Athari za maandamano zilivyopaisha bei za bidhaa

Mwanza. Shughuli za kiuchumi kusimama, maduka kufungwa na wananchi kushindwa kununua mahitaji yao licha ya kuwa na pesa mikononi au kwenye simu, ndiyo hali iliyokumba baadhi ya maeneo ya mikoa ya kanda ya ziwa baada ya vurugu zilizotokea kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba mosi, 2025.

“Hali ilikuwa kama sinema. Kwa mara ya kwanza nilishinda njaa mimi na watoto wangu,”anasimulia mkazi wa Bwiru, Salome Jacob kuhusu athari za vurugu zilizotokea katika maeneo yao kwa siku tatu mfululizo.

Anasema asubuhi ya Oktoba 29,  hali ilikuwa shwari, kuna waliokwenda kupiga kura na wengine kwenye biashara zao ndogo ndogo, lakini ilipofika saa mbili usiku, hali ikabadilika ghafla, milio ya mabomu na risasi vilitawala.

“Yaani nilianza kujuta kwa nini sikuhemea vyakula…nikaanza kujipa moyo huenda kufikia asubuhi vurugu na risasi zinazorushwa zitakuwa zimeisha, lakini haikuwa hivyo, asubuhi hali ya risasi na mabomu viliendelea.

“Ndani nilikuwa na unga kidogo wa uji wa mtoto wangu wa chekechea, tukakoroga na kunywa, mchana tulishinda njaa, fikiria mtoto wa miaka minne anashinda njaa,”anasema Salome.

Anasema pesa ya kununua chakula alikuwa nayo, lakini pakununua ndiyo ilikuwa changamoto, hali ilikuwa hatari kiasi kwamba, maduka na magenge yote yalikuwa yamefungwa.

“Tulishinda njaa hadi baadaye jirani yangu alivyonishtua kuwa, mama kulwa anauza katika kibanda chake kwa siri, ndipo mfanyakazi wangu alipojitoa muhanga kwenda kununua,  ndiyo tukala usiku wa saa sita,”anasema.

Katika maeneo mengi ya mikoa ya Mwanza, Kahama, Shinyanga, Geita na Mara hali ilibadilika na gharama ya maisha kupaa baada ya vyombo vya ulinzi kutuliza vurugu.

Katika mikoa hiyo, amri ilitolewa ya watu kuingia ndani au kutoonekana barabarani kuanzia saa 12 jioni, huku bidhaa nazo zikipanda bei kwa kasi.

“Bidhaa nyingi zimepanda bei,  wengine tuna tabia ya kutunza pesa kwenye simu..kama unavyoona mawakala wamefunga vibanda vyao, kwa hiyo mtu una pesa, lakini huwezi kuitoa na kuitumia,” anasema Msekwa Haruna mkazi wa jijini Mwanza.

Kwa upande wa jijini Mwanza, vurugu zilitofautiana kulingana na maeneo, sehemu nyingine ikiwamo Kisesa zilianza Oktoba 29 na maeneo mengine zilianza Oktoba 30.

Hata hivyo, baada ya kutulizwa mahitaji ya binadamu ikiwamo chakula na usafiri vilipanda bei, huku pakununua kukiwa changamoto, kwa kuwa wafanyabiashara walikuwa wakiuza kwa kificho kama wanauza bidhaa haramu.

Kutokana na hali hiyo, bei ya nyama ilipanda kutoka Sh9,000 hadi Sh18,000 kwa kilo moja huku mchele ukipanda kutoka Sh2,300 hadi Sh3,500 kwa kilo moja.

“Siyo mchele tu na maharagwe vilivyopanda, sasa tunanunua mchicha Sh500 kwa fungu moja wakati tulikuwa tunanunua mafungu matatu kwa bei hiyo,” anasema Hamida Zephania mkazi wa Bulale.

Mama lishe nao wamepandisha bei, ugali kwa dagaa au maharagwe, ulikokuwa unauzwa Sh1,000 sasa unauzwa Sh2,500 huku wali wa maharagwe kati ya Sh2,500  hadi Sh3,000 kulingana na wingi wa wateja.

“Kwa kweli hali imekuwa ngumu, hizi siku mbili (Oktoba 31 na Novemba mosi, 2025) imenilazimu nifunge tu, kula ni nyumbani maana siwezi kutoa Sh3,000 kula wali maharagwe wakati wali ulikuwa Sh1,500,” anasema Bakari Juma, dereva bodaboda Mkolani, Mwanza.

Pia, bei ya usafiri imepanda,  sehemu iliyokuwa inatozwa Sh1,000 sasa ni Sh5,000 na sehemu za Sh2,000 bei ni kuanzia Sh7,000 hadi Sh10,000 kulingana na hali ya usalama na upatikanaji wa mafuta siku hiyo.

Mikoa mingine ya kanda ya ziwa

Mkoani Geita, baada ya vurugu zilizodumu kwa siku tatu, zikianza Oktoba 29, 2025 katika Mji wa Katoro, hali ikawa mbaya zaidi Oktoba 30 zikasambaa mpaka Nyankumbu Geita eneo lenye watu wengi na linalotegemewa na Manispaa.

