Maisha yarejea baada ya hekaheka ya siku sita

Dar/mikoani. Baada ya hekaheka za siku za tano zilizosababisha wananchi kukosa huduma muhimu, sasa hali ya maisha imerejea kawaida, ikiwemo usafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Kuanzia Oktoba 29 siku ya kupiga kura na kuendelea zilizozuka vurugu na maandamano yaliyotikisa baadhi ya majiji makubwa ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Mwanza na kusababisha athari ya miundombinu ya umma, binafsi, vituo vya polisi na mafuta, magari yalichomwa moto huku baadhi ya wananchi wakidaiwa kujeruhiwa na wengine kufariki dunia.

Hali hiyo, iliyosababisha Jeshi la Polisi kutoa amri ya kuwataka kutotembea zaidi ya saa 12 jioni, huku baadhi ya barabara zikiwekwa vizuizi na Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ), usafiri wa umma haukupatikana kirahisi hata ule wa kwenda au kuingia Dar es Salaam kutoka mikoani haukuwepo. 

Ilikuwa hekaheka za watu kusaka mahitaji muhimu ikiwemo vyakula, ambapo kutokana na hali ndogo ya amani wenye maduka waliyafunga kuhofia usalama wao. Kama hiyo haitoshi, hata yale yaliyofunguliwa bei ya vyakula au bidhaa zilikuwa juu na kuleta ugumu wa maisha kwa wananchi wa kawaida.

Ingawa hali imerejea kawaida lakini kuna maumivu na kicheko. Maumivu ni  kupanda kwa gharama ikiwemo usafiri wa umma hasa daladala na baadhi ya bidhaa muhimu zinazotumika na wananchi, wakati kicheko ni pale wananchi kutoka kujitafutia riziki.

Kwa ujumla ya hali imerudi kama zamani, barabara ambazo awali zilifungwa zimefunguliwa huku wananchi wakirejea katika maisha yao ya kawaida. Hali hiyo ilichagizwa na agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuwataka wakuu wa mikoa kuhakikisha maeneo yao yanarudi katika hali ya kawaida.

Wafanyabiashara, hususan wale wadogowadogo waliokuwa wamehifadhi bidhaa zao kwa hofu ya uharibifu, sasa wameanza kurudi madukani na kufungua biashara zao. Sauti za magari, daladala, na wauzaji mitaani zimeanza kusikika tena, zikirudisha uhai wa jiji lililokuwa kimya kwa siku kadhaa kutokana na hali ya taharuki.

Ingawa athari za vurugu hizo bado zinaonekana wazi kupitia majengo yaliyoharibiwa, vioo vilivyovunjika na alama za moto katika baadhi ya maeneo ya katikati ya jiji, matumaini mapya yameanza kuonekana na mwingiliano wa wananchi wanaotoka eneo moja kwenda jingine. 

Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam, waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti walisema wameanza kuona ahueni huku wakiendelea kurejea kwenye utaratibu wa maisha ya kawaida wakati ambao Serikali imeahidi kuchukua hatua thabiti kuhakikisha usalama na kudumisha amani. 

Waandishi wa Mwananchi walitembelea maeneo ya Kariakoo, Ubungo, Buguruni, Kimara, Manzese na kushuhudia watu wakirejea katika shughuli zao kwa tahadhari lakini wakiwa na matumaini mapya. 

Wengine walionekana wakisafisha maeneo yao ya biashara, wengine wakipanga upya bidhaa zao na magari ya mizigo yakianza kusafirisha bidhaa katika maeneo ya masoko.

“Nyumbani kukaa siyo shida, tatizo hela ya kula iliisha na chakula ndani kiliisha jambo linalonifanya nikose chaguo na badala yake niamue kuja kufungua tu,” alisema Almas Nzige ambaye ni muuzaji wa kava za simu mtaa wa Congo, Kariakoo.

Kwa mujibu wa Nzige, eneo la Kariakoo limeanza kurejea katika hali yake ya kawaida, ambapo machinga wanaendelea na shughuli zao huku maduka makubwa yakisalia kufungwa na machache yakiwa wazi.

Katika maeneo mengine ya jiji la Dar es Salaam wananchi waliendelea na maisha yao ya kila siku licha ya maduka mengi ya mtaani kuendelea kufungwa tofauti na hapo awali.

