Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wametahadharisha kuhusu ongezeko la matumizi ya vinywaji vyenye sukari nyingi, hususani soda kwa wajawazito, wakieleza ni tishio kwa afya ya mama na mtoto.
Tafiti zinaonesha idadi ya wajawazito wanaokunywa soda mara kwa mara inaongezeka hasa mijini kutokana na urahisi wa upatikanaji wake pamoja na dhana kuwa havina madhara makubwa kiafya.
Utafiti kuhusu lishe wa mwaka 2024 uliochapishwa na Tovuti ya ScienceDirect unaonesha kuwa, vitafunwa na vinywaji vyenye sukari vinasababisha ongezeko kubwa la uzito wakati wa ujauzito.
Vilevile, unywaji mkubwa wa vinywaji hivyo unahusishwa na ongezeko la uzito la mama na kiumbe kilicho tumboni.
Utafiti huo uliofanywa kwa wanawake nchini China, umeonesha unywaji mkubwa wa vinywaji vyenye sukari una uhusiano na ongezeko la uzito wa ujauzito na uzito wa mtoto wakati wa kuzaliwa.
Hivyo, udhibiti unywaji wa vinywaji vyenye sukari ni muhimu katika kudhibiti uzito wakati wa ujauzito ambao huathiri watoto wanaozaliwa.
Utafiti mwingine kuhusu uhusiano kati ya unywaji wa vinywaji vyenye sukari na hatari ya magonjwa wakati wa ujauzito wa mwaka 2024 uliochapishwa katika tovuti ya PMC unaonesha kuwapo uhusiano wa unywaji wa vinywaji hivyo na ongezeko la hatari ya kupata kisukari cha ujauzito, shinikizo la damu la ujauzito na uzito mkubwa wa mtoto wakati wa kuzaliwa.
Mbali ya huo, mwingine kuhusu athari za unywaji wa vinywaji vyenye sukari kwa maendeleo ya kijamii na kihisia ya watoto uliochapishwa mwaka 2022 na mtandao wa Frontiers in Nutrition ulionesha unywaji mkubwa wa vinywaji vyenye sukari na vinywaji vya chai vyenye sukari wakati wa ujauzito una uhusiano na ucheleweshaji katika maendeleo ya kijamii na kihisia ya watoto wa miezi sita na 12.
Wataalamu wa afya waliozungumza na Mwananchi wameeleza ingawa soda ni sehemu ya maisha ya watu wengi, matumizi kupita kiasi wakati wa ujauzito yanaweza kusababisha madhara kwa afya ya muda mfupi na mrefu.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Agnes Mwakipesile, amesema unywaji wa soda mara kwa mara huongeza hatari ya kupata kisukari cha mimba, hali inayoweza kuathiri ukuaji wa mtoto tumboni.
“Kisukari cha mimba kinaweza kusababisha mtoto kuzaliwa mkubwa kupita kawaida, jambo linaloongeza uwezekano wa mama kupata uchungu wa muda mrefu au kujifungua kwa upasuaji.”
Mbali na hilo, amesema soda pia huongeza hatari ya upungufu wa madini muhimu mwilini, hasa kalisiamu na chuma, jambo linaloweza kuchangia upungufu wa damu kwa mjamzito na udhaifu wa mifupa kwa mtoto anayekua.
“Mjamzito anapokunywa soda mara kwa mara, kiwango cha sukari mwilini huongezeka haraka. Hii inaweza kusababisha matatizo kama mtoto kuzaliwa mkubwa kupita kawaida, uzito kupita kiasi kwa mama na hata shinikizo la damu,” amesema.
Kwa upande wake, Dk Jesca Massawe, amesema soda moja ina kati ya vijiko vinane hadi 12 vya sukari, hivyo unywaji wake kupita kiasi huweza kumsababishia mama kupata ugonjwa wa kisukari au shinikizo la damu la kudumu hata baada ya kujifungua.
“Mjamzito anayekunywa soda nyingi sukari yake inaweza kupanda ghafla au kushuka ghafla na hii inaweza kumsababishia kupata kichefuchefu, ikumbukwe kitu anachokula mama ndicho anakula mtoto, hivyo unaweza kumsababishia mtoto asiwe na ukuaji mzuri wa ubongo na mifupa,”
Kwa upande wake, mtaalamu wa lishe, Fadia Nnko amesema vinywaji vingi vya aina hiyo havina virutubisho vinavyohitajika katika kipindi cha ujauzito.
