Leo ndio siku ile ambayo Watanzania tulikuwa tukiisubiri kwa hamu kubwa. Siku yetu ya kushiriki kidemokrasia uchaguzi wa viongozi wetu watakaotupeleka kwenye hali bora zaidi ya huko tulikotoka.
Tukio kama la leo lilifanyika miaka mitano iliyopita, na litakuja kujirudia miaka mitano inayokuja. Wengi tumelisubiri kwa hamu kama wana wa Israel walivyokuwa wakimsubiri masihi kwa kufuatia utabiri.
Walioshiriki zoezi hili mara kadhaa wanaona kama mambo yanakwenda yakijirudia. Yamekuwa ni mazoea ya Watanzania kuuchukulia uchaguzi kama mwanzo mpya.
Kwamba baada ya hali ngumu, watakuja watu aidha walewale au wengine, wataahidi kwa kupitia mikutano ya kampeni kwamba wamekuja kuyarekebisha.
Na kwamba safari hii wana mbinu mpya za kuweka mambo sawa.
Huku mtaani kila anayesikia ahadi hizi anaondoka na lake. Wapo wanaopata matarajio makubwa yanayoweza kumtia mtu tamaa ya mafanikio. Hawa wanategemea kujengewa viwanda, na kupata huduma zote bure.
Lakini wengine wanakariri kuwa baada ya uchaguzi, ahadi nyingi zinaenda likizo ndefu kusubiri uchaguzi unaofuata. Hao ndio wanaowaza “labda safari hii” au “labda mgombea yule” katika kila msimu.
Matatizo ya Watanzania ni mengi kiasi cha kutoweza kuelezeka kwa siku moja. Kama yalivyo maisha, kila siku ina changamoto zake.
Kuna changamoto zilizoanza kabla ya siku hiyo, kuna zilizozaliwa na changamoto za kale, na pia kuna zingine mpya kabisa zinazoibuka.
Ni kama ngoma isiyoisha; kila mzunguko una midundo mipya. Jana ilikuwa maji, leo ni barabara, kesho ni afya, keshokutwa ni bei ya sukari.
Haya matatizo hufanana kama ndugu wa familia moja. Ukilitatua moja, mengine matatu yanakuja kuziba pengo kwa kupokezana. Waswahili husema “haba na haba hujaza kibaba,” na ndio yanayotokea. Kibaba sasa kimejaa na tunashidwa kuzifikia punje za chini. Bora ingelikuwa “bandubandu” tungemaliza gogo, sasa tungekuwa tunasubiri matatizo mapya yaibuke ili tushughulike nayo.
Tanzania haina shida kubwa kama zilivyo nchi zingine zenye majangwa, ukame, matetemeko ya ardhi, mafuriko ya mfululizo na kadhalika.
Badala yake nchi imetunukiwa kila aina ya utajiri kwa maana ya madini na kadhalika. Tena kwa bahati nzuri wakazi wake ni wasikivu na wanaoishi kwa kuvumiliana.
Pamoja na kutokubaliana juu ya mambo fulani, wanaitikia miito ya kudumisha amani na utulivu huku wakitafuta suluhu ya matatizo yao.
Muda mfupi kutoka sasa matangazo ya washindi wa mbio za uchaguzi yatatolewa. Washindi watakuwa viongozi wetu kwa awamu ingine ya miaka mitano.
Viongozi hao wanatarajiwa kuziishi ahadi zao na kutorudia makosa yaliyofanywa mwanzoni. Makosa makubwa ni ya baadhi ya viongozi wasiotimiza wajibu wao ipasavyo. Yale yote wanayoyasema kwenye kampeni hubaki kuwa ngazi ya kuwafikisha kwenye matamanio yao.
Nakumbuka kauli ya Rais wa Kwanza wa nchi hii, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Katika moja ya hotuba zake alisema; kila kitu kitawezekana baada ya kila mmoja kutimiza wajibu wake.
Kiongozi hatakiwi kulala fofofo na kudhani matatizo yatakuja kwa miadi. Akeshe akishughulika na matatizo ya awali kabla hayajazaa mengine. Hii itamsaidia kushughulikia matatizo mapya kabla nayo hayajaanza uzazi.
Baada ya uchaguzi, viongozi watapata nafasi ya kujikita kwenye mapambano dhidi ya mabadiliko ya kiulimwengu. Namaanisha wawe na utamaduni wa kuyamaliza matatizo kwa wakati.
Hivi sasa tuna mengi mapya kama ukuaji wa kasi wa teknolojia na mabadiliko ya hali ya nchi. Haya yanahitaji uwajibikaji kamilifu kwa sababu hayatawaachia muda wa kushughulikia changamoto zilezile za ukosefu wa maji, afya na elimu.
Wagombea wote wameshajinadi kwa uwezo wao. Sasa ni jukumu la mwananchi ni kutumia haki yake ya kikatiba. Amebakiwa na kazi ya kumchagua yule unayemwona ana nia ya dhati ya uwezo wa kuongoza njia. Asimchague kwa sababu ya kulipa fulana, kofia au wali wa kampeni. Achague mtu mwenye nia ya kweli ya kumvusha mtoni, si yule atakayemwacha katikati ya maji kisha ampungie mkono kutoka ng’ambo.
Kwako mpigakura; ukiona mgombea hakufai achana naye kwa heri. Kamwe usijiingize kwenye mkondo wowote wa uvunjifu wa amani.
Jitazame nafsi yako na ukumbuke kuwa una watu wanaokuhusu na kukutegemea. Si uungwana kuwafanya nao wateseke kutokana na maamuzi yako binafsi.
Usisahau kwamba mzigo wa mwisho uko mikononi mwako. Wewe ndiye unayeamua nani awe dereva wa Taifa lako, na nani ashuke kituo cha pili.
Nasisitiza kwa wale ambao wagombea wao hawatashinda, tafadhali tulieni.
Msilete nogwa wala msipige kelele kana kwamba dunia imeanguka. Demokrasia siyo vita, ni maridhiano. Wa wenzenu akishinda leo, kesho anaweza kushinda mtu wenu. Chukulieni yote kwa utulivu kwani mwisho wa siku, tunabaki Watanzania wale wale wenye upendo, utani, na imani kwamba kesho itakuwa bora.
Kwa hiyo, Watanzania wenzangu, leo tuvae nyuso za tabasamu. Tukumbuke kwamba demokrasia siyo tu kupiga kura, bali ni maisha ya kawaida. Tustahimili baada ya matokeo kama vile hakuna kilichobadilika. Ukiona mambo yamekuwa kinyume na matarajio yako wala usikufuru.
Mshukuru Mungu na useme “aliyeshinda anatosha”. Maisha mengine hayana budi kuendelea baada ya jambo hili kupita.
