Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemtangaza Kocha Miguel Gamondi kuwa kaimu kocha mkuu wa timu ya taifa (Taifa Stars), akichukua nafasi ya Hemed Suleiman ‘Morocco’.
TFF imetangaza mabadiliko hayo baada ya kufikia makubaliano ya kusitisha mkataba na kocha Morocco, ambaye alikabidhiwa jukumu la kuiongoza Stars, kufuatia kuondoka kwa kocha Adel Amrouche raia wa Algeria.
Taarifa ya TFF imeeleza kuwa, makubaliano ya kusitisha mkataba yamehusisha pande mbili, yaani TFF kwa upande mmoja na Kocha Morocco kwa upande mwingine.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa uamuzi wa kumtangaza Gamondi kuwa kaimu kocha mkuu wa Taifa Stars, umefikiwa baada ya kufanyta mazungumzo uongozi na Singida Black Stars kuhusu Kocha huyo kuchukua majukumu hayo mapya.
Kocha Gamondi ndiye atakayeiongoza Taifa Stars kwenye Fainali za AFCON zitakazofanyika nchini Morocco kuanzia Desemba mwaka huu.
