CAF yaongeza timu za WAFCON

KAMATI Kuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imeidhinisha kuongeza idadi ya timu zitakazoshiriki mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) kutoka timu 12 hadi 16, kuanzia toleo lijalo litakalofanyika nchini Morocco kuanzia Machi 17, 2026 hadi Aprili 3, 2026.

Kwa kuwa hatua ya kufuzu kwa toleo la mwaka 2026 tayari imekamilika, Kamati Kuu imeidhinisha utaratibu maalum wa kuchagua timu nne za ziada zitakazokamilisha orodha ya washiriki.

Kwa mujibu wa viwango vya sasa vya ubora vya FIFA kwa timu za wanawake, timu nne zilizoorodheshwa juu zaidi kati ya zile zilizotolewa kwenye raundi ya mwisho ya kufuzu zimechaguliwa kukamilisha idadi hiyo.

Timu hizo ni Cameroon (nafasi ya 66 katika viwango vya FIFA), Ivory Coast (71), Mali (79) na Misri (95). Zinaungana na zile 12 ambazo tayari zimefuzu kwa fainali za WAFCON 2026 ambazo ni Morocco (mwenyeji), Zambia, Tanzania, Malawi, Algeria, Nigeria, Ghana, Burkina Faso, Kenya, Cape Verde, Afrika Kusini na Senegal.

Uamuzi huu unaendana na mkakati wa CAF wa kukuza ushindani na maendeleo ya soka la wanawake barani Afrika.

Hatua hii itaziwezesha nchi nyingi zaidi kushiriki katika mashindano makubwa ya soka la wanawake barani Afrika, hivyo kuchangia ukuaji endelevu na umaarufu wa mchezo huo duniani.

Mashindano ya WAFCON pia yanatumika kama hatua ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la Wanawake la FIFA mwaka 2027 litakalofanyika nchini Brazil.

Mapema Oktoba 2025, kabla ya raundi ya pili na ya mwisho ya kufuzu WAFCON 2026, ziliripotiwa taarifa zikidai kuwa mashindano hayo yangepanuliwa kutoka timu 12 hadi 16, ingawa hakukutolewa maelezo yoyote kuhusu mabadiliko ya muundo wa mashindano hayo. Hata hivyo, Oktoba 25, 2025, CAF lilikana madai hayo, likibainisha kwamba mchakato wa kufuzu ungetoa timu 11 kuungana na wenyeji kukamilisha idadi ya timu 12. Baadaye, ziliripotiwa taarifa kwamba CAF bado lilikuwa likifikiria upanuzi huo na Novemba 3, 2025, ilithibitishwa rasmi kupanuliwa kwa mashindano hayo kutoka timu 12 hadi 16.