Chadema Yatoa Taarifa Kuhusu Makamu Mwenyekiti Wao, John Heche – Global Publishers



Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa taarifa kwa umma kuwa leo, Alhamisi tarehe 28 Oktoba 2025, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa,  John Heche, amechukuliwa na askari wa Jeshi la Polisi kutoka kituo cha Polisi cha Mtumba kwa madai kuwa anahitajika na RPC wa Dodoma.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, tukio hilo lilitokea mbele ya mke wake pamoja na Katibu wa Kanda ya Kati, Bi. Ashura Masoud. Walipojaribu kufuatilia ili kujua wanapompeleka, magari yaliyombeba yaliongeza mwendo na kuwaacha nyuma.

Baadaye, walipofika kwa RPC wa Dodoma walielezwa kuwa RPC hana taarifa yoyote kuhusu kumhitaji Mh. Heche. Hadi sasa, haijulikani alipo huku familia yake na Chama kimebaki na wasiwasi mkubwa juu ya usalama wake na wapi alipo.

CHADEMA imeeleza kuwa, inamtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camilius Wambura, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Ramadhan Kingai, Mkuu wa Polisi Mkoa (RPC) na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtumba watoe maelezo ya haraka kwa umma kuhusu mahali alipo na hali ya usalama wa Mheshimiwa John Heche.