Wabunge wote Wateule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wametakiwa kufika katika Ofisi ya Bunge Dodoma kwa ajili ya shughuli za usajili na taratibu nyingine za kiutawala zitafanyika kuanzia tarehe 8 hadi 10 Novemba, 2025 kabla ya kuanza kwa mkutano wa kwanza wa Bunge la 13.
Taarifa ya leo Novemba 5, 2025 iliyotolewa na Katibu wa Bunge, Baraka Leonard imeeleza kuwa wito huo wa Wabunge wote wateule umekuja kufuatia Tangazo la Rais lililotolewa kwenye Gazeti la Serikali toleo maalumu Na. 11 la Novemba 4, 2025 lililoeleza kuwa kikao cha kwanza cha mkutano wa kwanza wa Bunge jipya kitafanyika Novemba 11, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, miongoni mwa shughuli zitakazofanyika katika mkutano huo ni pamoja na kusomwa kwa Tangazo la Rais la kuitisha Bunge, uchaguzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uapisho wa Wabunge wote.
Shughuli nyingine ni kuthibitisha uteuzi wa Waziri Mkuu, uchaguzi wa Naibu Spika na ufunguzi rasmi wa Bunge jipya utakaofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Katibu wa Bunge amesisitiza kuwa Wabunge Wateule wote wanapaswa kufika wakiwa wamevaa mavazi rasmi na wakiwa na nyaraka muhimu zikiwemo hati ya kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge, Kitambulisho cha Taifa, Kadi ya Benki yenye namba ya akaunti, cheti cha ndoa (kwa waliooa au kuolewa), vyeti vya kuzaliwa vya watoto (kwa walio na watoto), vyeti vya elimu vilivyothibitishwa, pamoja na wasifu binafsi.

Related
