaa, tutazalisha wahitimu bora zaidi.’’
Shule za sekondari zaanza kuchanua
Moja ya shule zilizopokea mageuzi haya kwa mikono miwili ni Shule ya Sekondari Baobab, ambapo wanafunzi wa mkondo wa amali wapo tayari kidato cha pili. Mkuu wa shule hiyo, Venance Hongoa, anasema walijiandaa mapema kwa mpango huu.
“Tulikamilisha miundombinu yote na tulikuwa karibu kuanzisha chuo cha Veta, lakini Serikali ilipokuja na mageuzi haya, tulikuwa tayari. Wanafunzi wetu wana mwamko mkubwa na walimu wamejiandaa vizuri,” anasema.
Miongoni mwa wanafunzi hao ni Korie Kipingu, mwanafunzi wa kidato cha kwanza anayesomea ufundi bomba.
“Nimechagua fani hii kwa sababu nikimaliza sekondari naweza kujiajiri au kusaidia nyumbani nikiona bomba limepasuka. Ujuzi huu unanifanya nijiamini,” anasema kwa tabasamu.
Chanzo cha elimu ya amali nchini kinarejea enzi za baada ya uhuru, ambapo Serikali ilihimiza elimu ya kazi na ufundi kama sehemu ya kujitegemea.
Hata hivyo, mageuzi makubwa zaidi yalionekana kupitia Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, iliyoboreshwa tena mwaka 2023, ambayo ilisisitiza kujumuishwa kwa elimu ya ufundi na amali katika shule za msingi na sekondari.
Kuna jumla ya shule 39 za sekondari mpaka sasa zinazofundisha mkondo wa amali ingawa katika miaka ya hivi karibuni, Serikali imezindua mpango wa kujenga shule 103 za sekondari za elimu ya amali kote nchini, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kujenga zaidi ya shule 500 za mafunzo ya ufundi na vyuo vya amali ifikapo mwaka 2030.
Mitalaa ya elimu ya amali inajumuisha zaidi ya fani 15 zinazogawanyika katika nyanja mbalimbali kama uhandisi wa umeme, mitambo na ujenzi, ufundi magari na usafirishaji, ushonaji na usindikaji wa vyakula, Tehama na nyingnezo.
