Fyatu afyatuliwa kupenda ‘kupendwa’ na kusifiwa!

Mfyatuko wa leo si wangu. Hata kama ni wangu, si wangu. Hayo tuyaache. Msomaji na shabiki wangu mmoja aliniandikia yafuatayo, nami nikaona nishare nanyi. Sharing is caring. Fyatu huyu aliandika: Kuna mafyatu wana ugonjwa wa ukosefu wa ubunifu kiasi cha kugeuzwa wadudu. Mafyatu, sorry, wadudu hawa wana silaha moja tena ya hovyo. Nayo ni kujikomba, kusifia hata ujinga, kujigongagonga, kutabiri upuuzi, kuimba pambio na mashairi tena wamuimbiaye akiwa kipofu na taahira. Je, hapa tatizo ni nini? Ni wale wasifuo au wale wasifiwao au wote? Kwani, nani asiyejua? Kizuri huwa chajiuza na kibaya chajitembeza?

 Sijui sijui na kama najua sijui hali halisi! Sijui kwanini fyatu huyu aliniandika maneno ambayo naona kama hayanihusu au hanielewi, au niseme. Aliamua kunichafua na kunichafulia sifa nzuri ya kutopenda kufisiwa. Fyatu sitaki wala sihitaji kusifiwa tena wanafiki na wasaka tonge ambao wanaweza kukugeuka hata kukuuza wakati wowote wakiahidiwa na maadui zako tonge kubwa kuliko uwapalo hata kama ni uongo. Asiyejua hili ajue. Anayejua akupuuzia ajue. Anajipuuzia mwenyewe. Onyo, si kila wakusifuo wanakusifu. Wengi wanakuramba kichogo na kukugeuza bunga wakutumie na wakishafanikiwa, unatupwa kama diaper achia mbali ganda la muwa ambalo, lau, sisizimizi waweza kurirudufu.

Wanakuponda wakikudanganya wanakupenda wakati ukweli mchungu ni kwamba wanakuchukia. Kahaba huwa hapendi wateja wake bali mifuko yao fedha. Zikiisha, nawe unaisha. Uliyedhani anakupenda, anaweza kukulinganisha hata na kaburi. Ukimpenda fyatu vilivyo na kimakweli ni wamwamba ukweli hata kama wauma siyo kuuma na kupuliza.

Kitimoto ni kiti fire hata apakwe blusher. Juhaa ni juhaa hata aitwe mjuvi. Kiti fire ni mchafu tu hata apakwe mafuta na kufukizwa ubani na utuli. Fisi ni fisi hata avishwe ngozi ya kondoo. Cha hovyo ni cha hovyo hata kisifiwe vipi bado kibaki kuwa hovyo. Sijui kama kuna mashonde au ushuo (zi) mzuri. Sijui na sitaki hata kujua. Ubaya ni ubaya hata uitwe uzuri hauishi ubaya wake. Urongo ni urongo hata uitwe ukweli na kuaminika bado ni uongo. Hakuna uongo mbaya kama kuwadanganya wengine halafu nawe ukajidanganya. Isitoshe, hakuna uongo wa kudumu bali ukweli.

 Ni mpumbavu apangaye kupaka rangi upepo. Sikieni maneno haya ya mwenye akili lau yawaweke huru. Mtumwa awe wa kujituma au kulazimishwa ni mtumwa. Tofauti ni kwamba mtumwa wa kulazimishwa anaweza kujikomboa ilhali yule wa hiari anachukia na kuogopa ukombozi. Huyu, hana tofauti na kuku atagaye mayai na kulishwa nafaka kavu ilhali mayai yake yenye virutubisho yakiliwa na wengine. Mbwa hulinda mali lakini yu maskini daima. Sindano hushona nguo ila siku zote i uchi. Ngoja niachie hapa kupiga kelele kimya kimya na kuwaza kichini chini.

Hakuna mashindano mabaya na ya hovyo kama fyatu kushindana mwenyewe. Unajiuliza. Unapowaua au kuwazuia wapinzani wako kuingia uwanjani mshindane ukashindana na ombwe, kweli unashindana au unajidanganya? Huwezi kuniandikia haki halafu ukaziua na kunifanya nizipate zikawa haki. Hii si haki bali dhihaka. Woga ni ugonjwa mbaya ambaye humfanya mwoga kujifanya shujaa wakati ni mwoga. Kuna wakati mafyatu wasiofyatuka wakafyatua wanaogopa hata vivuli.

Asiyejua wala kuchelea kesho hana tofauti na maiti. Unawezaje Kutenda mabaya ukategemea mema? Unawezaje kuumiza wenzako nawe usiumizwe hata kama si leo wala kesho. Watenda maovu wanajua uovu wao. Hata hivyo, japo wanajua matokeo ya uovu huu, wengi hujifanya hamnazo na kujitoa akili wakidhani siku yao haitafika. Wenya akili sawa sawa huwapenda wanaowakosoa na kuchukia wanaowasifia ujinga na uongo. Heri akulaumuye kwa haki kuliko akusifuye kwa hila. Kwani, hawapo? Jana, walimsifu fulani. Leo wanambagaza.

Walijifanya wanampenda. Leo, wanamchuuza tena kwa sababu ya sifa na udohoudoho. Hao ndiyo mafyatu wasiofyatuka. Wanaweza kukukweza nawe ukakwea usijue watakushusha kwa aibu!

Ndugu zanguni ogopeni sifa. Sifa za uongo ni mbaya kuliko hata upupu kwani, waweza kuoga ukakutoka. Sifa za wenye hila ni kaburi la wamsifiaye. Kwani, humpotosha na kumdanganya akapotoka, akadanganya na kujidanganya.

Waweza kudhani mko pamoja kumbe kila mtu ana safari yake. Wapo wanaokupaka mafuta kwa mgongo wa chupa ili unogewe wakupige visu. Tumeyaona au tunajisahaulisha?

Ukiona mchugaji anamsifia ng’ombe unono, ujue ana mpango wa ima kumuua au kumuuza. Kuku hata alale kwenye kitanda, bado ni kuku. Atayarunda humo. Nani awezaye kumfuga swila asimng’ate. Heri swila swila kuliko swila mdudu. Kunyamaza si ujinga na kusema sana si busara. Kuna wakati fyatu anapaswa kukubali kujisuta kabla ya kusutwa.

Heri ajisutaye kuliko asutwaye japo kote ni kusuta. Ni kiziwi pekee asiyesikia wala kufaidi muziki. Ni kipofu pekee asiyehitaji mwanga. Nondo ni mdudu wa ajabu. Huona moto na kujitupa mwenyewe akidhani anaota moto.

Hayo ndo yalinikuta mwenzenu toka kwa moja wa mafyatu wangu katika kaya yangu niitawalayo, Fyatuland.

Onyo, usione wamenyamaa ukadhani hawajui chafu yako hata kukuzushia. Du! Hivi niko wapi?