Kilio zaidi kwa walioharibiwa mali zao kwenye vurugu

Dar es Salaam. Huenda baadhi ya wamiliki wa mali zilizoharibiwa wakati wa maandamano wasipate fidia kutoka kampuni za bima baada ya kubainika kuwa, sera za kawaida za bima hazijumuishi matukio yanayosababishwa na shughuli za kisiasa.

Mali hizo zilibaribiwa wakati wa maandamano yaliyofanyika Oktoba 29 mwaka huu yakilenga kupinga uchaguzi mkuu uliokuwa ukifanyika.

Katika maandamano hayo, baadhi ya kampuni ikiwamo za mabasi kama Shabiby, Abood na Ratco zilichomewa magari huku baadhi ya biashara ikiwamo maduka ya bidhaa mbalimbali kama simu, kamera zikivunjwa, kuchomwa moto na bidhaa zake kuibwa.

Akizungumza leo Novemba 5 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Sanlam General na Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Watoa Bima Tanzania (ATI), Khamis Suleiman amesema sera za kawaida za bima ya moto hazijumuishi vurugu za kisiasa isipokuwa mteja awe amenunua bima ya ziada inayojulikana kama Political Violence and Terrorism (PVT).


“Hapo awali, sera za moto zilijumuisha uharibifu unaosababishwa na vurugu za kisiasa, lakini kadri matukio kama hayo yalivyoongezeka duniani, kampuni za bima ziliamua kwamba, kinga hii itatolewa tu iwapo mteja atanunua bima ya ziada,” amesema Suleiman.

Pia, amesema sera za moto bado zinashughulikia uharibifu wa makusudi kama vile uchomaji moto unaotokana na chuki binafsi au migomo ya wafanyakazi yenye masilahi ya pamoja, lakini siyo uharibifu unaotokana na sababu za kisiasa.

Suleiman amebainisha kuwa, kwa Tanzania, bima ya PVT ziliuzwa zaidi wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015 kutokana na uwezekano uliokuwapo wa kutokea vurugu za kisiasa; hata hivyo, kufikia mwaka 2020 na mwaka huu, bima hizo hazikununuliwa kwa wingi kutokana na mahitaji madogo na ushindani mdogo wa kisiasa.


“Mwaka huu hakukuwa na mvutano mkubwa wa kisiasa, hivyo wafanyabiashara hawakuomba bima ya PVT. Mawakala wanashauriwa kuwaelimisha wateja kuhusu aina hii ya bima, hasa kwa wamiliki wa maduka makubwa na biashara zilizo katika maeneo yenye hatari ya vurugu mijini,” amesema.

Suleiman amesema ni asilimia sita pekee ya wateja ndiyo wanaohudumiwa na kampuni za bima na wengine wanaobakia wanapitia kwa mawakala na benki ambao ndiyo wanabeba jukumu za kuwaelimisha wateja.

Katika hilo Kamishna wa Bima, Dk Baghayo Saqware amesema watakaolipwa ni wale tu waliokuwa na bima za PVT.

“Bima inashughulikia hatari zisizokusudiwa na za asili. Uharibifu wa mali uliotokea wakati wa uchaguzi isipokuwa kwa wale waliokuwa na bima ya PVT.

 “Amani na utulivu wa muda mrefu nchini imekuwa changamoto kwa kampuni za bima kuwashawishi wateja kununua bima,” amesema Dk Saqware.

Kamishna huyo alifichua kwamba, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) itapitia upya hatari zikiwamo vurugu za kisiasa na matukio yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi, kwa kuwa zinapaswa kujumuishwa katika sera za kawaida za bima siku zijazo.

“Tumelipokea suala hili na tutalichambua kwa makini. Matokeo ya uchambuzi yatatusaidia kutoa ushauri kwa kampuni za bima kuhusu jinsi ya kubuni bidhaa zinazofaa kwa hatari mpya zinazojitokeza,” amesema.


Mkurugenzi Mtendaji wa ACCLAVIA Insurance Brokers & Risk Consultants, Dk Anselmi Anselmi, amewataka Watanzania kutafuta ushauri wa kitaalamu kuhusu bima.

“Watu wengi hupuuzia umuhimu wa ushauri wa kitaalamu. Mawakala wa kawaida huwashauri wateja kuhusu aina hizi za bima. Kinga ni bora kuliko tiba na gharama ya kujikinga ni ndogo sana ukilinganisha na hasara inayoweza kutokea bila bima,” amesema.

Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Bima ya Dexter, Optatus Costantine amesema kama maandamano yakisababisha uharibifu wa mali kama kuchomwa magari, majengo, maduka kulipwa au kutolipwa kwa hasara hizo inategemea aina ya bima aliyokuwa nayo mteja.

Hiyo ni kwa sababu maandamano yanaingia kwenye kundi la ajali ambazo si za kawaida bali ni matukio maalumu yanayohitaji ulinzi wa ziada.

“Sasa ili uweze kulipwa wateja wote wenye biashara, maghala au magari ya bima kubwa wanashauriwa kuwa na bima ya nyongeza kama PVT au ile inayoweza kukupa fidia kupitia uharibifu uliofanywa na vurugu, mgomo na ghasia za raia (Riot, Strike & Civil Commotion) amesema.

“Bima kubwa kama za magari, moto, mali hazifidii hasara zinazosababishwa na maandamano, ghasia, vurugu au uharibifu wa makusudi isipokuwa kipengele hicho kikiwa kimeongezwa kwenye bima yako.”