WAKILI MNDEME AFUNGA KAMPENI ZA UBUNGE KIGAMBONI

………………….

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kigamboni kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo Wakili Mwanaisha Mndeme, amehitimisha kampeni zake za Ubunge  kwa kishindo katika Uwanja wa Mzimu, Vijibweni.

Mgeni rasmi kwenye mkutano huo wa kufunga kampeni akiwa ni Kiongozi wa Chama hicho Ndugu Dorothy Semu.

Wakili @mwanaisha__mndeme amehaidi  mageuzi makubwa katika miundombinu, huduma za jamii na uchumi wa wananchi wa Kigamboni endapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo.

Katika hotuba yake ya kufunga kampeni, Mndeme aliahidi kuhakikisha tozo za kulipia Daraja la Mwalimu Nyerere zinaondolewa, ili wananchi wa Kigamboni wanufaike zaidi na miundombinu hiyo muhimu. Aidha, alisema ataisimamia serikali katika kuhakikisha  vivuko vinakuwa vya uhakika, salama na bei nafuu kwa watumiaji pamoja na uhakika wa miundombinu bora ya barabara.

Akizungumzia sekta ya uchumi wa wananchi, Mndeme aliahidi kuwawezesha wavuvi, bodaboda na mama lishe kupitia mikopo nafuu, mafunzo ya ujasiriamali na upatikanaji wa masoko bora.

Katika sekta ya afya, alisema ataweka mkazo kwenye kuboresha zahanati, kuongeza upatikanaji wa dawa na huduma za uzazi salama katika kila kata ya Kigamboni. Aidha, aliahidi kuimarisha elimu kwa kuhakikisha uwepo wa  madarasa, madawati na vifaa vya kujifunzia, pamoja na kuwapatia vijana mafunzo ya ufundi na fursa za ajira.