Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kibiti Bw.Denis Kitali leo Oktoba 26,2025 ameongoza mafunzo kwa watendaji wa vituo (Wasimamizi wa Vituo na Wasimamizi Wasaidizi wa Vituo) ambayo yanafanyika kwa siku mbili hadi Oktoba 27,2025.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo Bw.Kitali amewaasa watendaji hao kutekeleza kazi hiyo ya usimamizi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo mtakayopewa hadi hapo tutakapokamilisha jukumu hili la uchaguzi mkuu.

‘’ Dhamana mliyopewa ya kusimamia zoezi la kupiga kura na kuhesabu kura, ikiwa ni sehemu ya usimamizi na uratibu wa uchaguzi wa Rais na wabunge wa Jamhuri ya Muungano na madiwani kwa Tanzania Bara ni kubwa, nyeti na muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu. Hivyo, mnategemewa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo mtakayopewa hadi hapo tutakapokamilisha jukumu hili la uchaguzi mkuu’’

Katika hatua Nyingine Bw.Kitali amesema kuwa, uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kikatiba na kisheria ambazo hupaswa kufuatwa na kuzingatiwa hasa katika ngazi ya kituo ambapo mchakato wa kupiga kura na kuhesabu kura huendesha na hatimaye, matokeo ya uchaguzi kwa kiti cha Rais, Ubunge na Udiwani ndio yanapoanzia.

Hatua na taratibu hizo ndio msingi wa uchaguzi huru na wa haki na hatimaye kupunguza au kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.Mafunzo haya yanajumuisha wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa vituo 1,175 watakaofanya shughuli za uchaguzi katika vituo 381 vilivyopo katika kata 16 za Halmashauri ya Wilaya Kibiti.
Related
