Dk Mwinyi na kiapo bila hotuba
Unguja. Dk Hussein Ali Mwinyi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) anakuwa miongoni mwa marais wachache wa Zanzibar ambao hawakuhutubia siku ya sherehe za uapisho wao, kama ilivyokuwa kwa baba yake, Ali Hassan Mwinyi mwaka 1984.
Katika sherehe za uapisho wa Dk Mwinyi zilizofanyika Uwanja wa New Aman Unguja, visiwani Zanzibar, kiongozi huyo hakuhutubia baada ya kiapo, kama ambavyo aghalabu inafanywa na marais baada ya kula kiapo.
Tukio hilo la Dk Mwinyi, linakumbusha enzi za urais wa baba yake, Ali Hassan Mwinyi mwaka 1984, ambaye pia baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar, hakuhutubia siku hiyo.
Dk Mwinyi aliapishwa kuviongoza visiwa hivyo Novemba mosi, 2025 hafla iliyohudhuriwa na maelfu ya wananchi wa Zanzibar na wawakilishi wa mataifa mbalimbali.
Hatua ya kuapishwa kwake, imetokana na kiongozi huyo kushinda katika uchaguzi mkuu wa visiwani humo, kwa kupata kura 448,892 sawa na asilimia 74.8 ya kura zote.
Mpinzani wa karibu wa Dk Mwinyi, Othman Msoud Othman wa ACT- Wazalendo alipata kura 139,399 sawa na asilimia 23.22 kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
ZEC ilitangaza waliojiandikisha kupiga kura visiwani humo ni 717,557 lakini waliopiga kura 609,096 sawa na asilimia 84.88. Kati ya kura hizo zilizoharibika ni 8,863 sawa na asilimia 1.46.
Ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2020, Dk Mwinyi ameshuka kwa asilimia mbili, mwaka huo alipata asilimia 76.27 dhidi ya aliyekuwa mshindani wake wa karibu wa ACT-Wazalendo, hayati Maalif Seif Sharif Hamad ambaye alipata asilimia 19.87.
Wagombea wa vyama vingine na kura walizopata ni Laila Rajab Khamis wa NCCR- Mageuzi kura1,643, Juma Ali Khatib wa Ada- Tadea 1,455, Ameir Hassan Ameir wa Makini 1,435 na Hamad Rashid Hamad wa ADC 1,345.
Wengine ni Mfaume Khamis Hassan wa NLD kura 1,301, Hamad Mohamed Ibrahim wa UPDP 1,299, Said Soud Said wa AAFP 1,238, Khamis Faki Mgau wa NRA 1,161 na Hussein Juma Salim wa TLP kura 1,065.
Hotuba baada ya kutangazwa
Hotuba pekee iliyotolewa na Dk Mwinyi ni baada ya kutangazwa kuwa mshindi na ZEC akisema yupo tayari kufanya kazi na kila mmoja kwa masilahi ya Taifa na maendeleo ya nchi hiyo.
Alisema inawezekana wakati wa kampeni wamesema na kuumizana kwa sababu ndio demokrasia ilivyo kila mmoja kusaka nafasi hiyo, lakini kwa kuwa wamemaliza uchaguzi, wanapaswa kuunganisha nguvu zao pamoja kujenga Taifa na yeye atakuwa Rais wa wote bila kubagua.
“Ndugu zangu uchaguzi ndio umeisha tena, basi nawaomba tukubali kupokea matokeo haya, maana wananchi wameamua na haya ndio uamuzi wao hatuwezi kuupinga.
“Ninawaomba wagombea wote na vyama vyao wakubaliane matokeo, nitapata nafasi tena baadaye kuzungumza nao, inawezekana kipindi cha kampeni tulitajana na kukwaruzana, lakini tunapaswa kuweka masilahi ya umma mbele,” alisema.
Akitumia fursa hiyo pia, aliwashukuru wagombea hao na wananchi kwa jumla kuonesha ukokavu wa kisiasa kwa kuwa, tangu mchakato wa uchaguzi ulipoanza, kupiga kampeni, kupiga kura hadi kutangazwa mshindi hakuna uvunjifu wa amani wowote uliotokea.
“Nimatarajio yangu kwamba, amani tuliyonayo tutaidumisha, Mwenyezi Mungu atudumishe katika amani tuliyonayo,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya wagombea wengine, aliyekuwa mgombea wa ADC, Hamad Rashid alisema uchaguzi umeisha, hivyo wanapaswa kuwa wamoja na kumpa ushirikiano aliyeshinda ili kuendelea kuijenga Zanzibar.
Baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, Othman aliwataka wanachama wa chama hicho kutulia wakati viongozi wakiendelea kutafakari.
Uchaguzi huo ulioshirikisha vyama 11 vya siasa, Dk Mwinyi wa CCM, aliibuka kidedea kwa kupata asilimia 74.8 ya kura zote zilizopigwa huku Othman akipata asilimia 23.22.
Akizungumza na viongozi na baadhi ya wanachama katika ofisi za chama hicho Vuga, Oktoba 31, 2025, Othman alisema licha ya kutokubaliana na matokeo hayo, lakini hawana budi kuwa na utulivu.
“Ndugu wanachama, tunaona yaliyotokea lakini niwaombe tutulie wakati viongozi tukiendelea kushughulikia jambo hili,” alisema.
Othman alisema jambo lolote litakalofanyika lazima watawashirikisha wanachama na hakuna uamuzi watakaoamua bila kupata baraka za wanachama.
“Kama ambavyo kila kinachofanyika tunakuwa kwenu kuomba ridhaa, hata hili hakuna uamuzi utakaotolewa na sisi viongozi, lazima tutakuja kwenu na ninyi mtakachokiamia ndio tutakachotekeleza,” alisema Othman.
Wakati ACT – Wazalendo wakisema hayo, CCM iliwashukuru na kuwapongeza wananchi wote kwa kuchagua viongozi wao kwa kura nyingi na kuendelea kuiweka madarakani.
Katibu wa Kamati Maalumu, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama hicho Zanzibar, Khamis Mbeto alisema chama hicho kinavikaribisha vyama vingine washirikiane kujenga uchumi wa Zanzibar.
“Tumeshinda kwa kishindo, hii ni kuonesha kwamba, mgombea wetu alikuwa anakubalika, lakini inaonesha jinsi ambavyo CCM imetekeleza ilani yake kwa asilimia kubwa, hivyo ikajenga imani kwa wananchi, uchaguzi umeisha sasa ni wakati wa kuendelea kuijenga nchi,” alisema Mbeto.
Majimbo waliyopoteza CCM na kuchukuliwa na ACT – Wazalendo ni Mtambile, Shumba, Ole, Wete, Gando, Mtambwe, Pandani, Wingwi na Tumbe na Ziwani.
Ilivyokuwa siku ya uapisho
Katika hafla ya uapisho iliyofanyika Novemba mosi, mwaka huu viongozi mbalimbali walihudhuria sherehe hiyo, wakiwamo kutoka mataifa mbalimbali.
Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na maelfu ya wananchi na wafuasi wa CCM. Hakukuwa na mbwembwe nyingi zaidi ya kukagua gwaride la kumaliza muhula wake wa kwanza.
Baadaye akala kiapo kisha kwenda kukagua gwaride la kuanza muhula wake wa pili wa awamu ya nane.
Hatua hiyo, ilihitimisha sherehe hizo na kila mtu akatawanyika.