Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Chato Kaskazini na Chato kusini, Abel Manguya, akizungumza na vyombo vya habari
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chato,Mandia Kihiyo akizungumza na vyombo vya habari
………………….
CHATO
MKURUGENZI mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita, Mandia Kihiyo, amewaomba watumishi wa halmashauri hiyo kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya kesho kwa kuwa ni haki yao kikatiba.
Hatua hiyo itasaidia kuwachagua viongozi bora wanaofaa kwa maendeleo ya taifa.
Amesema kupiga kura ni takwa la kikatiba na kwamba wananchi wote wenye sifa zilizoainishwa kisheria hawana budi kutimiza azma hiyo ambayo hutokea kila baada ya miaka mitano.
Akizungumza na vyombo vya habari ofsini kwake leo Oktoba 28,mwaka huu, Kihiyo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuruhusu siku ya Oktoba 29, mwaka huu kuwa ya mapumziko ili watu wote waweze kushiriki haki yao ya kikatiba.
“Ninawasihi sana watumishi wote wa halmashauri yetu ya wilaya ya Chato wajitokeze kwa wingi kesho ili wapige kura kwa viongozi wanaoona wanafaa kwaajili ya maendeleo ya taifa” amesema Kihiyo.
Hata hivyo amewasihi kurejea majumbani mwao baada ya kumaliza kupiga kura ili kusubiri matokeo ya ushindi kwa watakao kuwa wameibuka kidedea.
Kwa upande wake Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Chato Kaskazini na Chato kusini, Abel Manguya, amesema maandalizi ya Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani nchini yanakwenda vizuri.
Hata hivyo amesema Tume huru ya taifa ya Uchaguzi (INEC) imezingatia umuhimu wa makundi maalumu katika upigaji kura ikiwemo watu wenye ulemavu, wajawazito na wazee ambao watapewa kipaumbele.
Kadhalika amekitaja kisiwa cha Mulila kilichopo kata ya Muungano kuwa jitihada za mapema zimefanyika kuhakikisha vifaa vyote vya Uchaguzi vinafika eneo hilo mapema ili kutoa fursa kwa wananchi kutimiza haki yao ya msingi pasipo kikwazo chochote.
Manguya amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki suala zima la Uchaguzi kwa madai ni takwa la kikatiba.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 8 (A) inasema “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya jamii, na kwahiyo wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake kutoka kwa wananchi”.
Katiba pia inaongeza kuwa, Lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi, serikali itawajibika kwa wananchi na wananchi watashiriki katika shughuli za serikali yao kwa mujibu wa masharti ya katiba hii.
Aidha Manguya, amesema mchakato wa upigaji kura, kuhesabu na kutangaza matokeo utakuwa wazi hivyo wananchi wasiwe na hofu ya namna yoyote katika kuwachagua viongozi wawapendao.
Jumla ya vituo 820 vimeandaliwa kwaajili ya kupiga kura katika vijiji 115 vilivyo kwenye Kata 23 za majimbo ya Chato Kaskazini na Chato kusini.
Mwisho.