Oktoba 31  hali ilianza kuwa tulivu na leo Novemba 3 watu wameanza kutoka mchana huu japo shughuli hazijarejea.

Bidhaa mkoani humo zimepanda bei, ukiwamo mchele umepanda kutoka Sh2,400 hadi  Sh 3,500, nyama imepanda kutoka Sh11,000 hadi Sh16,000 na dagaa kisado kilichokuwa kikiuzwa Sh12,000 kinauzwa Sh17,000.

Fungu moja la mihogo mitatu linalouzwa Sh1,000 linauzwa Sh2,000  katika Soko la Nyankumbu la jumla kwa mtaani bei ilikuwa hadi Sh1,000 kwa mhogo mmoja.

Mkoani Shinyanga, Wilaya ya Kahama usafiri wa boda boda kwa kawaida ni  Sh1,000 lakini sasa hivi Sh5,000 na sehemu ya kwenda kwa Sh2,000 ni Sh10,000.

Mboga za majani, fungu lililokuwa linanunulia Sh100 sasa hivi Sh200 hadi Sh300, huku karoti hazipo kabisa sokoni, nyanya zilizokuwa zinauzwa nne kwa Sh500 sasa hivi mbili Sh500, pilipili hoho zilizokuwa zinauzwa nne kwa Sh500 sasa hivi ni tatu au mbili.

Shinyanga mjini, mchele umepanda bei kutoka Sh2,800 hadi Sh3,500 kwa kilo, nyama ya ng’ombe ikipanda kutoka Sh12,000 hadi Sh15,000.

Mkoani Simiyu katika soko la mjini Bariadi kilo moja ya mchele ilikuwa ikiuzwa Sh2,000 lakini kutokana na hali ilivyo sasa ni Sh3,000, nyama ambayo kilo moja mchanganyiko ilikuwa ikiuzwa kwa Sh10,000 sasa imepanda hadi Sh14,000.

Vyakula vibichi kama vile viazi mbatata vimepanda kutoka Sh1,000 kwa kilo moja hadi kufikia Sh2,000, unga wa sembe ulikuwa unauzwa kilo moja Sh2,000 sasa ni Sh3,000.

“Mzunguko wa pesa umekuwa mdogo kutokana na baadhi ya taasisi za kifedha zikiwamo benki kutofunguliwa na hata mashine za kutolea fedha hazifanyi kazi; wananchi wanazuiwa kufika kwenye majengo ya benki,” anasema Mashinde Kija, mkazi wa Bariadi.

Vyakula katika hoteli na migahawa, bei imepanda; sahani ya wali pamoja na maharagwe iliuzwa kwa Sh1,500 kwa sasa bei ni Sh2,500.

Mikoa ya Tabora, Kagera na Kigoma hali imeendelea kama kawaida, japo viungo vimepanda bei mikoa ya Tabora na Kagera, ndizi zimeadimika Bukoba na kupanda kutoka Sh10,000 hadi Sh20,000 kwa mkungu mmoja kutokana na magari ya mizigo yaliyokuwa yanazifuata Karagwe na kwingineko mkoani humo kusitisha safari.

Mkazi wa Manispaa ya Bukoba, Mkoa Kagera na mfanyabiashara ndogo ndogo, Royce Kaijage  anasema tangu machafuko na vurugu vitokee katika maeneo mbalimbali, ndizi zimekuwa changamoto.

Mkoani Tabora karoti, hoho na nyanya chungu zimepanda bei, awali karoti nne hadi tano kubwa zilikuwa Sh1,000 lakini sasa zinauzwa Sh2,000.

Hoho ndogo ilikuwa ikiuzwa kwa Sh100 na kubwa tatu kwa Sh500 lakini kwa sasa moja kubwa ni Sh300 au mbili kwa Sh500 huku nyanya chungu zilikuwa zikiuzwa 12 kwa Sh500, kwa sasa zinauzwa  saba kwa Sh500.

Kwa upande wa upatikanaji wa mafuta kwa ajili ya vyombo vya moto bado ni changamoto, Tabora kwa kuwa, mpaka sasa vituo vya mafuta vimefungwa, hivyo kusababisha vyombo vingi vya moto kushindwa kufanya safari zake hasa boda boda.

Mohamedi Mazimba, mwendesha boda boda anasema mafuta hayapatikani na kwa sasa nauli imeongezeka mara mbili.

Katika vurugu zilizotokea, baadhi ya maduka yamevujwa kisha bidhaa kuporwa.

Miongoni mwa maduka yaliyovunjwa ni ya vifaa vya kielektroniki zikiwamo simu, televisheni na kompyuta mpakato (laptop) kisha vifaa hivyo kuibwa.

“Kama unavyoona duka langu ni la simu, limevunjwa na hakuna simu hata moja. Wameniachia msiba, mtaji wote wameuiba, nina mkopo sijui maisha yangu yatakavyokuwa,” anasema mfanyabiashara wa duka la simu Buhongwa jijini Mwanza baada ya duka lake kuvunjwa.

Pamoja na maduka kuvunjwa, ofisi na majengo ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika baadhi ya maeneo mikoa ya kanda ya ziwa, vituo vya polisi na vituo vya kuuzia mafuta yalivamiwa na kuchomwa moto.