Yanga yapewa Waarabu watatu, Simba yatupwa Kundi D Ligi ya Mabingwa

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika, leo Novemba 3, 2025 limechezesha droo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Yanga imepangwa Kundi B wakati Simba ikiwa Kundi D.

Droo hiyo iliyofanyika Johannesburg nchini Afrika Kusini ikiongozwa na wanasoka wa zamani barani Afrika, Cristopher Katongo wa Zambia na Alexander Song kutoka Cameroon, Yanga katika Kundi B itakabiliana na Waarabu watatu ambao ni mabingwa mara 12 wa michuano hii, Al Ahly ya Misri, AS FAR (Morocco) na mabingwa mara mbili wa Afrika, JS Kabylie kutoka Algeria.

Kwa upande wa Simba, itakutana na Mwarabu mmoja, Espérance Sportive de Tunis kutoka Tunisia ambao ni mabingwa mara nne Afrika. Zingine ni Petro de Luanda (Angola) na Stade Malien (Mali).

Katika michuano hii, kutakuwa na mechi ya kusisimua na ya kihistoria kati ya mabingwa watetezi Pyramids FC ya Misri na wababe wa Morocco, RS Berkane. Timu hizi zilikutana katika CAF Super Cup na Pyramids kuwa mabingwa ikishinda 1-0.

Hatua hii inaonekana kuwa na ushindani mkubwa kutokana na aina ya timu zinazoshiriki.

Kundi A linatajwa kuwa na mvuto zaidi  kutokana na uwepo wa RS Berkane ambao ni mabingwa wa Kombe la Shirikisho msimu uliopita 2024-2025 na Pyramids, mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika 2024-2025.

Rivers United ya Nigeria na Power Dynamos ya Zambia zinakamilisha kundi hilo lenye mvuto mkubwa.

Kundi C linawaweka washiriki wa kudumu Mamelodi Sundowns dhidi ya Al Hilal, MC Alger na St Éloi Lupopo, timu zenye historia ndefu na mashabiki wa dhati.

Hatua ya makundi itaanza mwishoni mwa wiki ya Novemba 21 na 23, 2025, huku michezo miwili ikichezwa kabla ya kuanza kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 nchini Morocco.

Mashindano yataendelea tena mwishoni mwa wiki ya Januari 23 na 25, 2026 baada ya kumalizika kwa michuano ya AFCON. Hatua ya mtoano (knockout) itaanza Machi 13, 2026.

Bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika atapokea Dola za Marekani milioni 4 (Sh9.8 bilioni), huku mshindi wa pili akipokea Dola za Marekani milioni 2 (Sh4.9 bilioni).

MAKUNDI YA LIGI YA MABINGWA AFRIKA 2025/26

Kundi A: RS Berkane (Morocco), Pyramids FC (Misri), Rivers United (Nigeria), Power Dynamos (Zambia)

Kundi B: Al Ahly (Misri), Yanga (Tanzania), AS FAR (Morocco), JS Kabylie (Algeria)

Kundi C: Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Al Hilal (Sudan), MC Alger (Aljeria), St Éloi Lupopo (DR Congo)

Kundi D: Espérance Sportive de Tunis (Tunisia), Simba SC (Tanzania), Petro de Luanda (Angola), Stade Malien (Mali)