“Soda haina vitamini, madini, au protini muhimu. Kinyume chake ina sukari na kemikali zinazoweza kuathiri mfumo wa homoni wa mtoto. Wajawazito wanapaswa kuzingatia majisafi, juisi za matunda asilia au maziwa,” amesema.
Baadhi ya wanawake huchagua soda zisizo na sukari wakiamini ni salama. Hata hivyo, mtaalamu wa lishe ameonya kuwa soda hizo mara nyingi huwa na vionjo vinavyoweza kuathiri figo za mama na ubongo wa mtoto.
Hata hivyo, mtaalamu huyo wa lishe akinukuu utafiti uliochapishwa katika Jarida la American Journal of Clinical Nutrition amesema wanawake wanaotumia soda za ‘diet’ mara kwa mara wana hatari kubwa ya kujifungua kabla ya wakati.
“Soda za ‘diet’ ni hatari zaidi kwa sababu kemikali zake zinachangia kuharibika kwa seli na kusababisha msukumo usio wa kawaida wa homoni. Tafiti zimeonesha pia kwamba wanawake wanaotumia soda za aina hiyo wana uwezekano mkubwa wa kujifungua kabla ya wakati,” amesema.
Licha ya tahadhari kutolewa, baadhi ya wajawazito wanasema ni vigumu kuacha kunywa soda kutokana na ladha yake na unafuu wa upatikanaji.
Neema Kasanga, mkazi wa Tabata anayetarajia kujifungua mwezi ujao (Novemba) amesema: “Mara nyingi napata hamu ya kitu chenye sukari, soda hunipa nguvu haraka. Nimejaribu kuacha lakini siwezi, hasa wakati wa joto.”
Mariam Hassan, mama wa watoto wawili mkazi wa Mbagala, amesema alikuwa akinywa soda kila siku alipokuwa na ujauzito wa mtoto wake wa kwanza, lakini baadaye aligundua kuwa mtoto alizaliwa na uzito mkubwa.
“Madaktari waliniambia nisinywe tena sana. Kwa ujauzito wa pili niliamua kutumia maji mengi na juisi za matunda, nilijisikia vizuri zaidi na sikupata matatizo yoyote wakati wa kujifungua,” amesema.
Happiness John, mfanyabiashara wa vinywaji Muhimbili, amesema soda ndizo kinywaji kinachonunuliwa zaidi na wajawazito.
“Wengi huja na hamu ya kitu cha baridi au kitu chenye sukari. Hata kama wanajua si nzuri, bado husema aah! leo moja tu na mimi kama mfanyabiashara siwezi kumzuia asinywe,” amesema.
Mzigo wa kiafya, kiuchumi
Wataalamu wamesema athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya soda kwa mjamzito huongeza pia mzigo wa kifedha kwa familia na mfumo wa afya.
Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2024 inaonesha wagonjwa wa kisukari cha mimba na shinikizo la damu wakati wa ujauzito huongeza gharama za matibabu kwa wastani wa asilimia 20 hadi 30.
“Kila chupa ya soda inayonywewa na mjamzito inamaanisha gharama zaidi kwa matibabu, lishe na wakati mwingine upasuaji wa dharura wakati wa kujifungua,” amesema Dk Agness.
Wataalamu wanashauri elimu zaidi kutolewa kwa jamii kuhusu athari za vinywaji vyenye sukari, hasa kwa wajawazito.
Pia, wanashauri mashirika yasiyo ya kiserikali kuanzisha kampeni za uhamasishaji kwenye vituo vya kliniki ili kuwafundisha kina mama namna ya kuandaa vinywaji asilia vyenye virutubisho.
Katika hilo, mtaalamu wa lishe Fadia anasisitiza familia ina jukumu kubwa katika kumsaidia mjamzito kuepuka soda.
“Ujauzito ni kipindi nyeti kinachohitaji uangalizi wa hali ya juu katika chakula na vinywaji. Soda haipaswi kuwa sehemu ya mlo wa kila siku wa mjamzito. Kuepuka soda si jambo la kujinyima, bali ni uwekezaji katika afya ya maisha ya baadaye ya mama na mtoto,” amesema.
“Mume au ndugu wa karibu anaweza kusaidia kwa kumwandalia juisi za matunda au kumkumbusha kunywa maji, mbogamboga na matunda badala ya soda. Ujauzito ni safari ya pamoja, si ya mama peke yake, hivyo anapaswa kuangaliwa kuhakikisha anapata virutubisho muhimu na si vinginevyo,” amesema Fadia.
