Dar es Salaam. Siku moja baada ya Serikali kutangaza kusitisha huduma za mabasi yaendayo haraka (mwendokasi) jijini Dar es Salaam, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imetangaza kutoa vibali kwa daladala 150.
Daladala hizi zitatoa huduma katika ruti za Mbezi -Posta, Mbezi-Mnazi Mmoja, Mbezi- Muhimbili na Mbezi- Mnazi Mmoja.
Hatua hiyo inalenga kupunguza changamoto za usafiri, hususan katika maeneo yaliyokuwa yakitegemea huduma za mwendokasi ikiwamo ya Barabara ya Morogoro.
Hatua hiyo inalenga kurejesha uwiano wa huduma za usafiri wa umma, huku Serikali ikiendelea kufanya tathmini ya uharibifu uliojitokeza wakati wa maandamano yaliyofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025, jijini Dar es Salaam.
Huo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila Novemba 4, 2025 la kuwataka Latra kutoa vibali vya muda mfupi kwa mabasi ya kawaida ili yaweze kutoa huduma kwa njia ambazo zilikuwa zikitegemea mabasi ya mwendokasi.
Akizungumza na wanahabari leo Novemba 5, 2025 Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amesema kuanzia sasa wanatarajia kutoa vibali kwa mabasi takribani 150 ili kupunguza changamoto ya usafiri katika maeneo hayo.
Chalamila amesema vibali hivyo vitadumu kwa miezi mitatu wakati tathmini na ukarabati wa miundombinu ya mabasi ya mwendokasi ukiendelea.
“Atakayetuma maombi mapema yatashughulikiwa na kupewa kibali kwa haraka, lengo ni kuondoa changamoto ya usafiri katika maeneo hayo,” amesema.
Ametoa wito kwa wale wenye mabasi yenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 26 na kuendelea kutuma maombi ya kutoa huduma hiyo kupitia mfumo.
Ametaja ruti ambazo zitatolewa vibali hivyo ni Mbezi -Posta, Mbezi-Mnazi Mmoja, Mbezi- Muhimbili na Mbezi- Mnazi Mmoja.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Shifaya Anaselema amepongeza hatua hiyo na wapo tayari kutoa huduma katika maeneo hayo.
Anaselema amesema hadi mamlaka kufikia uamuzi huo tayari wameona uhitaji katika maeneo husika.
Amesema lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kuondoa changamoto ya usafiri katika maeneo hayo.
“Sisi tupo tayari kuwahudumia wananchi katika maeneo hayo, tunachosubiri ni kupata vigezo vinavyohitajika ili kupata kibali kutoka kwa Latra,” amesema.
Shihuka yapongeza hatua hiyo
Katibu wa Shirika la Kutetea Haki za Abiria (Shikuha), Hashim Omary amesema hatua hiyo itasaidia wanachi kuendelea kupata huduma ya usafirishaji wakati Serikali iliendelea kufanya uchunguzi na tathmini ya uharibifu ya miundombinu ya mabasi ya mwendokasi.
Amesema kinachotakiwa ni kuhakikisha wananchi katika maeneo husika hawapati adha ya usafiri wanapokwenda katika shughuli zao za kila siku.
“Ni uamuzi wa busara, unapoingia katika uchunguzi wa tatizo lililotokea huwezi kuacha wananchi wakikosa usafiri ni vyema kuruhusiwa kwa mabasi hayo ili yaweze kusafirisha abiria hadi pale huduma za mabasi ya mwendokasi zitakaporudi katika hali ya kawaida,” amesema.
Khatibu Juma, mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam ameziomba mamlaka kuharakisha mchakato wa mabasi hayo kupata vibali ili kupunguza changamoto ya usafiri iliyopo katika maeneo hayo.
“Ni vyema mabasi hayo yakaanza kutoa huduma kwa haraka maana tangu kusitishwa kwa huduma za usafiri wa mabasi ya mwendokasi hali ya usafiri imezidi kuwa changamoto,” amesema.
Naye Chiristina John, Mkazi wa Mbezi ameomba idadi ya daladala zitakazopewa vibali kuongezwa ili huduma za usafiri katika eneo hilo ziwe za uhakika.