UONGOZI wa TRA United upo katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato wa kupata kocha mkuu wa kuinoa timu hiyo ambapo kwenye mchujo yamebaki majina mawili tu.
Ipo hivi; baada ya mabosi wapya wa timu hiyo kupokea maombi ya takribani makocha 500 walioomba kazi ya kufundisha kikosi hicho, mchujo umefanyika na sasa ni vita ya makocha wawili Etienne Ndayiragije na Mecky Maxime.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya TRA United kimeliambia Mwanaspoti kuwa mchakato unaendelea vizuri na wakati wowote mmoja kati ya makocha hao wawili waliobaki kwenye mchujo ndio atakayekuwa kocha mkuu.
“Ni kweli mchakato ulikuwa mgumu kutokana na wingi wa maombi ya makocha waliojitokeza kuomba kazi ya kuinoa timu yetu, hadi sasa tumebakiwa na makocha hao wawili, mmoja kati yao ndiye atakayepewa mikoba ya kuiongoza timu yetu.
“Kutokana na matokeo mabaya ambayo timu yetu inayapata, tunahitaji umakini zaidi kutafuta kocha ambaye ataitoa timu kwenye nafasi mbaya iliyopo na kuipambania iweze kufikia malengo tuliyojiwekea tangu mwanzo wa msimu.”
Chanzo hicho kilisema haitakuwa rahisi kwa kocha huyo lakini wanaamini mipango mikakati iliyopo itamuongoza kuipambania timu ili kufikia malengo wanayoyakusudia.
TRA United msimu huu imecheza mechi tatu za Ligi Kuu Bara, imekusanya pointi tatu baada ya kuambulia sare zote, ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo kati ta timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo.
Maxime tangu aachane na Dodoma Jiji mwishoni mwa msimu wa 2024-2025, amekuwa hana timu ya kuifundisha. Kocha huyo amewahi kuzinoa Mtibwa Sugar na Kagera Sugar katika Ligi Kuu Bara.
Kwa upande wa Ndayiragije, msimu uliopita aliipa Kenya Police ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya. Si mgeni wa soka la Tanzania kwani amefundisha KMC, Azam, Mbao na Timu ya Taifa ya Tanzania.
TRA United ambayo zamani ilifahamika kwa jina la Tabora United, tangu msimu uanze imekuwa haina kocha mkuu ikiongozwa na kocha msaidizi, Mkenya, Kassim Ottieno.
Msimu uliopita timu hiyo ilimaliza nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikifundishwa na makocha wanne, akianza Mkenya, Francis Kimanzi, kisha Mkongomani Anicet Kiazayidi anayeifundisha Azam akiwa msaidizi wa Florent Ibenge baada ya kuondoka akatua Mzimbabwe Genesis ‘Kaka’ Mangombe. Aprili 18, 2025 akatangazwa Kocha Mzambia Simonda Kaunda kuchukua nafasi ya Mangombe hadi mwisho wa msimu wa 2024-2025.
