VIONGOZI WA DINI IKUNGI WAOMBA WANANCHI KUSHIRIKI KWA AMANI UCHAGUZI MKUU KESHO

Askofu Philemon Nyika wa Kanisa la International Evangelism Church Ikungi, mkoani Singida, akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini Wilaya ya Ikungi walipokuwa wakitoa tamko la kuwaomba wananchi kushiriki kikamilifu uchaguzi mkuu utakaofanyika kesho Oktoba 29, 2025.

Na Mwandishi Wetu, Ikungi

VIONGOZI wa Dini Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wametoa tamko la kuwaomba wananchi wote wa wilaya hiyo kushiriki kikamilifu kwa Amani uchaguzi mkuu utakaofanyika kesho Oktoba 29, 2025.

Tamko hilo wamelitoa Oktoba 27, 2025 wakati wakizungumza na waandishi habari na kueleza kuwa Oktoba 29 kila baada ya miaka mitano ni siku ya uchaguzi mkuu wa kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini wenzake Askofu Philemon Nyika wa Kanisa la International Evangelism Church Ikungi alisema wakiwa kama walezi wa maadili, amani na mshikamano katika jamii wanatoa tamko hilo kuhamasisha wananchi wote wa Wilaya ya Ikungi na Tanzania kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo.

“ Kupiga kura ni haki ya kila mtu kikatiba na ni wajibu wa kizalendo, tunawasihi wananchi wote waliojiandikisha wajitokeze kwa wingi kesho Oktoba 29, 2025 kwenda kupiga kura,” alisema Askofu Nyika.

Aidha Askofu Nyika aliwataka wananchi kufanya maamuzi ya busara na ya haki kwa kuchagua viongozi wanaoamini watawatumikia kwa uadilifu huku wakitambua kwamba kura ni haki yao na kulinda amani ya nchi ni wajibu wa kila mmoja wetu.

Askofu Nyika alisema kudumisha amani ni msingi wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiroho, hivyo wanawakumbusha wananchi wote kwamba tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa chanzo cha chuki, migawanyiko, maandamano na vurugu siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi na visipewe nafasi kwa sababu amani ni zawadi kutoka kwa Mungu isichezewe hata kidogo.

“Sisi Viongozi wa dini kutoka Wilaya ya Ikungi tutaendelea kuliomba taifa letu liendelee kuwa na utulivu, mshikamano, upendo na tunawasihi waumini wetu waendelee kuiombea nchi yetu ya Tanzania,” alisema Askofu Nyika.

Kwa upande wake Sheikh wa Wilaya ya Ikungi, Abdi Selemani alisema tunapoenda kupiga kura kesho jambo la kwanza ni kuangalia amani ya nchi yetu kwani amani ni tamko lililotoka kwa Mungu na ni jambo kubwa sana.

“Tuna wasihi wananchi wa Wilaya ya Ikungi na Tanzania kwa ujumla kuendelea kuitunza amani hii tuliyopewa na Mwenyezi Mungu, “ alisema Sheikh Selemani.

Sheikh Selemani aliwaomba wananchi wote waliojiandikisha kupiga kura kesho Oktoba 29, 2025 kwenda kufanya hivyo kwani ni haki yao na wasipofanya hivyo watakuwa wamejinyima haki hiyo.

Naye Askofu Jeremia Samuel wa Kanisa la The Free Pentecostal Church Of Tanzania Jimbo la Ikungi, alisema kesho Oktoba 29, 2025 ni jukumu la kila Mtanzania aliyejiandikisha kujitokeza kwenda kupiga kura kwa ajili ya kumchagua Rais wetu, wabunge na madiwani.

“Kwa bahati nzuri vyama vyote vilivyoshiriki kampeni tumewaona wagombea wao walivyoshiriki kunadi sera za vyama vyao hivyo imetupa urahisi wa kujua ni nani wa kuweza kutuongoza katika taifa letu hivyo ni wito wetu viongozi wa dini kwenu kesho Oktoba 29, 2025 mjitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura,” alisema Askofu Samuel.

Viongozi wa dini walioshiriki katika mkutano huo ni kutoka Jumuiya Zawwiyyatul Qaadiriyya Tanzania (JZQT) ambayo,ni muungano wa mazawiyya yote ya Tanzania, Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), The Free Pentecostal Church Of Tanzania, Kanisa la CPCT na Aswar Suna

Sheikh wa Wilaya ya Ikungi, Abdi Selemani akizungumza kwenye mkutano huo.

Askofu Jeremia Samuel wa Kanisa la The Free Pentecostal Church Of Tanzania Jimbo la Ikungi, akichangia jambo kwenye mkutano huo.

Viongozi wa dini Wilaya ya Ikungi wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano huo.

Viongozi wa dini wa Wilaya ya Ikungi waliopata fursa ya kuzungumza kwa niaba ya wenzao. Kutoka kushoto ni Sheikh wa Wilaya ya Ikungi, Abdi Selemani, Askofu Philemon Nyika wa Kanisa la International Evangelism Church Ikungi na Askofu Jeremia Samuel wa Kanisa la The Free Pentecostal Church Of Tanzania Jimbo la Ikungi.

Viongozi wa dini wakiwa kwenye mkutano huo.

Mkutano huo ukiendelea.

Viongozi wa dini wakiwa kwenye mkutano huo.

Viongozi wa dini wakiuombea uchaguzi uchanyike kwa Amani hapo kesho Oktoba 29, 2025.