Imeshuhudiwa kwenye baadhi ya mitaa wananchi wakiendelea na shughuli zao za kila siku huku wakichua tahadhari ya kiusalama kama ilivyoshauriwa kupitia tangazo la Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka lililotolewa Jumatatu (juzi) iliyopita.

Baadaye, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilitangazwa kufutwa kwa zuio lililokuwa likiwataka wananchi wa jiji la Dar es Salaam kuwa ndani ifikapo saa 12 jioni ambalo liliwekwa awali.

Hali hii imefanya sasa baadhi ya huduma kuanza kufunguliwa ikiwemo vituo vya mafuta ambavyo awali vilikuwa vimefungwa kwa hofu ya kushambuliwa na waandamanaji sambamba na kuchomwa moto. 

Hatua hii ya kufunguliwa kwa vituo vya mafuta kumeanza kuchochea sekta ya usafirishaji iliyokua imedorora kufuatia baadhi wamiliki kufunga vituo hivyo kwa kuhofia usalama wa mali zao, huku baadhi ya wamiliki vyombo vya uchukuzi yakiwemo magari ya abiria maarufu daladala, bajaji na pikipiki za biashara ‘bodaboda’ zikirejea .

Hata hivyo, gharama za usafiri zimepanda kutoka za awali huku waendeshaji wa vyombo hivyo wakidai ni kutokana na gharama ya mafuta kupanda hadi kufikia lita moja kuuzwa kwa Sh5,000 hadi Sh10,000 kwa njia za kificho.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwenye vituo vilivyofunguliwa umeonesha bei imebaki ileile ya awali, ingawa waendeshaji wa vyombo vya usafiri wa umma wameongeza gharama ya nauli bila kuzingatia maelekezo kutoka mamlaka husika.

“Mafuta yalipoadimika na bei kupanda hata nauli nazo zilipanda kwa sababu huduma lazima ziendelee lakini huwezi kuendesha chombo bila mafuta. Nauli ilipoongezeka ilikuwa ni ngumu kwa watu kumudu kwa sababu hawakuwa wakifanya kazi kuingiza kipato,” alisema Lyimo Mkazuzu.

Lyimo alisema wakati kazi zinasimama wao walikuwa hatarini zaidi kwani licha ya kuwa usafiri uliotegemewa lakini walikuwa hatarini kushambuliwa na waandamanaji.

Mwendokasi ulinzi waimarishwa

Wakati vituo vya mwendokasi vikiwa sehemu ya vile vilivyoshambuliwa zaidi ulinzi umeimarishwa ambapo askari zaidi ya sita wamewekwa katika kila kituo.

Askari hao ambao walivalia sare zao za kazi walikuwa wamebeba silaha za moto huku wakionekana kudumisha ulinzi huku wakiendelea kupata baadhi ya huduma ikiwemo chakula walichokuwa wakisambaziwa.

Askari hao waliwekwa katika vituo vya mwendokasi vilivyopo katika barabara ya Morogoro hadi Kimara huku wakiwa wengi zaidi katika kituo cha Ubungo ilipokuwa stendi ya mabasi zamani sehemu ambapo mabasi ya mwendokasi yalichomwa moto.

Wakati askari wakilinda vituo hivyo, wanajeshi waliovalia sare walikaa karibu kila makutano ya barabara jijini hapa wakiwa juu ya magari na wengine wakiwa wamesimama, huku wakiwa wamebeba silaha zao ili kuhakikisha ulinzi unaimarishwa.

Maisha katika majiji na miji

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, amewahakikisha wananchi wa mkoa huo pamoja na wageni wakiwemo watalii kuwa hali ya usalama ni shwari na

huduma za msingi zote zinapatikana.

Makalla amesema timu maalumu iliyoundwa mkoani humo inaendelea kupita maeneo yote yaliyoathirika na vurugu zilizotokea kuanzia Oktoba 29.

“Kwa sasa Arusha ni shwari na salama, vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kuhakikisha usalama unakuwepo muda wote na ili huduma za kijamii na kiuchumi ziendelee kama kawaida,”

“Kuanzia Novemba Mosi maduka yalifunguliwa ili  kutoa huduma na leo shughuli zote zinaendelea kama kawaida. Arusha ni mkoa wa biashara na utalii, tumewahakikishia usalama wageni wetu wanaokuja,” alisema Makalla.

