Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally ndiye atamsaidia Miguel Gamondi katika benchi la ufundi la timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Gamondi alitangazwa jana kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars baada ya mkataba wa Hemed Suleiman ‘Morocco’ kusitishwa.
Habari kutoka chanzo cha uhakika ndani ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeithibitishia Mwananchi Digital kuwa Ahmad Ally ndiye atamsaidia Gamondi katika kipindi ambacho atakuwa anakaimu nafasi hiyo.
“Msaidizi wa Gamondi atakuwa ni Ahmad Ally wa JKT Tanzania. Kuna mambo yanawekwa sawa kisha itatangazwa rasmi lakini kwa muda mfupi uliopo kabla ya AFCON, mtu sahihi tumeona awe Ahmad Ally,” kilifichua chanzo hicho.
Katika msimu huu, Ahmad Ally ameiongoza JKT Tanzania katika michezo mitano ya Ligi Kuu ambapo imevuna pointi saba, ikipata ushindi mara moja na kutoka sare nne.