Ligi Kuu Bara, Championship kurejea Novemba 8

Ligi Kuu Tanzania Bara itarejea Jumamosi, Novemba 8, 2025 baada ya kusimama kwa muda hivi karibuni, huku wadau mbalimbali wakichekelea.

Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na ile ya Championship zilisimama kwa muda katika kipindi cha Uchaguzi wa Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kusimamishwa kwa Ligi Kuu kulisababisha kutochezwa kwa mechi kadhaa ambazo zilipangwa kuchezwa ndani ya muda huo wa siku sita.

Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Karim Boimanda amesema kuwa baada ya serikali kuruhusu shughuli ziendelee kama kawaida, Ligi itarejea mwishoni mwa wiki hii.

“Ligi Kuu tunarudi pia Novemba 8. Championship mizunguko inayofuata pia inachezwa. Mechi zilizoahirishwa zitapangiwa tarehe za mbele,” amesema Boimanda.

Mchezo wa TRA United dhidi ya Simba ulipangwa kuchezwa Oktoba 30, 2025, siku ambayo pia ilipangwa iwe ya mechi baina ya Azam FC na Singida Black Stars.

Mbeya City inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi nane ilizokusanya katika mechi sita.

Pointi hizo nane pia ndizo za Dodoma Jiji FC ambayo ipo katika nafasi ya pili baada ya kucheza mechi sita za Ligi.

Mechi ambazo ziliahirishwa ni TRA v Simba, Azam v Singida BS, Prisons v Yanga, Simba v Azam, Singida BS v TRA, Yanga v KMC, JKT v Simba, Namungo v Azam na Pamba Jiji v Singida BS.