Kuhusu usafiri, Makalla aliwahakikishia watoa huduma za usafirishaji kuwa hali imeimarika hivyo waendelee kutoa huduma hizo kwa wananchi.

“Tumejadili kwenye kikao, vituo vyote vya mafuta viko wazi na tumeelekeza waagizaji na wafanyabiashara wa mafuta Arusha kuendelee kuagiza mafuta kwa wingi ili kupatikana wakati wote,” alisema Makalla.

Katika Soko la Samunge wafanyabiashara wamerejea huku wananchi wakijipatia mahitaji muhimu ya nyumbani.

Mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo, Mary John alisema baadhi ya bidhaa zimepanda bei kutokana na gharama za usafirishaji kuongezeka.

“Huwa nanunua kiroba cha ngogwe (nyanya chungu) kwa Sh50,000 lakini sasa hivi zinauzwa Sh70,000 hivyo wateja wetu wawe wavumilivu hadi hali itakaporejea kawaida,” alisema Mary.

Mkazi wa Kwamrombo jijini humo, Joseph Mushi aliiomba Serikali kuingilia kati bei ya usafirishaji akidai zimeongeza gharama za maisha na wamiliki wa daladala, bajaji na bodaboda wanaopanga bei kulingana na matakwa yao bila kuzingatia kipato cha watumiaji.

“Kutoka Kwamrombo hadi Mjini nauli ni Sh1,000 badala ya Sh600 wanasema mafuta yamepanda sababu vituo vya mafuta vimefungwa,” alisema Mushi.

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia vijana 11, wakiwemo wawili wanaodaiwa kuhamasisha maandamano kupitia mitandao ya kijamii huku tisa wakituhumiwa kujihusisha na uchomaji wa matairi wakati wa uchaguzi wa Oktoba 29, mwaka huu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani taratibu za kisheria zitakapokamilika, akisema polisi lina ushahidi dhidi yao.

“Kabla ya uchaguzi kulikuwepo na watu waliokuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuhamasisha maandamano siku ya uchaguzi, tunawashikilia kwa ushahidi tulionao, na hatua hiyo ilisaidia kupunguza kasi ya vurugu,” alisema Kamanda Maigwa.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema hali ya usalama katika mkoa huo imeendelea kuwa shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku bila uvunjifu wa amani, baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu 

 “Uchaguzi umekwisha, Rais ameshaapishwa. Nitoe wito mtu yeyote anayefikiria kufanya jambo lolote la uvunjifu wa amani hilo sasa halihusiani na uchaguzi, atakuwa mhalifu kama mwingine.”

“Nitoe wito kwa watumishi na watendaji wote wa serikali wawahudumie wananchi na kumaliza changamoto zao. Watatue matatizo yao, nitashirikiana na viongozi wengine kuendelea kushughulikia changamoto zitakazojitokeza,” alisema mkuu huyo wa mkoa.

Alitumia pia nafasi hiyo, kumtaka Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) mkoani humo, kuhakikisha hakuna upandaji wa nauli kiholela, watakaobainika hatua kali zichukuliwe dhidi yao.

Hata hivyo, baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Moshi, nauli zimepanda kutoka Sh1,000 hadi Sh2,000 kwa bajaji na bodaboda Sh5,000 badala ya Sh2,000 ya awali.

Mkoani Mbeya wananchi wa mkoa huo, wampongeza Rais Samia kutokana na hotuba yake aliyoitoa wakati akiapishwa Novemba 3 jijini Dodoma.

Maclina James alisema uamuzi wa Rais Samia kuelekeza shughuli zirejee ulikuwa wa huruma na busara kwa kuwa wananchi wengi wanapata riziki pale wanapotoka.

Kwa mujibu wa James, siku tano za kukaa ndani bila shughuli ziliwapa wakati mgumu ilihali majukumu ni mengi, ikiwemo ada za watoto shuleni, chakula na gharama nyingine za uendeshaji maisha.

“Unakaa ndani hadi unachoka, kuna muda unaanza kupishana kauli na familia yako kwa kuwa mtu amezoea kutoka kila siku, sasa akishinda nyumbani anaona mambo tofauti,” alisema James.

Imeandikwa na Aurea Simtowe (Dar), Filberty Rweyemamu (Arusha) na Janeth Joseph, Flora Temba (Moshi)